Sio jambo geni katika maisha yetu ya kila siku kumwona mtu akikanywa kuhusu tabia yake mbaya, mtu huyo akaja juu na kuona watu wanamwonea wivu tu wakati yeye yupo vizuri.

Haya sio mambo mageni katika maisha yetu ya siku za leo, wapo watu hawapo tayari kurekebishwa/kukanywa, wakati wote huwa wanafikiri watu wanawaonea wivu au washamba.

Watu wa namna hii huwa wanajiona wapo vizuri kwa Mungu, njia zao au matendo yao huwa wanaona yapo sawa mbele za Mungu.

Unapochukua hatua ya kumrekebisha mahali ambapo unaona hayupo sawa, anaweza kukutolea mifano mingi kukuthibitishia yupo vizuri kiroho.

Napenda kukuambia kwamba sio kila njia au sio kila matendo ya mtu anayoyaona ni mazuri machoni pake, ndio yatakuwa mazuri kweli. Mtu anaweza akajiona yupo vizuri ila mbele za Bwana yupo vibaya sana.

Haijalishi unaona njia zako ni salama, yupo Mungu ambaye huupima moyo wa mtu. Hata kama unaonekana upo vizuri kwa watu, ikiwa haupo vizuri itabaki hivyo tu.

Rejea: Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; Bali BWANA huipima mioyo. MIT. 21:2 SUV.

Huenda wapo marafiki zako wanakupigia kelele juu ya tabia fulani, huenda wapo watumishi wa Mungu wameongea sana juu ya mwenendo wako usiofaa. Lakini umewaona wanaokuonea wivu tu ila wewe upo vizuri.

Nataka nikuambie kwamba, kama kuna watu wanakusifia upo vizuri, ukiendelea kujaa kiburi siku ya mwisho Yesu atakukataa.

Unachopaswa kuelewa ni kwamba Bwana huwa haangalii kama mwanadamu anavyoangalia, kama kuna watu wanakusifia upo vizuri na wewe unajiona hivyo. Haiwezi kubadili ukweli kuwa haupo vizuri kabisa.

Rejea: Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. 1 SAM. 16:7 SUV.

Hapa Yese aliona watoto wake waliokuwepo watafaa  ila haikuwa hivyo, bali alikuwepo Daudi machungani huko ndiye Mungu alimwona anafaa na alimchagua yeye.

Mungu huutazama moyo wa mtu, kitu kama hakipo sawa kwako kitaonekana kwa matendo yako ya nje. Maana kile kiujazacho moyo wa mtu ndicho kitaonekana kwa matendo yake.

Kwahiyo mtu anaweza kuona njia zake zipo sahihi na akakataa kusaidiwa, lakini kupitia njia hizo mwisho wake ukawa mbaya sana.

Rejea: Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. MIT. 14:12 SUV.

Mwisho, sio kila njia unayoiona machoni pako ni sawa, itakuwa sawa kweli kwako, ila fahamu zipo njia utaziona ni salama kwako ila ni machukizo mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com