“Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo?”, 1 Yoh 3:17 SUV.

Jamii zinatofautiana na maisha wanavyoishi wanapishana baadhi ya maeneo kadhaa kutokana na tamaduni na taratibu zao za familia.

Wapo watu wanaishi kwa pamoja na sehemu moja kutokana na familia yao, wengine kila mtu hupewa eneo lake la kuishi na familia yake.

Wapo kutokana na majukumu ya kazi wametawanyika kila mahali, wamebaki wachache nyumbani wanaoishi pamoja.

Wale walio pamoja husaidiana katika maisha yao kwa kuwedheshana kiuchumi na mahitaji mbalimbali.

Wapo watu Mungu amewasaidia wamefanikiwa kwenye maisha ya kawaida kabisa, wanazo Mali na nafasi nzuri za kuweza kuwapatia fedha nzuri.

Fedha huwa hazitoshi kwa wengi wetu ila tunapaswa kusikiliza Mungu anatuelekeza nini katika maisha yetu.

Wapo ndugu zetu ni wahitaji sana, wanahitaji msaada wetu ili waweze kuondokana na hali ngumu walizonazo.

Tunaweza kuwasaidia watu ila tukapokea mambo mabaya badala ya mema kwa wema wetu tulioutenda kwao, hii haipaswi kuwa sababu ya kusitisha kutoa msaada wetu.

Upendo wa dhati kwa mwamini ni kumsaidia yule ndugu anayehitaji msaada wetu kupitia vile vitu ambavyo Mungu ametubariki.

“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake”, Yak 2:14‭-‬17 SUV.

Msaada sio fedha tu, yupo mtu anahitaji chakula, yupo anahitaji mavazi, yupo anahitaji matibabu, yupo anahitaji malazi. Ukiwa na nafasi kati ya hivi unapaswa kumsaidia mhitaji kweli kweli.

Yapo maeneo ambayo hajafikiwa na Injili, ndugu zetu wanaishi huko, hawa pia ni wahitaji wakubwa sana. Tunahitaji kutoa Mali zetu kusapoti watumishi wa Mungu walio tayari kwenda maeneo hayo kuhubiri injili.

Wapo wanaweza kutumia nafasi hii ya kusaidiwa vibaya, watu kama hawa wasije wakatuvunja moyo tukawa vipofu wa kushindwa kuwaona wahitaji wa kweli.

Tunapozungumzia ndugu anaweza asiwe wa tumbo moja au wa ukoo wako, wapo watu unawafahamu ni wahitaji kweli kweli na unaona unaweza kufanya jambo kwao, usiache kufanya hivyo.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest