Kuna vitu katika maisha yetu tunaweza kuvipoteza kwa kushindwa kutii maagizo tunayopewa na Mungu.

Tunapovipoteza wengi huwa tunabaki tunaumia, wengine hubaki kulalamika, wengine hubaki kulia, wengine hufikiri kujiua.

Wapo wengine huacha wokovu, hasa pale wanapoona sifa yao imekuwa mbaya. Badala ya kutubu na kunyenyekea mbele za Mungu, huwa wanaona njia rahisi ni kuacha wokovu.

Wengine hukimbia kanisa, anahamia sehemu nyingine kukwepa aibu. Kuhamia mahali pengine napo hakumsukumi kutubu.

Wachache huwa wanakumbuka kumrudia Mungu, sio kumrudia tu kwa maneno, humaanisha kweli.

Tukiachana na hayo, yapo mambo muhimu sana katika maisha yetu huyapoteza kabisa.

Tunapoyapoteza mambo muhimu tunapaswa kumwomba Mungu arejeshe kile kimepotea.

Hili tunajifunza kupitia andiko hili, huyu mtu alipoteza mkono wake. Alichojua Mungu anaweza kumrejesha tena mkono wake.

Rejea: Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza. 1 FAL. 13:6 SUV.

Hili ni funzo kwetu, yapo mambo muhimu sana huwa tunapoteza. Tunachopaswa kufanya ni kumwendea Mungu wetu.

Kumwendea Mungu inatufanya turejeshewe kile ambacho kimepotea.

Hebu jiulize ni mambo mangapi umekuwa ukipoteza  katika maisha yako. Na ulikumbuka kumrudia Mungu?

Nikuache na tafakari hiyo, naamini lipo jambo la muhimu umejifunza kupitia ujumbe huu.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com