Haleluya, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, habari za kutwa nzima ndugu yangu katika Kristo YESU. Wakati mwingine tena mzuri wa kushirikishana TAFAKARI zetu kwa kile tulichokivuna katika sura ya leo.

Mungu anapendezwa na mambo mengi mazuri tukiyafanya kwa ajili ya utukufu wake, moja ya jambo analolipenda sana kutoka mwanzo ni kumsifu katika roho na kweli.

Tunapomaanisha kwa kile tunachofanya mbele zake, Mungu wetu lazima ashuke awahudumie watu wake waliokusanyika kwa jina lake.

Tunapaswa kujifunza hili sana, hasahasa sisi tunaotoa huduma madhabahuni, tunapaswa kujitakasa kabla ya kusimama mbele za watu kuwahudumia.

Njia zetu zinapaswa kuwa safi, ili Mungu apate kushuka kupitia sisi tunaotoa huduma. Katika kumwimbia Mungu, watu wamwone Mungu wasikuone wewe, wamwone Mungu aliye ndani yako.

Tukilijua hili na tukalifanyia kazi kwa umakini, tutaanza kuona Mungu akishuka kupitia huduma mbalimbali za uimbaji.

Najua hata wewe unapenda kusifiwa, hasahasa unapofanya vizuri, unapopongezwa ndani yako utajisikia vizuri sana. Ila utakapofanya vizuri alafu usipate hata mtu mmoja wa kukutia moyo kuwa ulifanya vizuri sana. Uwezekano upo wa kuanza kufikiri labda ipo sehemu umekosea, ukifikiri sana ulipokosea unakosa jibu unabaki kuwa myonge.

Mungu wetu ni zaidi, anaposifiwa na watoto wake, hushuka kwa nguvu zake za Roho Mtakatifu. Unaweza kuona nguvu za MUNGU ndani ya kusanyiko lake kwa sababu tu wewe ulijiandaa vyema kutoa huduma.

Hili tunalithibitisha kwa maandiko haya Matakatifu;
hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru BWANA nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya BWANA, hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa BWANA. 2 NYA. 5:13‭-‬14 SUV.

Moyo uliojaa shukrani mbele za Mungu, unaweza kusababisha ukamsifu Mungu katika roho na kweli. Tuondoe mazoea ya kwenda mbele za MUNGU tutaona mafanikio makubwa sana KIROHO.

Tamani kujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu kama bado hujajazwa, hakika nakwambia utaona mabadiliko mengi sana kitabia katika maisha yako KIROHO.

Ikiwa maisha yako ni safi mbele za Mungu, mwambie Mungu nahitaji kujazwa na nguvu zako za Roho Mtakatifu. Mungu sio mchoyo atakujaza sawasawa na haja ya moyo wako.

Hapo ndipo utajisikia hamu ya kuendelea kumtafuta Mungu zaidi kwa bidii, bidii isiyo na kikomo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Chapeo Ya Wokovu.

Chapeo@chapeotz.com

+255759808081.