Mmea wa tango utatambuliwa kwa kuzaa matango yake.
Mti wa mpapai utatambuliwa kwa matunda yake ya mapapai.
Ipo mimea ya matango inazaa matango yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu lakini inafanana vilevile na matango ya kawaida yanayofaa kuliwa. Haya yasiyofaa hufahamika sana na huitwa matango pori maana ni machungu.
Ipo miti ya mipapai ambayo mingine hutoa matunda yasiyoeleweka, wengine huita mipapai dume ambapo kabla ya kuzaa huwezi kuijua.
Mkulima aonapo mapando kama haya yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu huyang’oa na kubakisha ile miti/mimea inayotoa matunda.
Tukija kiroho ndivyo ilivyo ndugu; mtumishi wa Mungu wa kweli atatambuliwa kwa matunda ya kazi yake, iwe kazi ya Bwana wetu Yesu Kristo ama ya bwana yesu mwingine itajulikana.
Mkristo anayesema ameokoka, hatuwezi kujiridhisha na kuishia hapo kuwa ameokoka, tutamtambua kwa mienendo na tabia zake. Kama ni mchanga kiroho atambulika kwa matunda ya matendo yake, kama ni msanii wa kiroho atajulikana, kama ni mkomavu kiroho na mtu anayetembea katika njia za Bwana atatambuliwa kwa matunda ya matendo yake.
Kila mmoja anajua mmea wa mahindi hutoa mahindi na si mtama/uwele, ukiona muhindi umetoa mtama/uwele ujue huo sio muhindi.
REJEA; Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Mathayo 7 : 16.
Umeona hapo neno la Mungu limeongezea kitu kingine cha msingi, huwezi kuchuma nyanya kwenye mpilipili hoho, haipo kabisa na ukiona kitu kama hicho ujue kuna pandikizi lisilo lake.
Sehemu nyingine tunaona neno likisema; Wanakiri ya kwamba wanamjua Mungu, bali kwa matendo yao wanamkana; ni wenye machukizo, waasi, wala kwa kila tendo jema hawafai. Tito 1 : 16.
Wengi wanakiri Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao, wengi wanalitumia jina la Yesu kuombea wagonjwa lakini matendo yao yanalikataa jina la Yesu Kristo.
Tupo nyakati ambazo kwa wachanga kiroho ni ngumu kutambua sehemu wanazosali zinamwabudu Mungu wa kweli ama wanaabudu miungu mingine.
Lakini neno la Mungu lipo wazi na linatuonyesha wale wenye kulikiri jina lake katika roho na kweli matendo yao ni safi mbele za watu na mbele za MUNGU.
Neno la Mungu linafungua fahamu za kila mwamini, tafakari uchukue hatua.
Samson Ernest.
+255759808081.