“Akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe”, Mt 4:6 SUV

Shetani alitumia Neno la Mungu kumjaribu Kristo kutenda dhambi. Pia lilikuwa ni jaribio la kumshawishi Yesu atoke kwenye njia ya utii mkamilifu kwa mapenzi ya Mungu.

Kumbuka kwamba katika kila jaribu, Yesu alijitiisha chini ya mamlaka ya Neno la Mungu kuliko matakwa ya Shetani (Mt 4:4, 7, 10). Tunajifunza nini hapa kutoka katika majaribu ya Kristo?

Jambo la kwanza, tunajifunza Shetani ni adui yetu mkuu. Tukiwa Wakristo ni lazima tufahamu kwamba tuko katika vita vya kiroho tukipambana na nguvu za uovu zisizoonekana kwa macho lakini ni halisi.

“Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”, Efe 6:12 SUV.

Jambo la pili, tunajifunza bila Roho Mtakatifu na matumizi sahihi ya Neno la Mungu, mkristo hawezi kushinda dhambi na majaribu yanapokuja kwake.

Kuna nyakati watu wa dunia hii watatumia Maandiko Matakatifu katika kujaribu kukushawishi kufanya kitu ambacho wanajua si sahihi kufanya. Baadhi ya vifungu vya biblia vinapotolewa nje ya maana yake au visipolinganishwa na vifungu vingine vya Neno la Mungu, vinaweza kuonekana kama havikatazi dhambi, mfano kifungu hichi;

“Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote”, 1 Kor 6:12 SUV.

Ukisomewa hichi kipande tu “vitu vyote ni halali kwangu” unaweza kuingizwa kwenye mtego wa Shetani na ukafanya kitu ambacho ni dhambi mbele za Mungu, alafu baadaye unakuja kugundua kuwa ulichofanya ni kibaya.

Wakristo ni lazima walifahamu vizuri na kwa usahihi Neno la Mungu na wawe macho na wale ambao hupotosha Maandiko Matakatifu ili kutimiza tamaa zao zinazotokana na asili ya kibinadamu ya dhambi.

Mtume Petro alilizungumzia hili kwa wale ambao huyageuza Maandiko Matakatifu na kujiletea uharibifu wao wenyewe.

“Vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe”, 2 Pet 3:16 SUV.

Yafuatayo ni mambo 5 muhimu namna ya kutumia Neno la Mungu katika kushinda majaribu;

  1. Tambua kwamba kwa kupitia Neno la Mungu unayo nguvu ndani yako ya kupinga kila hila au hoja anayoweza kuileta Shetani kwako (Yn 15:3,7). Usiwe na wasiwasi, hoja yeyote iliyo kinyume na neno la Mungu usiiamini kabisa hata kama imesindikizwa na andiko.
  2. Jaza neno la Mungu kwa wingi ndani ya moyo na ufahamu wako (Yak 1:21). Hii ni muhimu sana kwako, ukiwa na akiba ya kutosha ndani yako, ni rahisi kupangua hoja zote za Shetani unapokuwa kwenye jaribu.
  3. Tafakari usiku na mchana ile mistari uliyoikariri au uliyoijaza ndani ya moyo wako (Zab 1:2; 119:47-48). Huwezi kutafakari kitu ambacho huna ndani yako, unapaswa kusoma neno la Mungu kila siku, ujae Neno la Mungu ndani yako, hapo ndipo utakuwa na nafasi nzuri ya kutafakari yale uliyojaza ndani yako.
  4. Jiambie na jikumbushe wewe mwenyewe na Mungu vile vifungu ulivyovikariri pale unapojaribiwa (Mt 4:4, 7, 10). Shetani anaweza kukujaribu kupitia mawazo yako, unaweza ukasikia kitu kibaya na kikakuingiza katika jaribu zito, ukawa na unapambana ndani kwa ndani. Kumbuka neno la Mungu linasemaje juu ya hilo unalopata ushawishi kulifanya, utapata majibu na utashinda hiyo hali.
  5. Tambua haraka na kutii msukumo wa Roho Mtakatifu unavyokusukuma kufanya kupitia Neno la Mungu (Rum 8:12-14). Unapokuwa kwenye jaribu na una neno la Mungu ndani yako, Roho Mtakatifu atakusemesha kupitia neno la Mungu, utashangaa unakumbuka andiko fulani na litakujia kwa nguvu sana.

Usilipuuze bali litii, kufanya hivyo utaweza kumshinda Shetani na hila zake mbaya kwako, pia unaweza kupata uzito na huzuni ndani yako unapotii sauti, ujue hiyo ni huzuni ya Roho Mtakatifu umeacha kutii sauti yake.

Haya ni mambo muhimu sana kwako, ukiyazingatia na kuyafuata utamshinda Shetani siku zote, haijalishi atakujia kwa njia gani na kwa jinsi gani, utaweza kumshinda kupitia Neno la Mungu lililo ndani yako.

Karibu sana uungane nasi kwa njia ya wasapu kusoma na kutafakari neno la Mungu kila siku na kushirikishana tafakari zetu, wasiliana nasi kwa njia ya wasap kupitia namba hii +255759808081 ili uweze kuungwa kwenye group.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081