“Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko”, Mwa 32:29 SUV.
Kila jina lina maana yake, wapo hupewa majina kutokana na matukio waliyokutana nayo wazazi, sio ajabu kukutana na mtu anaitwa Mawazo, Tabu, Shida na majina mengine mengi yanayofanana na hayo.
Wapo hupewa majina kutokana na mambo mazuri yaliyotokea kipindi hicho, na wengine hupewa majina ya watu maarufu wa kipindi hicho, na wengine siku za leo hutumia majina ya watu mbalimbali walioorodheshwa kwenye Biblia.
Tukija kwa Yakobo, jina lake lilimaanisha “mdanganyifu”, na jina alilopewa la Israeli lilimaanisha “aliyeshindana na Mungu”. Mtu aliyekuwa anashindana naye alimpa sababu ya jina lake kubadilishwa na kuitwa Israeli.
“Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye”, Mwa 32:24-25 SUV.
Usiku wa Yakobo inaonyesha ulikuwa wa hekaheka kubwa, usiku ambao ulikuwa wa kushindana na Mungu mwenyewe, usiku ambao ulibadilisha historia ya Yakobo na kupelekea kubarikiwa maisha yake.
Kubarikiwa kwa Yakobo inaonyesha wazi kabisa kulibadilisha mtazamo wake na kujua ya kwamba ustawi wa maisha yake hautategemea tena ujanja wake bali msaada wa Mungu pekee.
Tunaona hata baadaye Mungu aliwakumbusha Israeli ukweli huu wa kumtegemea yeye peke yake ndipo wataweza kufanikiwa katika maisha yao.
“Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi”, Zek 4:6 SUV.
Ushindi wetu na baraka zetu huja si kwa sababu ya ujuzi mwingi au elimu au kwa nguvu zetu wenyewe, bali huja kwa uweza wa Mungu peke yake, zaidi ya hapo ni kujidanganya.
Tunajifunza kwa Yakobo na kuona kuwa Mungu hupenda wale watu wanaomtafuta kwa bidii na kung’ang’ana naye hadi kuhakikisha wanapokea baraka zao kutoka kwake.
Jambo lingine kubwa ambalo tunajifunza kupitia Yakobo ni kwamba, Mungu anaweza kubadilisha jina baya la mtu na kuwa jina zuri, kama mtu alizoeleka kuitwa tapeli, mwizi, muongo, kahaba, maskini, mjinga, mlevi na majina mengine mengi mabaya. Mtu huyo anaweza kubadilishwa na Mungu na kuanza kuitwa mtumishi wa Mungu, mtu aliyebarikiwa sana na Mungu.
Hatupaswi kuwakatia tamaa watu na kuwabatiza majina yao mabaya, tukifikiri watakufa na hayo majina, wakati wowote mambo yanaweza kubadilika na kuanza kuitwa jina jipya lililobeba matendo mema ya mtu.
Bila kujalisha umekuwa mtu wa namna gani, Mungu anaweza badilisha jina lako, kama watu wamekupa jina baya kutokana na hali yako ya maisha au tabia yako, fahamu ya kwamba Mungu anao uwezo wa kubadilisha hilo jina lako baya, na kuitwa jina jipya zuri.
Maisha yetu yanawezekana kuchongwa upya, tusijidharau na kujikatia tamaa, hakikisha unakabidhi maisha yako mbele za Mungu, ikiwa ni wazazi wako, watoto wako, ama ndugu yako yeyote yule usiache kumwombea, ipo siku Mungu atakutana naye na kumbadilisha maisha yake.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081