Kuna maisha unaweza kupita, ukafikiri kama vile dunia imekulemea, ila ukweli huwezi kubadilika kwa hali unayopitia.

Ndugu zangu mnaopenda kukaa kwa mashemeji, iwe mnapenda, iwe hampendi, ukishaanza kuona vituko kama hivi vya kuwekewa vikwazo kwenye chakula ujue wamekuchoka.

Upo nyumbani kwenu au kwa ndugu yako, ila huna kazi unayofanya ya kukuingizia kipato, na umeanza kukutana na maneno magumu ya kukuvunja moyo. Ujue wameshakuchoka.

Vipo vituko vingi sana ambavyo unaweza kukutana navyo kwa ndugu unayeishi kwake, hili huwezi kulikataa kama limeshakufika.

Wakati mwingine unaweza kujikuta upo njia panda kwa jinsi unavyotendewa vituko vya ajabu, na ukitazama nyuma unaona huna pa kwenda kwa wakati huo.

Yapo mazuri sana ya kujifunza kwenye eneo hili, pamoja na maumivu yote unayokutana nayo kwa walezi wako, marafiki zako, na shemeji zako.

Lipo la kujifunza kwenye changamoto hiyo ngumu unayokutana nayo, uwezo wa kupanga chumba unaweza usiwe nao. Maana ni wakati ambao bado hujaweza kujimudu, unapambana ili ufike mahali ukaweza kujitegemea.

Shika yafuatayo;

1. UNYENYEKEVU; pamoja na dharau unazokutana nazo, endelea kuwa mnyenyekevu, tazama malengo yako. Usitazame changamoto za muda mfupi, tazama kile kitakufanye uondoke hapo.

2. UVUMILIVU; hili linaweza kuonekana gumu kwako, ila nakwambia kama huyo unayeishi naye hajafikia hatua ya kukufanyia vitendo vibaya vya kukuzalilisha. Endelea kuvumilia wakati unaendelea kupambana kufikia malengo yako.

Siku ikiisha mshukuru Mungu wako, maana umesogea hatua kubwa ambayo inakufanya ukaribie kutoka kwenye kifungo hicho.

3. KUJITUMA; jambo unalopaswa kulijua na kulifanyia kazi kila siku, ni kuepuka uvivu, fanya kazi za nyumbani na zile zote unazoona unapaswa kuzifanya. Ninaposema ufanye kazi, namaanisha ujitume haswa usione aibu katika hilo.

Huo ndio wakati wako wa kujinoa, hapo ndio unaandaliwa kuwa baba bora, hapo ndio unaandaliwa kuwa mama bora. Hapo ndio unaandaliwa kuwa mfanyakazi bora ofisi unayoenda kuajiriwa baadaye, na hapo ndio mahali panakuandaa kuwa mfanyabiashara bora.

4. KUSAMEHE; pamoja na vituko vyote, pamoja na masimango yote unayokutana nayo kwa huyo unayekaa naye. Unapaswa kufahamu kwamba, kuachilia yote uliyotendewa ni jambo la muhimu sana.

Usiwe mtu wa kuweka vitu moyoni, mchukulie jinsi alivyo, chukulia ni fursa yako uliyoipata kumfahamu huyo ndugu yako kwa undani. Huenda usingekaa umfahamu alivyo kwa undani kama usingeishi naye.

5. CHUKI; usipandikize chuki kwa watoto wako, huenda hapo ulipo bado huna watoto, ila kesho itafika utakuwa na watoto. Usije ukaanza kuwapandia chuki kwa matendo mabaya uliyotendewa na huyo uliyekuwa unaishi naye.

Kama ulishasamehe, usiwe na kinyongo moyoni mwako, tafuta njia nzuri ya kuwaeleza/kuwashuhudia wanao. Na angalia ufahamu wao na namna wanavyochukulia mambo, ili kuendelea kudumisha undugu wenu.

ONDOKA NA HILI; hili jambo likutie hasira ya kutafuta pesa nyingi ili uweze kuweka mazingira yako vizuri, ili watoto wako wasije wakapitia changamoto uliyopitia wewe.

Hili jambo liwe fundisho kwako kutomfanyia mwanao, au mtoto wa mwingine, isiwe na wewe ukafanya yale yale uliyofanyiwa.

Tafuta kukua kiroho ili uweze kushinda haya….unapenda kusoma Neno la Mungu kila siku, karibu group la whatsApp la Chapeo Ya wokovu, tuwe pamoja kulisha mioyo yetu chakula cha kiroho.

Nashukuru sana kwa muda wako.
WhatsApp +255759808081.