Asifiwe Yesu Kristo aliye hai, wakati mwingine tena wa kwenda kushirikishana tafakari. Kaa mkao wa kupokea kitu katika somo hili.

Wakati una nafasi ya kupanda mbegu ya wema kwa watu wengine, unapaswa kufanya hivyo bila kuchoka. Endelea kupanda wema maeneo mbalimbali, pale unapopata nafasi ya kufanya hivyo.

Una nguvu za kufanya vitu mbalimbali, hiyo ni mbegu yako sasa. Endelea kuipanda kwa kutumika kwenye eneo unalopaswa kufanya hivyo, utafika wakati wa kuvuna matunda yake mema.

Jitoe kwa hali na mali kila mahali unapohitajika kufanya hivyo, hiyo ni mbegu yako itakayoenda kuota siku moja. Itakwenda kuzaa matunda yaliyo mema katika maisha yako ya sasa au ya baadaye.

Hakikisha asubuhi na jioni unapanda mbegu iliyo bora, haijalishi utapanda mbegu nzuri alafu ikazaa mapooza. Uwe na uhakika utaingia hasara upande mmoja, ila upande mwingine lazima uwe vizuri kwako.

Mfano mzuri kwenye harusi, ukiona harusi yako inakupa shida kuifanya. Hata kamati yenyewe haionekani wala watu hawana muda na wewe. Kaa chini ufikiri ulikuwa mtu wa kushirikiana na wenzako katika matukio?

Kabla hujaanza kumsingizia Mungu hakusikii maombi yako, fahamu kuna mbegu hukupanda mapema. Umesubiri wakati wa mavuno ndio unaanza kutapatapa huku na kule.

Mbegu hii inapaswa kuwepo hata kwenye kuwekeza, kama umepata nafasi ya kuwekeza miradi ya kutosha. Endelea kupanda Mbegu hiyo, hata kama kwa uchungu mwingi na kujinyima kwingi au kukosa kula vizuri.

Wekeza maeneo mbalimbali kwa kadri Mungu atakujalia kufanya hivyo, kama inawezekana kabisa uwekezaji mwingine uzae kwa wingi zaidi ya wa kwanza.

Rejea: Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri. Mhubiri 11:6 BHN

Usiache kutenda mema hata kama utakutana na maneno mengi ya kukatisha tamaa, fanya mema kwa kadri ya uwezo wako, wema huo ni mbegu isiyooza itayokusaidia wakati u mhitaji.

Eneo lolote lile la maisha yako, hakikisha unapanda Mbegu njema kwa wingi. Mbegu itayakuokoa kesho wakati wewe ulishasahau kama uliwahi kufanya hivyo.

Mungu akubariki sana.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081