
Msalaba una nguvu ya damu ya Yesu, kwa sababu damu ya Yesu ilimwagika kupitia huo msalaba .
Damu ya Yesu iliachilia nguvu katika msalaba, na kwa hiyo damu tunashinda dhambi, na kwa hiyo damu tunaona ushindi katika matendo ya mwili.
Ambapo chanzo chake ni ile sheria, maana kupitia hiyo sheria, dhambi ilipata nguvu na ikaendelea kututesa, hivyo katika roho zetu tunaweza kuishinda dhambi, lakini katika miili yetu nguvu ya dhambi inapiga kelele.
Ndiyo maana mtu unaweza kujaribu utende yaliyo mapenzi yake Mungu, lakini ukajikuta umetenda lile ambalo hujalikusudia kutenda.
Unatamani usimkosee Mungu kwa jambo lolote, lakini baada ya muda fulani, unashangaa umemkosea pasipo wewe kutaka.
Ngoja tuona maandiko yasemaje katika hili;
Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. RUM. 7:18-20 SUV.
Maandiko yanatuambia kwamba, kutaka kufanya lililo jema nataka, lakini sipati kulifanya, hapa tunaweza kuelewa ni kwanini kuna watu hata ajitahidi vipi kuacha kitu fulani, lakini utashangaa hawezi kabisa kuacha.
Kwa mtu ambaye hajaamua moja kwa moja kumpa Yesu maisha yake ili ayatawale, ni ngumu sana kwake kushinda eneo hili.
Kwa sababu siyo yeye atendaye kwa nafsi yake, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yake, kwakuwa katika mwili anajitahidi ili aache, lakini nguvu ya dhambi ndani yake inamtumikisha, ili asiweze kutenda lililo jema.
Utakuta mtu anasema! Natamani kabisa niache pombe lakini nimeshindwa.
Mtu anatabia ya uzinzi anatamani kuacha, akijaribu kujizuia siku mbili, ya tatu anarudi kulekule, ni kwa sababu ya ile dhambi inayomtumikisha, hivyo hana nguvu ya Mungu ambayo inaweza kumfanya ashinde,
Kwa mujibu wa neno la Mungu ambalo ndiyo KWELI (Yoh 17:17) hakuna jambo lisilowezekana mbele za Mungu.
Ukimkaribisha Yesu katika maisha yako, hakuna jambo litashindikana ndani yako, Damu ya Yesu inapoingia ndani ya mtu inadhoofisha ile nguvu ya dhambi iliyokuwa ikimtesa huyo mtu, lakini pia inaondoa kabisa hiyo kiu ya dhambi ndani yake.
Ndiyo maana Yesu alikufa ili sisi tuwe washindi si katika dhambi tu, bali katika mambo mengine pia.
Ukisoma YN 17:17 SUV inasema kwamba; Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
Kwa hiyo kazi ya neno la Mungu pia ni kututakasa, neno la Mungu pia linatuimarisha baada ya kututakasa, kutuongoza katika njia ya uzima wa milele.
Kama Mungu amesema nawe kupitia ujumbe huu, yamkini umo kanisani na kila siku unaenda kumwabudu Mungu, lakini kuna dhambi inayokutesa, au yamkini hujaokoka kabisa na unatamani kumpokea Yesu awe Bwana na mwakozi wa maisha yako, AMUA SASA NA YESU YUPO TAYARI KUKUPOKEA UWE MWANA WAKE.
Ujumbe huu umeandikwa na Rebecca Ernest.
Mungu akubariki sana.
www.chapeotz.com