Unaweza ukajiuliza sana na ukafakari sana kuhusu maisha yako ya wokovu ukashindwa kufika mwisho wake. Moja ya kitabu kinachosisimua habari zake, ni hichi cha Ayubu, ni moja ya vitabu vinavyofanana na kuzungumzia maisha yetu ya kila siku.
Nimekaa nikatafakari sana, wakati mimi najitahidi kumcha Mungu na kumpenda kisawasawa. Kumbe kitendo hichi kinamkwaza shetani vile Mungu anajivunia uaminifu wangu kwake, na anafika wakati anaenda kunisemea huko mbinguni kwa Baba.
Huwa tunajua Mungu hawezi kuruhusu jambo baya likupate kama hajakupa taarifa wewe uliye mwaminifu kwake. Ila hii ya Ayubu hakuna mahali inasema alimpa taarifa, hata kwa maono/ndoto haijasemwa, hata kupitia nabii yeyote hakutumwa kwake.
Shetani baada ya kukubaliana na Mungu, Ayubu alianzishiwa makombora makali makali tena yaliyopangana kwa pamoja. Hapo hakupewa taarifa kuwa unakutwa na shetani kukujaribu uwe macho, labda biblia imefunika hili ila kwa sababu haijasema tunao ujasiri wa kusema hili jaribu lilimjia kimyakimya.
Labda nikupe mfano huu unaweza ukanipata vizuri; yaani ni sawa leo unasema una mchumba ambaye unatarajia kuishi naye siku chache kuanzia sasa. Kumbe mchumba yule uliyenaye mipango imesukwa tayari kimyakimya, siku unataka kufunga ndoa baada ya maandilizi yote kuisha. Inatokea mambo yanaharibika siku ya tukio lenyewe yaani uchumba unaharibikia madhabahuni.
Labda huo mfano unaweza usiwe sahihi sana kwako uliyeoa/kuolewa tayari, tusema sasa hivi unamtumikia Mungu vizuri sana. Una kazi nzuri sana yaani ni boss mkubwa kwenye ofisi fulani, unaamka asubuhi unaambiwa huna kazi, hujakaa sawa unaambiwa kile kiwanda chako kinaungua moto sasa hivi na zima moto wamejaribu kufanya kila namna imeshindikana. Wakati unaendelea kujisikilizia kuhusu hilo, unaambiwa zile basi/gari zako zote unazosafirisha abiria zimepata ajali na zimeharibika vibaya kwa kuungua moto.
Kabla hujakaa sawa unasikia msiba wa watoto wako waliokuwa wanarudi nyumbani likizo, wamepata ajali wote na kufariki pale pale. Hizi ni taarifa za siku moja au siku mbili tofauti ila ni kwa mfululizo niliokutajia hapo juu, hapa kama sio kusikia mtu amekufa amesimama basi utasikia mengine.
Hebu fikiri kama mchanga wa kiroho unawezaje kuhimili haya matukio, kumbuka hakuna taarifa yeyote Mungu aliyokupa hata kwa ndoto kuwa utakumbwa na mambo mazito. Ili angalau uchukue hata maombi ya kufunga ili kujiepusha na hilo balaa…lakini hii ilikuwa siri baina ya Mungu na shetani.
Nyakati kama hizi ndipo utakuta wengi wanajiua, nyakati kama hizi ndipo utakuta wengi wanajinyonga, nyakati kama hizi ndipo utakuta wengi wamekunywa sumu, nyakati kama hizi ndipo utakuta wengi wanamwacha na Mungu. Lakini cha kushangaza Ayubu hakufanya hivyo, zaidi alianguka magotini kumlilia Mungu wake.
Ndugu yangu Usifikiri ukishaokoka na ukawa unamsumbua shetani kwa kumharibia kazi zake atakaa kimya bila kukushtaki kwa Mungu wako. Utashitakiwa kama alivyo fanya kwa Ayubu.
Rejea; Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. AYU 1:9-10 SUV.
Uwe tayari ndugu, kama ulikuwa unaishi kwa mtazamo fulani tu ujue kuna maeneo utaguswa ambayo hukupanga kabisa. Kama ulikuwa unamtumikia Mungu kwa sababu ya mali zako siku zikifutika ujue hapo ndio itakuwa mwisho wako, kama ulikuwa kipaumbele kanisani kwa sababu ya kazi yako nzuri, ujue ukifukuzwa kazi utakuwa mwisho wako wa kumpenda Mungu.
Usishangae mtu kujiua katika haya matatizo, inahitajika stamina ya kiroho kuvuka eneo hilo na sio nguvu za ugali samaki/kuku. Mtegemee sana Mungu mama/baba yangu, mtegemee sana Mungu kaka/dada yangu. Si kwa sababu mambo yako ni safi, sio kwa sababu unataka akupe kitu, mtegemee Mungu kwa sababu ya alikukukomboa msalabani.
Nitakuwa nakushirikisha machache kuhusu kitabu cha Ayubu, Mungu akupe mwanga wakuelewa hichi kitabu cha Ayubu tunapoendelea kujifunza hatua kwa hatua.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.