Kutangaza habari za Yesu Kristo, kuisema kweli ya Mungu bila kuangalia mtu usoni, kuihubiri injili isiyogushiwa na chochote. Inahitaji uwe na moyo wa ujasiri kweli, inahitaji uwe mtu uliyetulia vizuri, na uwe mtu mwenye mahusiano mazuri na Mungu wako.
Huhitaji uwe na nguvu nyingi za chakula cha mwili, hiyo haiwezi kukufanya ukapambana na changamoto za utumishi aliokupa Mungu. Unahitaji uwe umeshiba Neno la Mungu, unahitaji uwe umejaa nguvu za kutosha za maombi.
Utahubiri injili iliyonyooka bila kupindapinda, wapo watakaoipokea na kuamua kufanya maamzi sahihi ya kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao. Na wapo watakaojitokeza kukupinga, wapo watakaokasirishwa na injili uliyohubiri, wapo watakuweka ndani ya vyombo vya sheria, na wapo watakaokutukana matusi mabaya ya kukuzalilisha.
Ukishapata misukosuko ya namna hii, uwe na uhakika kibinadamu utasikia kuchoka, utajisikia vibaya moyoni mwako, na utaona unachofanya hakina faida yeyote. Unaweza kufika wakati ukaanza kujiuliza Mungu yupo pamoja na wewe, au tayari ameshakuacha peke yako.
Sio hivyo tu, unaweza kufika mahali ukaona labda unakosea kuhubiri kweli ya Mungu, unaweza kufikiri huenda hujui vizuri Neno la Mungu, unaweza kufikiri huenda unakosea kutafisiri maandiko matakatifu. Hii yote ni kwa sababu umekutana na vipingamizi vikali kwenye huduma yako.
Sisemi kwa wale wanaopotosha maandiko matakatifu, hao kupata upinzani mkubwa kwa wanachopotosha watu, ipo wazi kabisa. Ninachosema hapa ni kwa wale wanaoihubiri kweli ya Mungu, wanaokemea maovu waziwazi bila kupindishapindisha maneno.
Nakumbuka miaka ya nyuma wakati naanza kuhubiri injili kwa njia ya mitandao ya kijamii, nilipata upinzani mkubwa sana. Tena upinzani mkubwa niliokuwa naupata ni kwa ndugu zangu wa karibu mno, ikafika wakati nikaanza kuogopa kusema maneno makali yenye ukweli.
Nikisema naacha kusema, moyoni nasikia kuugua, nasikia kuumia mno mpaka najikuta nimerudi tena kuhubiri. Tena nakuja na kasi kubwa zaidi ya mwanzo, nikienda siku kadhaa, nakutana tena na vipingamizi vingine kwa marafiki zangu. Nilichoshindwa ni kule kuacha, maana huenda ningeacha usingesoma ujumbe huu ninaokuandikia hapa.
Leo nimekutana na andiko ambalo huenda ningekutana nalo wakati huo lingekuwa msaada sana kwangu, ila sipaswi kujilaumu, kwa sababu sikuacha kuhubiri Neno la Mungu hadi sasa. Ni kwa sababu ndani yangu kuna kitu kinachonisukuma kuhubiri/kufundisha kweli ya Mungu, haijalishi mazingira nitakayokutana nayo.
Ninachomshangaa Mungu alivyo na maajabu makuu, anaweka kitu ndani ya mtumishi wake ambacho kitamsaidia kutorudi nyuma. Hata pale atakapokutana na changamoto ngumu, kitu chenyewe anaweka kuugua moyo, unakosa amani kabisa pale unapoacha/unapotaka kuacha kulitumikia kusudi lake.
Ndio Maana ukifuatilia mitume wa Mungu waliotangalia, tunaona walipitia vipindi vigumu sana kwenye huduma zao za injili. Ila hawakuacha kumhubiri Yesu Kristo, wala hawakuikana imani yao, wengine walifungwa gerezani na wengine walidumbukizwa kwenye pipa la mafuta ya moto, hawakusema kuanzia sasa hakuna kulitaja tena jina la Yesu Kristo.
Tunapata kujua kupitia Neno la Mungu, ipo nguvu ya Mungu ndani ya mtumishi wake aliyemchagua, haijalishi atakutana na vikwazo vingapi. Huwezi kumkuta amenyamaza, kuna moto wa Roho Mtakatifu unawaka ndani yake, akijaribu kunyamaza utamuunguza mpaka atoke kusema.
Rejea: Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia. YER. 20:9 SUV.
Kama umefika mahali umechoka na umeona uachane na huduma uliyokuwa unafanya, na ndani ya moyo wako unajisikia vizuri kabisa na amani juu. Hapo ulijituma wewe, na ulikuwa unahubiri mambo yako binafsi yasiyomtukuza Yesu Kristo.
Mtumishi wa Mungu yeyote hawezi kunyamaza kwa habari za wokovu, hawezi kusema kuanzia sasa sitalitaja tena jina la Yesu Kristo, kwa sababu ya kuchekwa, kuzomewa, kufungwa, na kupigwa mawe. Atafanyiwa yote, ila kesho yake utamwona yupo barabarani anatangaza habari za aliyemwokoa na aliyemwita.
Mtu wa Mungu, huhubiri kwa matakwa yako, ipo nguvu inayokusuma kufanya hivyo, hufundishi, kwa sababu unapenda kufundisha, yupo anayekusuma kufanya hayo yote. Ukijaribu kuacha kile Mungu anataka ufanye, uwe na uhakika utajisikia kuugua moyo wako, utajisikia moyo unawaka kama moto umewashwa ndani yako.
Mungu akupe ujasiri na nguvu za kumtumikia yeye.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.