
Kumekuwepo na utata juu ya utozaji riba, wapo wanaosema kukopesha fedha kwa riba ni dhambi mbele za Mungu. Na wapo wanaosema kukopesha fedha kwa riba haina shida yeyote maana ni biashara kama biashara zingine.
Migongano hii imeleta shida kwa wengi hasa wale ambao wanasikia kukopesha kwa riba ni dhambi, baadaye tena anasikia mahali pengine sio dhambi.
Wapo wamebaki njia panda, hawajui ni sahihi, ama sio sahihi, na kama ni sahihi andiko lipi linathibitisha hilo kuwa ni sahihi.
Na wale wanaosema kukopesha fedha kwa riba au vitu kwa riba ni dhambi, ndio hao hao wanaoenda taasisi za kutoa mikopo wanakopa vitu kwa riba.
Mtu huyo huyo aliyekopa fedha au vitu kwa riba utamkuta mahali anasema kufanya hivyo ni dhambi mbele za Mungu, haipaswi kabisa mkristo kukopesha vitu kwa riba.
Wanaosema kukopesha fedha au vitu kwa riba ni dhambi, wapo sawa kabisa kwa mjibu wa andiko hili;
Rejea: Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba. KUM. 23:19 SUV.
Aliyekusudiwa hapa ni nani sasa? Aliyekusudiwa hapa ni ndugu yako, huyu ndiye Mungu aliwakataza wana wa Israel wasimkopeshe mwisrael mwenzao kwa riba.
Nje na mwisrael mwenzao waliruhusiwa kumkopesha kwa riba, sijui kama umeelewa hapo. Kama hujanielewa vizuri usiwe na shaka utanielewa kupitia mstari huu hapa chini.
Rejea: Mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki. KUM. 23:20 SUV.
Unaona hapo, aliyeruhusiwa kukopeshwa kwa riba ni mtu aliye nje na ndugu yao, lakini aliye ndugu(Mwisrael) hakupaswa kumkopesha mwenzake kwa riba.
Hayo ndiyo yalikuwa maelekezo ya Mungu mwenyewe juu ya wana wa Israel, hawakupaswa kumkopesha ndugu yao kwa riba ila kwa mgeni ilikuwa ruksa kukopeshwa kwa riba.
Mambo kama haya usipokuwa msomaji wa neno la Mungu utayumbishwa sana na maneno ya watu, lakini ukiwa msomaji wa neno la Mungu utata kama huu huwezi kuwa nao.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com