Mzazi mzuri, mama mwenye malezi bora kwa watoto wake, baba mwenye malezi bora kwa watoto wake, na mlezi mwenye malezi bora kwa watoto anaowalea. Hakutokea ghafla, wala hakuota kama uyoga.

Alifunzwa akafunzika vyema, alipita vipindi vya kuumizwa, kwa kuchapwa fimbo, kwa kukemewa, kwa kunyimwa vitu fulani anavyovipenda, kwa kubanwa maeneo fulani anayoyapenda. Kwa nia ya kujengwa, ajue kuna kukosa, ajue sio kila analoona ni zuri ni zuri kweli, ajue kuna mipaka ya utendaji, ajue sio kila neno la kutamkwa.

Mtoto huyo akakua katika misingi hiyo, ikifika wakati na yeye akawa baba/mama na sio mtoto, akatakiwa kulea na yeye maana tayari amekuwa baba/mama. Kwa kuwa alilelewa katika misingi bora, misingi ya kumjengea uwezo wa kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na watu.

Misingi ile ile atamjengea mtoto wake, atatamani akue katika misingi ile ile maana anajua kuna faida katika hayo, na kuna hasara asipomfunza mwanaye katika hayo.

Ndipo utakuta katika malezi hayo bora kwa watoto wake, mzazi huyo atazalisha makundi mbalimbali ya watoto, baadhi wataona baba/mama mbaya, baadhi wataona baba/mama hawapendi, baadhi wataona baba/mama mkorofi, baadhi wataona baba/mama ana upendeleo, na baadhi wataona baba/mama ana uonevu.

Lakini wakikua na kuwa watu wazima, wale waliomsikiliza baba/mama na kufuata njia aliyokuwa anawaelekeza, watamshukuru sana na kuona vile walikuwa wanamfikiri baba/mama wakati wa utoto wao haikuwa hivyo. Baba/mama alikuwa na nia njema na wao.

Na wale ambao hawakumsikiliza baba/mama, wakafanya yale waliyokuwa wanaona wao ni sahihi, au wakaenda njia ambayo waliona wao nzuri machoni pao. Lakini ilikuwa njia ya mauti.

Rejea: Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. MIT. 14:12 SUV.

Hawa huwa wanabaki kukumbuka maonyo ya baba/mama, wanakumbuka vile walipuuza na kuona njia yao ni njema. Huwa wabaki na kauli za ningejua nisinge… ningelijua ninge… wakati huo majuto huwa mengi.

Ili uwe mzazi bora unapaswa kupitia maumivu fulani, unapaswa kukubali kuelekezwa, unapaswa kumheshimu na kumtii mzazi wako.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255 759 80 80 81