Ukiwa kama mwanadamu, hutoshangaa kuhusu Yona, mategemeo ya Yona yalikuwa Mungu aangamize mji wa Ninawi.
Yona alivyoona Mungu ameghairi hukumu yake juu ya mji huo, kitendo hicho kilimkasirisha sana Yona.
Kwa ninavyofikiri hapa, mji huu wa Ninawi, watu wake walikuwa chukizo sana kwa Mungu kiasi kwamba waligeuka kero hata kwa watu wengine wacha Mungu.
Kwanini nawaza hivi, mategemeo ya Yona yalikuwa kuangamizwa kwa mji wa Ninawi. Alivyoona Mungu amebadili uamzi, kile kitendo kilimuumiza kiasi kwamba alitaka Mungu achukue roho yake.
Sawa na leo, kuna watu wanamtenda Mungu dhambi kiasi kwamba unashindwa kuelewa kwanini wanafanya hivyo bila wasiwasi.
Huenda kuna watu umeongea nao sana kuhusu habari za wokovu, badala yake wamezidi zaidi kumtenda Mungu dhambi na sio kubadilika.
Siku inafika Mungu anakutuma kwa watu wale wale uliowaeleza sana habari za wokovu hawakuta kukusikia. Mategemeo yako yalikuwa Mungu awangamize tu ili kizazi hicho kiweze kufutika kabisa.
Baada ya kupeleka ujumbe ule Mungu aliokupa, wewe unaondoka eneo hilo na kwenda eneo lingine. Huku nyuma watu wanaingia kwenye toba ya nguvu, tena toba yenye kumaanisha haswa.
Wakati wewe unaendelea kusubiri Mungu awaangamize hao watu, kumbe wenzako walienda mbele za Mungu siku hiyo hiyo. Walivyoenda mbele za Mungu, Mungu akaachilia msamaha juu yao, bila wewe kufahamu hilo.
Inafika wakati unasikia Mungu amewasamehe watu wale, hatawaadhibu tena, au hatawaangamiza tena. Alafu baada ya kusikia hivyo moyoni mwako unasikia hasira kubwa.
Katika hasira yako, Mungu atataka kukufundisha kitu kupitia hayo hayo yanayokukasirisha ndani yako. Ni sawa na wale maadui zako, Mungu anaendelea kuwanyeshea mvua kama kawaida kama anavyofanya kwako.
Mungu alivyoona Yona amekasirika sana na anataka kufa kabisa, Mungu alifanya jambo hili jangwani alipokuwa Yona.
Rejea: Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa. Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja; na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana? YON. 4:9-11 SUV.
Hapa tunaona Mungu alimwoteshea Yona mti wa mtango ili apate kivuli kizuri, baadaye ule mti ukafa. Na ulivyokufa Mungu akamsemesha Yona kupitia mti ule ule, inakuwaje anahurumia mtango kuliko watu?
Yona akaona mtango ni wa thamani sana kuliko uhai wa watu, hii ni ajabu sana, wanadamu wakati mwingine huwa tunafanya mambo mpaka Mungu anatushangaa.
Hii ipo hadi leo, mtu yupo tayari kuua ndugu yake ili apate mali, yupo mdada anakubali kutoa mimba na kuua kiumbe kisicho na hatia kabisa. Kwa ajili tu ya maslahi yake binafsi.
Unaweza kuona kuna mtu yupo tayari kumsaliti mume/mke wake wa ndoa kwa kudanganywa na mwanaume/mwanamke mpita njia tu. Anaona huyo ndio anafaa kuliko mume/mke wake wa ndoa, akasahau agano lake na mume/mke wake.
Mungu anaweza kukuadhibu kwa jambo dogo sana likakuumiza zaidi moyo wako, ujue hapo Mungu anataka kukufunza jambo katika maisha yako. Haijalishi wewe ni mtumishi mzuri sana, kama kuna vitu havimpendezi Mungu kwako, atakuadhibu tu.
Tuwe makini sana, ndio maana ni vizuri kuwa na Neno la Mungu la kutosha mioyoni mwetu. Maana kuna vitu tunaweza kusubiri Mungu avifanye kwa wale tunaoona wanalichafua jina la Yesu Kristo. Mungu akafanya tofauti kabisa na vile tulikusudia mioyoni mwetu.
Mungu atusaidie sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.