“Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?” Mk 14:60‭-‬61 SUV

Katika maisha haya unaweza kujikuta upo kwenye shutuma fulani nzito, inaweza ikawa ni kweli, ama inaweza isiwe kweli.

Unaposhutumiwa jambo ambalo hujalifanya, inaweza ikakuumiza sana moyo wako na ukajisikia kuonewa kwa jambo ambalo hukuhusika nalo kabisa.

Nyakati kama hizi tunaweza kujikuta tunaongea sana na kutafuta huruma za watu, au kuonyesha jamii kuwa hatukufanya hilo na hatukustahili kuingizwa kwenye shutuma kama hizo.

Mtu anaweza kuangalia heshima aliyonayo na shutuma anazopewa, haziendani kabisa na vile anavyojiheshimu.

Shutuma huwa haziangalii heshima yako, wala haziangalii uaminifu wako, linaweza kuzuka jambo lolote zito kiasi kwamba unashindwa ufanye nini.

Nyakati kama hizi tunaweza kujikuta tunajitetea sana, tunaongea kupita kiasi, lengo ni kuonyesha kile tunachoshutumiwa sio kweli.

Yapo mazingira unaweza kujitetea sana au ukaongea sana, bado ukaonekana ni mwenye hatia. Unavyozidi kuongea ni kama unawapandisha hasira wale wanaokushutumu.

Upo wakati utapaswa kupunguza kuongea, unapaswa kuwa mtu mwenye maneno machache, muda mwingi unapaswa kuwa kimya.

Utaonekana kama una kiburi ila wewe utakuwa unajua nini unafanya, yanaweza kuongelewa mengi na watu wako wa karibu wakawa wanakutaka uongee neno.

Yesu ni mfano bora sana kwetu, linapofika suala la kushutumiwa kwa jambo lolote lile, tujue Yesu alishinda hizi shutuma nzito zilizokuwa zinamkabili.

Yesu alipewa mashitaka mazito ambayo kimsingi alipaswa kuwa mwongeaji au alipaswa kujitetea sana. Lakini kinyume chake alikuwa mkimya sana.

Tunapaswa kuelewa kunyamaza ni bora sana kwenye maeneo ambayo unaona watu hawana haja na maelezo yako. Hata kama utajitetea bado utatumikia kile walichokipanga kwako.

Faida ya kunyamaza, unampa nafasi Mungu akutetee, kuna mahali ungeongea usingeweza kueleweka hata kama ni fundi wa kuongea sana.

Hasara ya kuongea na kujitetea sana, unaondoa nafasi ya Mungu kukupingania kwenye shida iliyokupata, utaona kama unafanya vizuri ila utakuwa unajinyima fursa muhimu mbele za Mungu.

Narudia tena, haijalishi shutuma ulizopewa ni za uongo, haijalishi umenyimwa haki yako, angalia kuongea kwako sana kunaweza kukusaidia au unazidi kuongeza tatizo?

Haya yote utayaweza ukiwa umejaa moyoni mwako neno la Mungu, hili litakufanya usiongee ongee bila utaratibu.

Hakikisha unajaza kwa wingi neno la Mungu moyoni mwako, jiulize mara ya mwisho ulisoma lini neno na ukapata muda wa kutafakari.

Ukiwa una changamoto ya kusoma Biblia kila siku na kutafakari, usijali, tumekuandalia utaratibu mzuri wa kusoma Biblia kila siku. Wasiliana nasi wasap kwa namba hii +255759808081 ili uweze kuunganishwa kwenye group la wasap.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest