Kuna wakati mwingine huwa tunafika mahali tunaanza kulaumu sana kuhusiana na uongozi wa mtumishi fulani wa kanisa. Vile anavyoongoza washirika wake, vile hajali washirika wake, vile anajali tu pesa, vile anawapenda tu wale wenye uwezo wa kifedha, vile hana huruma na waliovunjika moyo.

Vile anaongea maneno ya kuchoma tu mioyo ya watu, tena wale walioumizwa na shida mbalimbali za maisha yao. Yeye mchungaji anakuja kuwaongezea maumivu makali zaidi yenye kuwatoa kabisa kwenye matumaini.

Upo kwenye shida ngumu sana, ukiwa unategemea mchungaji wako au kiongozi wako wa kanisa anayekulea kiroho. Akutamkie maneno ya faraja, maneno yenye kukutia moyo, badala yake anakuvunja moyo zaidi kwa kukutamkia maneno mabaya zaidi.

Wachungaji au watumishi kama hawa huwa tunaona wanatoka kwa shetani, na kweli unaweza kufikiri hivyo kutokana na machukizo yake kwa watu. Maneno anayotamka kwa washirika wake, hayaendani kabisa na mtu aliye na Roho wa Mungu ndani yake.

Unapaswa kufahamu kwamba wengine Mungu huwaleta mwenyewe, ndio Mungu huwachagua mwenyewe wakae kwenye nafasi hiyo kwa kusudi lake maalumu.

Mtalalamika weee, mtasema mchungaji gani huyu, mtasema mchungaji gani huyu asiye na utu kwa washirika wake, mtasema mchungaji gani huyu anayependa tu pesa. Kusema hayo yote haiwezi kubadilisha ukweli kuwa Mungu mwenyewe ndiye aliyeruhusu akae kwenye hicho kiti.

Ana matendo ya hovyo kweli, hana roho ya uchungaji kweli ila ni mchungaji wako, au wa kanisa la mahali na Mungu mwenyewe amemweka kwenye nafasi hiyo.

Ni kama vile hii haikuingii akilini ila unapaswa kufahamu kwamba maandiko matakatifu yameweka wazi hili ninalokueleza hapa.

Rejea: BWANA akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu. Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao. ZEK. 11:15‭-‬16 SUV.

Hili linaingia kwenye uongozi wowote ule, unaweza ukawa uongozi wa kiroho au kimwili kabisa. Mungu anaweza kumwinua mtu wa namna hii tuliyosoma kwenye andiko hilo hapo juu.

Unaweza kukutana na mchungaji wa namna hii, kupitia Neno hili nikuombe ubadilishe kufikiri kwako. Kama zamani ulikuwa unafikiri labda ni mpango wa shetani kuwa na mchungaji wa namna hiyo, ondoa kabisa fikra hizo.

Hapa tunajifunza kwamba Mungu atainua mchungaji ambaye hatakuwa na muda wa kuangalia kondoo waliopotea, hatawatafuta kondoo waliotawanyika huku na kule, wala hatawaganga waliovunjika mioyo yao, wala hatawalisha Neno la Mungu wale wenye uhitaji huo.

Ni jambo la kutisha sana ila haya mambo yanaweza kutokea kabisa katika maisha yetu, utalalamika sana mchungaji fulana ana roho mbaya kweli kweli utafikiri sio mchungaji. Lakini ndivyo alivyo, yupo kwenye kazi maalum kwa wakati huo.

Jifunze hili na uliweke moyoni mwako, pindi utakapokutana na hali kama hii. Usianze kupata shida sana moyoni mwako, uwe unajua hili jambo lipo linaweza kutokea kabisa katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.