Pamoja na mizunguko yako yote hapa Duniani, unapaswa kujua kuna siku ya mwisho, siku ambayo itakuwa ni kulia na kusaga meno kwa wale ambao wataachwa na unyakuo wa Yesu Kristo.
Ukiwaza kwa akili za kibinadamu ni kama jambo lisilowezekana, ila sisi wana wa Mungu tunapaswa kufahamu ni jambo linalowezekana kabisa. Hakuna namna tutaweza kulikwepa hili.
Neno la Mungu halisemi uongo, Neno la Mungu ni amina, lolote litakalosemwa na Mungu kupitia Neno lake, uwe na uhakika lazima lifanyike kwa wakati uliopangwa.
Tunapaswa kujua kuna siku ya mwisho, pamoja na mizunguko yako yote hapa Duniani, usije ukasahau hili, hakikisha una maandalizi mazuri.
Usifikiri ukishakufa ndio habari yako imeishia hapo, uwe unajua utafufuliwa siku ya mwisho, bila kujalisha ulitenda mema au ulitenda mabaya. Wote mtafufuliwa kwa pamoja, wa jehanamu ataenda na wa peponi/mbinguni naye ataenda.
Sasa usije ukawa umekaa unasema hakuna siku ya mwisho, utakuwa unajidanganya mwenyewe, siku ya mwisho ipo na wale walio makaburini watafufuliwa.
Rejea: Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. YN. 5:28-29 SUV.
Kama uhusiano wako na Mungu haupo vizuri, vyema kutengeneza sasa ukiwa hai, hakuna nafasi nyingine ya kutengeneza uhusiano wako na Mungu. Wakati ni sasa, ukishapita huu muda, hutoweza tena kutubu au kuombewa na mtu mwingine wakati wewe umelala kaburini.
Jehanamu sio mahali pazuri, Jehanamu panatisha, ukishaingia huko utakuwa umeingia kwenye mateso ya milele. Kwa hiyo uchaguzi ni wako, kuchagua njia ya kwenda uzimani, au kuchagua njia iendayo jehanamu.
Uchaguzi upo mikononi mwako, kuchagua uzima wa milele au kuchagua mateso ya milele huko jehanamu, hakikisha unajiweka tayari wakati wote. Maana hujui saa wala dakika, atakapokuja mwana wa Adamu kulichukua kanisa lake.
Fanya mambo yote ila hakikisha mbinguni haukosi kuingia, sio upate raha Duniani alafu unaikosa mbingu, haitakuwa vizuri kabisa, na itakuwa fedheha kubwa sana.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com