Agizo kama hili Mungu anakupa wewe mtumishi wake wa kweli, mahali ambapo watu wanatenda dhambi, mahali ambapo wamesikia sana injili, mahali ambapo hawataki kuacha mabaya yanayomchukiza Mungu wao.

Mungu anakutuma kwa watu wa namna hiyo, unaweza kutoa sababu za kiuzoefu, kutokana na vile umeshuhudia mikutano mbalimbali ikitendeka mahali pale. Ila inafika mahali Mungu anasema nawe moja kwa moja kupitia Neno lake.

Unaweza ukawa umeongea sana juu ya mtoto wako kuachana na dhambi anazozifanya, Mungu anaweza kusema na mtu mwingine akaseme na mtoto wako.

Inaweza kuwa mmefika mahali mkaanza kusema tutaenda kujua mbinguni, nani ataingia uzima wa milele na nani ataingia jehanamu. Hii inakuja baada kuwasihi sana wenzako waachane na imani potofu, lakini hawakutaka kukusikia.

Mungu anaweza kusema nawe kupitia Neno lake, useme nao tena, haijalishi mioyo yao ni migumu, haijalishi nyuso zao zimekosa aibu/haya kutenda mabaya. Unatumwa kusema nao tena, ili siku ya hukumu Mungu awakumbushe nilimtuma mtumishi wangu hamkutaka kumsikiliza.

Hili tunajifunza kwa wana wa Israel, Mungu alituma mtu wa kusema nao, pamoja na ugumu wa mioyo yao, na pamoja na nyuso zao kukukosa haya. Mungu anasema haijalishi watasikia, ama hawatasikia, kikubwa wafikishiwe ujumbe.

Rejea: Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo. Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi. Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao. EZE. 2:3‭-‬5 SUV.

Leo sio wana wa Israel tena, leo ni sisi, ukiwa kama mtumishi wa Mungu usiogope kuisema kweli ya Mungu pale anapokusuma kufanya hivyo. Haijalishi watasikia, wala haijalishi watakupuuza, hakikisha unapaza sauti yako.

Leo watu wanathamini dini zao na kuzitii kuliko Neno la Mungu, ukimweleza kuhusu kuzaliwa mara ya pili. Anaanza kukupa hadithi zingine, hii ni kwa sababu mioyo yao imekuwa migumu, na nyuso zao zimekosa haya kwa mambo mabaya wanayofanya.

Leo unamwambia mtu acha kuabudu sanamu, anaanza kukupa sababu za ovyo kweli kweli, hilo lisikupe shida ikiwa kama mtumishi wa Mungu(uliyeokoka). Wakubali ama wakatae, wewe utakuwa umetimiza wajibu wako kama ulivyoagizwa na Mungu.

Leo unamwambia mkaka/mdada, acha kuzini ovyo, subiri wakati wako wa kuolewa/kuoa. Badala ya kukusikia na kubadilika, anakuona unamfuatilia maisha yake, fanya wajibu wako nenda zako.

Chochote unachosukumwa na Roho Mtakatifu kukisema, kiseme kisha uache watu wenyewe wachukue hatua au wapuuze. Sio useme alafu wasipochukua hatua ya kubadilika, unazira, au unakasirika na kuacha huduma, huo ni utoto, aliyetumwa na Mungu haachi huduma kwa sababu yeyote ile.

Kuukataa ukweli kwa kutokubaliana nao, hakuwezi kuugeuza ukweli huo kuwa uongo.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081