
Kuomba kibali cha kusema jambo fulani au kufanya jambo fulani kabla ya kulifanya hilo ulilolidhamiria, ni jambo la busara sana kwa mtu yeyote.
Haijalishi unafanya jambo zuri, kuomba kibali ni jambo la msingi sana, ni moja ya jambo ambalo linamuweka mtu kwenye nafasi fulani ya pekee kutokana na busara zake.
Hata ukiwa kama mtoto ambaye unaishi kwa wazazi wako (mtoto hakui kwa wazazi, ataendelea kuitwa mtoto na wazazi hata akiwa na familia yake) kuomba ruhusa kwa wazazi wako kwa jambo lolote lile ni vizuri sana.
Ukiomba ruhusa kwa mume/mke wako ni jambo la muhimu sana, usifanye jambo kienyeji bila kumshirikisha mwenzako. Kama jambo hilo sio la ghafla ni vyema kutoa taarifa mapema.
Mama omba ruhusa kama unaenda mahali, ni jambo dogo sana ila lina maana kubwa sana, tena unajijengea nidhamu njema kwa mume wako.
Baba toa taarifa kwa mke wako, umepata safari ya ghafla kiofisi toa taarifa kwa mke wako, usisafiri kienyeji bila kutoa taarifa.
Kuna watu ni rahisi kuomba ruhusa kwa maboss zao ila ni ngumu kuomba ruhusa kwa mke/mume wake. Acha hiyo tabia mara moja kama unayo.
Kuna watu ni rahisi kuomba ruhusa kwa michepuko(wake/waume wa nje) kuliko kuomba ruhusa kwa mke/mume wake halisi. Acha hiyo tabia mbaya kama unayo.
Tuwe tunaomba ruhusa, hata kwa viongozi wetu makanisani tuwe tunaomba ruhusa, awe mchungaji wako omba ruhusa, awe m/kiti wako wa kwaya, wa wamama, wa vijana, omba ruhusa.
Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu, utaona ni jinsi gani ilivyo vizuri kuomba ruhusa, utaona ni vizuri baada ya kujua kuwa hili jambo lipo kimaandiko.
Rejea: Paulo akasema, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, mtu wa Tarso, mji wa Kilikia, mwenyeji wa mji usiokuwa mnyonge. Nakuomba, nipe ruhusa niseme na wenyeji hawa. MDO 21:39 SUV.
Usimdharau mtu, hata mtoto wako wakati mwingine mwombe ruhusa, mwage mtoto wako, utakuwa umeanza kumjengea tabia njema ya kuwa mtu anayeomba ruhusa kabla hajafanya jambo.
Bila shaka umewahi kuona mtu akikuomba ruhusa huwa unajisikia vizuri, na kumwona mtu huyo ni mtu anayejali au anakujali na anatambua nafasi yako kwake.
Uwe mtu wa kuomba ruhusa kabla ya kufanya jambo fulani ambalo unajua bila kupata kibali cha mkuu, hutaweza kufanya vizuri lile ulilolikusudia kulifanya.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com