Mtu aliye na Yesu Kristo moyoni mwake, na mtu huyo akawa na maisha matakatifu yanayompendeza Yesu Kristo. Mtu huyo huwezi kumlinganisha na watu wengine wasiomjua Kristo, nguvu aliyonayo ni kubwa zaidi ya vile unaweza kumwangalia kwa nje.

Kazi zile zile alizozitenda Yesu Kristo, watumishi wake wataweza kuzitenda zaidi yake yeye, Yesu mwenyewe alisema hayo kuthibitisha kuwa tunao uwezo wa kuzitenda kazi zake zaidi yake alivyokuwa Duniani.

Rejea: Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. YN. 14:12 SUV.

Nguvu walizonazo wale wote waliompokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao, wanayo nguvu kubwa mno ndani yao. Nguvu ambayo wakiitambua wanaweza kutenda mambo makubwa sana, kwa kuitumia hiyo nguvu.

Changamoto inakuja pale watu wengi wanapokosa maarifa sahihi ya kuweza kutambua uwezo walionao ndani yao ni mkubwa zaidi kuliko hata mwonekano wa miili yao.

Yesu Kristo akiwa moyoni mwako, wewe sio mtu wa kawaida kabisa katika ulimwengu wa kiroho na kimwili. Shetani analitambua hilo sana, ndio maana anakuletea kila vikwazo kuhakikisha unamwacha Yesu, unaenda kwake.

Mkristo aliyeokoka sawasawa akajua nguvu aliyonayo ndani yake, hakuna mchawi wa aina yeyote ataweza kumtishia maisha yake. Tena angejua kuwa wachawi wanapata shida juu yake, hadi wakati mwingine wanamwita mchawi, angetembea kifua mbele kwa ujasiri mkubwa.

Ujasiri wetu kama watu waliompokea Yesu Kristo upo chini ya kiwango, kwa sababu hatuna elimu ya kutosha ya Neno la Mungu. Laiti tungepata elimu hii ya Neno la Mungu, Ujasiri wetu ungekuwa wa kiwango cha juu sana.

Tunakosa maarifa ya muhimu sana kutokana na kutojua umhimu wa Neno la Mungu, na hata tunajua tunakuwa hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu. Wakati mwingine tumeanza vizuri kabisa kusoma Neno la Mungu ila tulifika mahali tukaishia njiani, hilo ndio limekuwa tatizo la wengi wetu.

Kwa mtindo huo wa kuishia njiani, tumekosa maarifa mengi ya muhimu ya kutusaidia katika maisha yetu ya wokovu, ndio pale unakuta mtu mkristo ila ni muoga kwa wachawi haijawahi tokea.

Wengine ile kuombea tu mtu mwenye nguvu za giza, anaogopa sana, unashindwa kuelewa huyu mtu ameokoka au anaigiza maisha ya wokovu. Kumbe ameokoka ila hajui jina alilobeba ndani yake lina nguvu kiasi gani, anaona nguvu za giza zinaogopesha zaidi bila kujua jina la Yesu Kristo ndio linaogopwa zaidi na mapepo na majini.

Nguvu hii ya Yesu Kristo tunaithibitisha kupitia Neno lake, siku anakamatwa, lile kundi kubwa lilotumwa na wakuu wa makuhani na Mafarisayo lililoongozwa na Yuda, walipofika kwake, Yesu alipowauliza mnatafuta nani? Waliposema wanamtafuta Yesu, Yesu aliwajibu ndio mimi.

Ile Yesu Kristo kujibu kwa kinywa chake, yale majibu yaliwafanya watu wale warudi nyuma na kuanguka chini, kilichofanya waanguke chini ni yale maneno ya Yesu Kristo aliyowajibu.

Rejea: Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. YN. 18:4‭-‬6 SUV.

Utiisho wa Yesu Kristo ni mkubwa sana, ukilitambua hili, maisha yako ya wokovu yatakuwa imara sana. Hutotishwa na jambo lolote la giza, maana wewe ni nuru ing’aayo gizani, hakuna nguvu yeyote ya giza inaweza kukuondolea usingizi wako.

Baada ya kusoma mstari ule wa sita, nimepata ujasiri mkubwa sana, wakati mwingine unaweza kuchukulia ukristo ni jambo la kawaida sana. Ila unaposoma Neno la Mungu kila siku, unakumbushwa kuwa ukristo sio wa kawaida kama unavyoweza kuuchukulia.

Hebu rudia kuusoma huu mstari wa sita; Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. YN. 18:6 SUV.

Hawa watu hawakuanguka kwa sababu walikuwa na njaa sana, wala hawakuanguka kwa sababu walikuwa na afya mbovu, maana Biblia haijasema hivyo. Hawa walikuwa ni askari walioaminiwa, na wote tunajua askari jeshi sio watu walegevu.

Pamoja na ushupavu wao mkubwa, maneno ya Yesu Kristo yaliwavuta nyuma na kuanguka chini, ni lile jibu la “NDIO MIMI” kujitambulisha kwake Yesu kuliwafanya askari na watumishi wale kuanguka chini.

Hebu tafakari hili jambo kwa kina, kama mtu uliyeokoka, kama mtu uliye na Yesu moyoni mwako, kipi kinaweza kukutisha na wakati wewe mwenyewe umebeba jina lenye Utiisho?

Sauti yako ina nguvu kubwa sana yenye mamlaka, ndio maana kuna mazingira unaweza kuongea kitu hadi hali ya hewa ya mahali pale ikabadilika kabisa. Hiyo ni kwa sababu ya kulibeba jina la Yesu Kristo moyoni mwako.

Karibu kwenye darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku, wasiliana nasi kwa whatsApp namba +255759808081. Utaunganishwa kwenye group baada ya kukubaliana na kanuni zetu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com