Haleluya mwana wa Mungu, saa nyingine tena ya kwenda kushirikishana tafakari nzuri za kujengana kiroho. Karibu ujifunze pamoja nami kupitia ujumbe huu, naamini hutotumia muda wako bure.

Kila mmoja wetu ni kiongozi, inategemeana na eneo alipo, kama sio kiongozi kanisani utakuwa kiongozi wa familia yako. Kama huna familia utakuwa kiongozi wa maisha yako mwenyewe yanayokutazama wewe uchukue hatua.

Tunapoongoza sehemu yeyote ile tunapaswa kuwa mstari wa mbele kwa wale tunaowaongoza, tunakuwa mstari wa mbele kwa matendo mema. Kama ni kuwajibika tunapaswa kuwa wa kwanza kuwajibika ili tunaowaongoza wakitutazama wapate kujifunza jambo jema kupitia sisi.

Hatuwezi kuitwa viongozi wema kama tunawapotosha wengine, hatuwezi kuheshimiwa na tunaowaongoza kama sisi wenyewe hatutajiheshimu. Tunaheshimiwa pasipo unafiki ndani yake kwa sababu ndani mwetu tunayo heshima ambayo inatutunza wenyewe.

Huwezi kuwa na nguvu ya kukemea uasherati kama wewe mwenyewe ni mchafu kupitiliza, kila utakapojaribu kuingia ndani zaidi umsaidie mwingine. Utasikia kutoka ndani ya moyo wako ukipiga kelele na shutuma zikikuandama ndani yako.

Tunakuwa na ujasiri wa kusimamia familia zetu kama sisi wenyewe tupo mstari wa mbele katika utendaji na utekelezaji wa majukum yanayotuhusu.

Utakuwa na nguvu ya kumsemesha kiongozi wako kazini kama unatekeleza majukumu yako kwa wakati, vinginevyo mkuu wako ataonekana adui yako. Kumbe sio adui bali uadui umeuleta mwenyewe kwa sababu ya kushindwa kwako kutekeleza majukum yako.

Mungu wetu pia ndivyo alivyo, hutupa nguvu na ujasiri zaidi wa kuitenda kazi yake. Kwa kuishi maisha Matakatifu yanayompendeza yeye kila wakati, Mungu anahusika sana na maisha yetu.

Mungu anakujaza nguvu zaidi zisizoelezeka kutokana na kuitenda kazi yake kwa utii wako, wa kuketi kwako na kulitii Neno lake. Kunakufanya kuwa wa viwango vya toafuti kutokana na uhitaji wa wale unaowahudumia.

Hizi habari tunaziona kwa mfalme Yothamu, aliyeishi maisha ya kumpendeza Mungu. Akazidi kuwa na nguvu zaidi katika utawala wake, sababu iliyo kuu iliyomfanya kufika hapo alipo. Ilikuwa kutii sheria za Mungu wake na kuzifuata asije akamtenda Mungu dhambi.

REJEA; Basi Yothamu akawa na nguvu, kwa kuwa alizitengeneza njia zake mbele za BWANA, Mungu wake. 2 NYA. 27:6 SUV.

Hebu jihoji mwenyewe, utawezaje kuwa na nguvu za kumtumikia Bwana, ikiwa unachanganya wokovu na upangani. Itakuwa ngumu sana Mungu kukuinua kwa michanganyo yako mibovu.

Walio mikononi mwa Mungu, wanatiwa nguvu Nyakati zote, itokee tu mhusika mwenyewe kukataa kutenda yaliyo mema mbele za Mungu.

Hebu tutengeneze njia zetu mbele za Mungu, ili Mungu wetu apate nafasi ya kuhusika na maisha yetu. Tunahitaji kutiwa nguvu maeneo mengi sana katika maisha yetu ya kiroho na kimwili.

Naamini umepata kitu, Mungu wangu wa mbinguni akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com