Adui yako anaweza akawa magonjwa yanayokusumbua katika mwili wako, magonjwa yanayokunyima raha ya kufurahia maisha yako.

Adui yako anaweza akawa kukata tamaa, kila ukijaribu kujipa moyo, kila ukijaribu kusahau kumbukumbu mbaya zinazochangia kukuvunja moyo. Unaona bado kuna mzigo ndani yako wa kukata tamaa, huyo ni adui yako.

Adui yako anaweza akawa hali ngumu ya uchumi wako, umekandamizwa kwenye eneo hilo kiasi kwamba huna nafasi ya kuhema/kupumua sawasawa.

Adui yako anaweza akawa mtu anayekutakia mabaya kila siku, anatamani upate shida ngumu ili moyo wake ufurahie.

Adui yako anaweza akawa ofisini kwako, anayetamani uanguke ili yeye ashike nafasi yako. Anafanya kila juhudi za kukuletea fitina ili uondolewe kwenye nafasi yako.

Adui yako anaweza akawa ni yule anayetamani watoto wako washindwe kwenye masomo yao, washindwe kutunza ujana wao waoe/waolewe bila utaratibu.

Adui yako anaweza akawa yule anayejitahidi kuwagombanisha na mke/mume wako ili mwachane. Ili ndoa yenu isambaratike.

Adui yako anaweza akawa yule ambaye hapendi kukuona ukiwa na furaha kwenye ndoa yako. Anapenda kusikia mmegombana sana au mmetengana.

Maadui hao wote wanaokutenda mabaya au wanaotafuta kila njia ili uanguke, Mungu anaenda kuwatenda jambo ngumu sana kwao. Endelea kumtumaini yeye Yesu, utaona maadui zako wakikukimbia na kukuacha kukufuatilia na kukutenda mabaya.

Wewe ni wathamani sana mbele za Mungu, ulipatikana kwa gharama kubwa mno. Mungu hawezi kukuacha peke yako uangamie kama unamcha katika roho na kweli.

Kama Mungu alivyoufanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea wa kabila zote. Kila atakayejitwika jiwe hilo(Yerusalemu) watapata jeraha nyingi.

Rejea: Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake. ZEK. 12:3 SUV.

Ndivyo itakavyokuwa kwa maadui zako, kila atakayejaribu kukuletea fitina au maneno yasiyofaa. Atapata jeraha nyingi sana katika maisha yake. Maana wewe ni jiwe.

Linaweza likawa jeraha katika familia yake, biashara yake, masomo yake, kazi yake, ndoa yake, huduma yake.

Wewe ni mwana wa Mungu aliye hai, hakikisha unaimarishwa katika Yesu Kristo kila iitwapo leo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com