“Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu”, Mwa 35:2 SUV.

Baada ya kuona matukio magumu katika sura iliyopita ya 34, katika sura hii ya 35 tunaona maelekezo ya Mungu akimpa Yakobo aende Betheli akamfanyie madhabahu. Eneo hili ni lile ambalo Mungu alimtokea Yakobo wakati amelala kipindi kile amemkimbia Esau.

“Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako”, Mwa 35:1 SUV.

Kuna kitu Yakobo alikiona kwa familia yake hasa uhusiano wao na Mungu, aliona hali ya kiroho haikuwa vizuri, akaamuru kuondolewa kwa miungu migeni yote iliyokuwa kwao, ili kumruhusu Mungu kuwafanya upya katika maisha yao.

Agizo hili lilikuwa halina utani kabisa, walipaswa kuondoa kila kitu kilichokuwa kinamchukiza Mungu, agizo ambalo hakupaswa mtu yeyote kulipuuza, maana ilikuwa ni nafasi nzuri kwao kumruhusu Mungu kuingia katika maisha yao.

Usafi huu wa kuondoa miungu ya kigeni ulikusudia Yakobo kurudi upya katika viapo vyake kwa Mungu, alivyoviapa kumwishia na kumwabudu yeye peke yake.

“Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi”, Mwa 28:20‭-‬22 SUV.

Jambo lingine muhimu ilikuwa kurejesha ushirika wake na Mungu na kuishi maisha yaliyo ndani ya msingi mzuri wa neno la Mungu, jambo ambalo lilikuwa muhimu sana katika maisha yake na watu wake.

Kufanywa upya kwa Yakobo kuliruhusu uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee sana, kulimwezesha tena kuona ulinzi wake, uwepo wake, ufunuo wake na baraka zake nyingi.

“Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako”, Mwa 35:9‭-‬11 SUV.

Tunajifunza nini hapa kupitia tukio hili? Lipo jambo kubwa sana la kujifunza katika maisha yetu, tunapoamua kurejea kwa Mungu au tunapoamua kuokoka, tunapaswa kuachana kabisa na miungu mingine ili tuweze kumruhusu yeye peke awe nasi katika maisha yetu.

Hatupaswi kubakisha jambo lolote la kumzuia Mungu katika maisha yetu, tuondoe vikwazo vyote vinavyosababisha kuondoa uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya wokovu, hili linapaswa kuwa jambo la kufanyia kazi kila mara katika maisha yako yote.

Tunaweza tukawa tunatembea ndani ya wokovu ila kuna vitu tumeviruhusu kuwa navyo katika maisha yetu vinavyoondoa uhusiano wetu na Mungu wetu, jambo ambalo ni hatari sana kwa maisha ya mkristo maana hataona uzuri wa wokovu katika maisha yake.

Tumeamua kumfuata Yesu, hili ni jambo jema sana katika maisha yetu, tunapaswa kutumia nafasi hii kuona mahali tulipoingia ni sahihi na hapahitaji kuchanganywa na miungu mingine ya mababu au ya mabibi, Yesu peke yake anatosha kabisa katika maisha yetu.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081