“Ndipo akafungua fahamu zao ili waweze kuyaelewa Maandiko”, Luka 24:45 NEN.

Tunaweza tusione ladha ya neno la Mungu ilivyo sawasawa, tukasoma na tusione msisimko wowote wa mguso ndani yetu, kutokana na kusoma kama habari zingine kwenye vitabu vingine.

Tunaweza kuwalaumu watu hawaelewi kile tunakifundisha au tunakihubiri tukifikiri wanafanya makusudi kutokuelewa yale tunawaambia.

Moja ya hitaji muhimu kumwomba Mungu ni juu ya ufahamu wako au akili zako au moyo wako uweze kufunguliwa, unapofunguliwa ufahamu wako utakuwa na uwezo wa kumwona Mungu akisema nawe kupitia maandiko matakatifu.

Mungu anaweza kuzungumza na mtu kupitia neno la Mungu akashindwa kumwelewa kabisa kutokana na ufahamu wake kutofunuliwa hilo neno, lakini anapofunuliwa anasikia kitu cha tofauti kabisa kwenye neno la Mungu.

Ndio maana ni muhimu sana kuombea ufahamu wetu uweze kufunguliwa au kufunuliwa vyema neno la Mungu, zipo faida nyingi sana za kufunuliwa maandiko matakatifu.

Maombi

Mioyo ya watu inaweza ikawa migumu sana kwa sababu bado haijafunguliwa, moyo ukifunguliwa unakuwa mwepesi kupokea kile Mungu amekikusudia mtu akipata au akipokee katika maisha yake.

“Mmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo”, Matendo 16:14 NEN.

Tuna haja ya kumwambia Bwana afungue mioyo yetu, akili zetu au fahamu zetu, tutaweza kuwa na kiu kubwa ya kusoma neno la Mungu, maana tutakuwa tunatamani kusikia Mungu anasema nini juu ya maisha yetu.

Huenda tunasikia kila mara neno la Mungu limebeba majibu ya mahitaji yetu au maswali yetu, tutaendelea kusikia hivyo kama ufahamu wetu hautafunguliwa kuweza kuelewa yale tunayoyasoma au kuhubiriwa au kufundishwa.

Amini ya kwamba ufahamu wako unaweza kukunyima mambo mengi muhimu ikiwa utakuwa umefungwa, na unaweza kukupa majibu ya maswali mengi ukiwa umefunguliwa na Mungu mwenyewe. Ambaye Roho Mtakatifu akiwa ndani ya mtu anaweza kumsaidia mambo haya yote, yeye ndiye hutufunilia yale tunayopaswa kuyafahamu.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest