Tukiwa kama wakristo tunapaswa kuelewa kwamba tunapokuwa tumeokoka, tunapaswa kusimama na Yesu nyakati zote.

Shida inakuja pale mtu anapokuwa ameokoka vizuri, alafu ikatokea shida ngumu kwake. Anaamua kumgeukia Shetani kwa kufikiri kuwa huko ndio kuna msaada mzuri zaidi.

Kufanya hivyo kwa mkristo kunamfanya afarakane na Mungu wake. Hii wengi huwa hawaoni kama ina madhara makubwa kwao.

Mtu anaweza akawa vizuri kanisani, ikatokea ana shida ngumu. Akaomba kwa muda bila kupata majibu ya shida yake, anaamua kugeukia waganga wa kienyeji.

Mwingine anaweza akawa ameombewa na watumishi mbalimbali wa Mungu, alivyoona hapati majibu anaamua kukimbilia kwa waganga wa kienyeji(wachawi)

Mambo haya yamewakosesha watu wengi mahusiano yao na Mungu, tena wameiamsha hasira ya Mungu juu yao.

Hii tunaiona kwa Sauli pia, Sauli alimkosea Mungu kwa kwenda kutafuta msaada kwa watu wenye pepo wa utambuzi.

Rejea: Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa BWANA, kwa sababu ya neno la BWANA, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake, asiulize kwa BWANA; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese. 1 NYA. 10:13‭-‬14 SUV.

Hili sio kwa Sauli tu, wapo watu ambao walishaijua kweli ya Mungu, ila wakageuka na kwenda kutafuta msaada kwa watu wa pepo wa utambuzi.

Kupitia andiko hili tuliloliona hapa, tunapata picha vile ambavyo Mungu alichukizwa na kitendo cha Sauli kwenda kutafuta msaada kwa watu wa pepo wa ufumbuzi.

Wengi wameingia katika mtego huu, badala ya kumtumainia Mungu. Wao wanageukia miungu mingine kutafuta msaada.

Hasa watu wanaopenda kutabiriwa tabiriwa, wengi wametabiriwa na watu wenye pepo wa utambuzi. Ambao wao husema ni nabii wa Mungu, kumbe sivyo.

Tunapaswa kuwa makini sana, maana kwenda kutafuta msaada kwa watu wenye pepo wa utambuzi. Hiyo ni dhambi mbele za Mungu, na inatufakaranisha na Mungu wetu.

Vibaya sana kufarakana na Mungu wako, sisi tunapaswa kuwa na uhusiano mwema na Mungu wetu. Bila kujalisha tumeomba sana na hajajibu kama tulivyotaka ajibu.

Mungu atusaidie sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081