Mtu anaweza akawa anahaingaka sana kumbadilisha mwenzake atoke kwenye tabia fulani mbaya, na awe na tabia njema.

Mahangaiko yale yanaweza yasizae matunda kabisa, na akabaki anaumia na kutumia nguvu za mwili na akili zake.

Tunachopaswa kufahamu ni kwamba, mwenye uwezo wa kumbadilisha mtu tabia mbaya na kuwa nzuri ni Mungu mwenyewe.

Sio hilo tu, tunapaswa kuelewa kwamba tabia mbaya yeyote iliyoonekana kwa mtu. Tabia hiyo inaweza kubadilika pale atakapomkubali Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake.

Pale Roho Mtakatifu atapojenga makao ndani yake, mtu huyo anaweza akawa wa tofauti sana na vile alifahamika awali kama mtu asiyefaa.

Ndio maana watu wanaweza kupinga sana juu ya mtu kuacha tabia fulani mbaya. Wakaona haiwezekani kabisa  mtu huyo kubadilika.

Wengine wataenda mbali zaidi na kuona ndivyo alivyozaliwa, ndivyo ukoo wake ulivyo, au ndivyo asili ya familia yake ilivyo.

Moyo wa mtu unaweza kubadilishwa na Mungu, haijalishi huyo mtu alikuwaje.

Hili tunajifunza kwa Sauli, baada ya kupakwa mafuta na Samwel. Kuanzia hapo moyo wake ulibadilishwa na Mungu.

Rejea: Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. 1 SAM. 10:9 SUV.

Kumbe mwenye uwezo wa kumbadilisha mtu moyo wake, kama ulikuwa ni moyo ulio mgumu au mbaya. Anakuwa ni mpendwa mzuri kabisa.

Tena wale waliomfahamu ni mtu wa namna fulani, wataanza kushangaa na kujiuliza imekuwaje kwa huyu ndugu.

Haya yapo katika jamii zetu, wapo watu tulikuwa tunawafahamu kwa namna isiyo njema.

Lakini baada ya kumruhusu Yesu katika maisha yao, mioyo yao ilibadilishwa kabisa.

Wale waliomjua Sauli hapo kabla, walibaki na maswali yaliyokosa majibu yake.

Rejea: Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? 1 SAM. 10:11 SUV.

Lazima watu wakushangae, sio kosa lao, ni vile wanakufahamu kwa muda mrefu.

Wapo wengine ulisoma nao, wapo wengine ulikua nao pamoja mtaani.

Wapo wengine umekuwa nao kazini kwa muda mrefu, wanakufahamu vizuri tabia yako.

Siku Mungu anaubadilisha moyo wako, unakuwa mpya kabisa. Tabia yako ikabadilika kabisa na kuwa tofauti na ile ambayo wameizoea.

Watu lazima wajae na alama za mishangao kwenye vichwa vyao. Lakini huo ndio utakuwa ukweli wenyewe.

Mtazame Mungu ndiye anayeweza kugeuza moyo wa mtu aliyeonekana hafai, akaonekana anafaa tena.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.