Utakuwa shahidi wa hili, nabii wa uongo anakubalika haraka zaidi na watu kuliko nabii wa ukweli. Nabii wa uongo anaenda moja kwa moja kwenye vitu vinavyopendwa na watu wa Dunia.
Nabii wa uongo atakuambia vaa nguo yeyote njoo kanisani, na anajua kabisa wengi wanapenda hayo. Na kuna mahali hawaruhusiwi kuvaa hivyo, sasa nabii wa uongo au mtumishi wa uongo atakuambia kuvaa hivyo haina shida.
Nabii wa uongo anajua kabisa wengi wanapenda kuachana na kuoa/kuolewa na mwanaume/mwanamke mwingine. Na anajua kuna mahali wanakatazwa kabisa kufunga ndoa ingali mke/mume wako yupo hai, yeye ataruhusu hicho kitendo kifanyike kwake.
Mchungaji, au nabii, au mtume, au mwalimu, au mwinjilisti wa uongo anajua kabisa kunywa pombe ukiwa kama mkristo ni dhambi mbele za Mungu. Kwa kuwa anajua wengi wanapenda kunywa pombe, atasema kunywa pombe haina shida, kikubwa kunywa kiasi usilewe sana kisha njoo kwenye ibada.
Na wote tunajua pombe ni pombe, haijalishi umekunywa sana au umekunywa kidogo. Bado utaitwa umekunywa pombe, na una hatia mbele za Mungu.
Mtumishi wa uongo atakuambia zaa na mwanaume/mwanamke yeyote, mambo ya ndoa baadaye. Cha muhimu wewe pata mtoto tu, anaelewa kabisa yapo makanisa huwezi kufanya hivyo, na wengi sana wanapenda tabia chafu.
Usishangae sana kuona vitu vya ajabu vinaruhusiwa na hawa manabii wa uongo, hiyo ni roho ya uongo. Roho hii ina kazi moja tu, kuendelea kuwashikilia wale watendao mabaya, ambao hawapo tayari kuachana na mabaya yao.
Usishangae kuna makanisa mabinti na wamama wanaenda kanisani wakiwa wameacha wazi sehemu kubwa ya miili yao. Inaweza ikakusumbua sana ila unapaswa kufahamu wameruhusiwa na madhabahu yao.
Usishangae kuona mamiujiza ya ajabu ajabu, yaani ya uongo, fahamu kwamba watu wengi wanapenda hayo. Sasa shetani ameingiza watumishi wake humo humo, nyie mnafikiri mnamwabudu Mungu wa kweli kumbe sivyo ilivyo.
Maandiko matakatifu yapo wazi kabisa kuhusu hili, unaweza usielewe sana kama huna Neno la Mungu ndani yako ila kama umepata nafasi ya kusoma ujumbe huu. Unaweza kuona ni jinsi gani shetani ameingiza mawakala wake kwa njia ambayo wengi tunaona ni mambo ya Mungu.
Rejea: Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa. MIK. 2:11 SUV.
Sijui kama umeona kitu hapo kwenye huo mstari, huu mstari umeeleza kitu kizito sana. Kitu kilichosemwa na huo mstari ndicho leo kinafanyika kwa wingi sana, kwa akili ya kawaida ya kibinadamu, huwezi kuelewa kabisa.
Nimependa biblia ya kiswahili cha kisasa jinsi ilivyo utafuna huu mstari, ni mstari ule ule na maana ile ile ila umeelezwa kwa kiswahili cha sasa. Tuseme lugha ya mazingira ya sasa, ambayo kila mtu anaweza kuelewa vizuri.
Hebu tuone biblia ya NENO inavyosema hili;
Rejea: Ikiwa mwongo na mdanganyifu atakuja na kusema, Nitawatabiria divai na pombe kwa wingi, angekuwa ndiye nabii anayekubalika na watu hawa! Mika 2:11 NEN.
Umeona hapo, nabii anayekubalika haraka na watu wengi, watu wanaopenda kuendelea kuishi maisha machafu. Ndio manabii wanaokubalika haraka sana.
Manabii hawa wa uongo, wanapenda kuhubiri sana mafanikio ya mwilini, wanapenda sana kusema maneno laini yenye kuwafariji watu katika uovu wao.
Nabii wa uongo hawezi kukemea dhambi, maana anajua hiyo sio kazi yake, kazi yake ni kutoa maneno mazuri na malaini tu.
Sio mimi ninayesema haya, Biblia takatifu ipo wazi kabisa kuhusu hili ninalokueleza hapa. Ukiwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu utakuwa umewahi kukutana na andiko hili;
Rejea: Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo. ISA. 30:9-10 SUV.
Umeona hapo, watu wenyewe wanataka maneno ya uongo, wanapenda kuambiwa maneno laini. Hata kama hayo maneno ni ya uongo, na baba wa uongo ambaye ni shetani amesimamia hili haswa.
Tuwe makini sana sisi kama watoto wa Mungu, kama kweli unatamani siku moja kwenda kuishi maisha ya umilele huko mbinguni. Naomba uwe makini sana nyakati hizi, hebu jichunguze mwenyewe mahali unapoabudu, wanaisema kweli ya Mungu?
Changamoto nyingine kama umefungwa ufahamu wako, itakuwa ngumu sana kuona hili. Ila Mungu wetu ni mweza wa yote, achilia damu ya Yesu Kristo kwenye ufahamu wako na mahali unaposali/unapoabudu. Lazima utaona vitu ambavyo vinapingana na Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.