Shida inayotesa vijana leo, ni kushindwa kuwa na nidhamu binafsi pasipo kuchungwa na mtu.

Wengi tunakuwa tumevaa kakofia fulani hivi cha upole, ila ndani yake si kweli.

Idadi kubwa huanguka dhambini na wachumba zao, madai yao ikiwa ilikuwa bahati mbaya.

Tunapozungumzia nidhamu binafsi, ni kujiheshimu wewe kama wewe pasipo kusubiri uonekane kwa watu.

Kukujijengea tabia hii ya kujiheshimu wewe kama wewe, inakufanya hata uliyenaye au wanokuzunguka waanze kujiuliza maswali…

Nidhamu ambayo tunaweza kuita tabia njema, inaongeza uwezo wa kujiamini mbele za watu na mbele za Mungu.

Huenda ulifanya vitu ambavyo vilipelekea mkaanguka dhambini, ama mlikuwa mna mpango wa kuelekea kutimiza kiu ya miili yenu. Naomba leo uchukue uamzi baada ya kusoma haya.

Imekuwa kawaida kabisa, vijana kutangaza uchumba madhahuni huku wameachiana nafasi fulani ya kumaanisha bado hawajawa mwili mmoja. Ila tayari wanakutana kimwili kila mara kama mke na mume.

Imekuwa kawaida wachumba kushikana shikana, wengine husema wanacheza michezo ya kimapenzi mpaka kupelekea kuamshana hisia za ngono.

Lakini wanapofika kwa watu, wanaonekana kwanza ndio wanaonana kwa jinsi wanavyoonyesha nidhamu ya uongo mbele ya macho ya watu.

Kijana wa kike/kiume, anaenda kwa mwenzake wanalala wote kitandani kwa madai hawafanyi kitu, zaidi wanabadilishana mawazo huku wakishikana shikana.

Hizi tabia zinavyoendelea siku kwa siku, zimezaa kitu ndani ya mioyo ya kila mmoja wao. Inafika kipindi hawawezi kupitisha siku pasipo kuonana na mwenzake kwa ajili y kufanya vitendo hivyo.

Inapokomaa hii tabia, wanajikuta wameingia kwenye uasherati… baadaye wanakuja kushtuka na kufunguliwa macho, tayari wamemalizana.

Kufanya hivyo, kinachofuata watajuta na kujisikia vibaya… kujisikia vibaya huko sio itawafanya waache, bali wataona ni mchezo fulani mzuri kwao pale wanapokumbuka ile michezo yao mibaya.

Michezo hii imepelekea mimba zisizo tarajiwa, imepelekea utoaji wa mimba, imepelekea kukimbiana, imepelekea kuacha wokovu pale mtu anapofika kipindi hawezi tena kuficha matendo yake.

Elewa kwamba kila tabia njema inataka maamzi ya mtu binafsi, hakuna miujiza kwenye hili. Ndio maana hata kwenye swala la kuokoka hakuna mtu atakushikia kisu/bunduki akulazimishe uokoke. Bali wewe na maamzi yako utahitaji kuamua.

Pia katika swala hili, hahitaji kuogopana bali inahitaji kuheshimiana ninyi kwa ninyi. Ndio maana kuna makanisa, wachumba wanaongelea mambo yao kwenye ofisi ya mchungaji ama kiongozi yeyote wa kanisa ama kanisani kabisa kwenye uwazi.

Ambapo leo hii kitu kama hichi hakipo, na kama kipo basi asilimia ndogo sana. Ukilazimisha wafanye hivyo watamalizana kwenye simu, kwa kifupi mambo yamebadilika.

Nikushauri kwamba, ikiwa huwezi kuji_control, ni bora usiwe na mwenzako katika mazingira ya peke yenu. Usikubali kukaa na mwenzako mazingira tata.

Kufanya hivyo, endelea kutengeneza tabia njema ya kuweza kujiendesha mwenyewe yaani mwili wako uwe una uwezo wa kuzuia vitu usivyovitaka wewe.

Zoezi hili sio la siku moja, lakini kwa kuwa unampenda Yesu…dhamiria kuokoka kweli kabisa na uachane na maigizo.

Epukana na marafiki ambao kazi yao ni kuongelea maneno machafu, ya jinsi wanavyowafanya wachumba zao. Bali kuwa na marafiki ambao unaona jinsi wanavyoishi na kumpenda Mungu katika roho na kweli.

Nidhamu isiwe mbele za watu, bali iwe ndani yako hata ukiwa kitandani/chumbani kwako mwenyewe pasipo mtu yeyote kukuona.

Kumbuka sijakuambia umwogope mwenzako bali nimekuambia nidhamu iwe katikati yenu. Wewe ni mtu mzima, uwe mtu mzima pia kwenye akili zako.

Chagua leo, onekana mshamba leo, nyima mwili tamaa zake mbaya leo, ili ujana wako na ukristo wako usilaumiwe.

Samson Ernest.

chapeo@chapeotz.com
+255759808081.