Rahisi kufikiri kila mabaya yanayotupata mwisho wake ni ili tuangamie, kwa kufikiri hivyo tunaweza tukawa na hofu kubwa sana juu ya maisha yetu ya kila siku.

Hofu ambayo inaweza kutupelekea tukaanza kufikiri kujizulu, ili kuepuka aibu itakayotupata, au kuepuka mateso yatakayotupa baada ya hicho kutokea. Kufikiri hivyo imewafanya watu wengi sana kuchukua maamzi ambayo hayakustahili kuchukuliwa.

Hatuwezi kukataa mabaya yanayotarajiwa kutupata yasitupate, kuokoka kwetu hakuwezi kubadilisha chochote kile tukaacha kupatwa na mabaya. Haitajalisha uhusiano wetu mzuri na Mungu, bado kuna nafasi ya mabaya kutupata.

Wengi tunapokuja kukosea ni kumwacha Yesu wakati wa mabaya yanayotupata, wakati ambao tulipaswa kuendelea kushikana na Yesu kisawasawa. Inakuwa nafasi ya wengine kumwacha Yesu na kugeukia njia nyingine.

Tunapaswa kubadili mtazamo mbaya juu ya mabaya yanayotupata katika maisha yetu ya wokovu, sio kila mabaya mwisho wake ni mbaya. Hata kama yule anayekutendea hayo mabaya anategemea upatwe na mabaya, hilo halipaswi kukunyima usingizi.

Kupitia yale yale mabaya yaliyokusudiwa kwako na yatakatimia kama yaliyopangwa yafanyike, endelea kumshikilia Yesu wako. Maana kupitia hayo mabaya lipo kusudi la Mungu linapitia humo humo.

Rejea: Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. MWA. 50:20 SUV.

Sikuelezi jambo ambalo halipo, hilo andiko linatuthibitishia yale Yusuf aliyotendewa na ndugu zake wa damu, kupitia makusudi yao mabaya, Mungu alikusudia yaliyomema juu yake.

Hii inatufundisha jambo kubwa sana, wakati mwingine ili tufikie ndoto zetu kubwa yapo mabaya yatapaswa kutufikisha huko, sio jambo la kufurahisha sana wakati huo ila ni hatua inayotufanya tufikie mafanikio makubwa.

Inaweza ikawa ngumu kuelewa wakati huo, maana huwa ni wakati ambao tunaona Mungu ametuacha, ni wakati ambao tunaona Mungu hatusikii kile tunamwomba kila siku atutendee.

Kama mtu atavumilia kipindi chote cha magumu anayopitia/anayopata pasipo kumwacha Yesu Kristo, utafika wakati atajua kwanini alipatwa na hayo mabaya. Hata wale waliohusika kuyatenda hayo mabaya wataishia kuomba msamaha, bila kujua ubaya wao ndio umemfikisha mwenzao hapo alipo.

Rejea: Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. MWA. 45:5 SUV.

Yesu akiwa ndani yako sawa sawa hutokuwa na hasira na wale waliokutenda mabaya, hata pale utakapoona wanajutia kwa yale mabaya waliyoyatenda. Wewe utakuwa mfariji wao wakati huo, maana utakuwa umejua mafanikio yako yamechangiwa na ubaya wao.

Kwa mtu aliyekosa maarifa ya Neno la Mungu atataka alipize kisasi, kulipa kisasi sio kazi ya mwanadamu, bali ni kazi ya Mungu. Mtu yeyote yule aliyejaa neno moyoni mwake hayawezi kujikwaa kwa hili.

Mungu atupe moyo wa kupenda Neno lake zaidi na zaidi, ili tuweze kujipushe na dhambi ambazo zingeweza kuua uhusiano wetu mzuri na Mungu wetu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
+255759808081
www.chapeotz.com