Wengi wetu tunapoingia kwenye maisha ya ndoa halisi, wapo huanza kujuta na kuona ameoa/ameolewa na mtu ambaye sio sahihi kwake kutokana na mambo yanayoanza kujitokeza mwanzoni mwa ndoa yake. Utashangaa imekuwaje mtu aliyetoa shukrani mbele za Mungu kuwa amempa mtu sahihi wa kuishi naye, amegeuka ghafla na kuwa mtu ambaye sio sahihi kwake!

Kuna vitu anaanza kuviona vipo tofauti, kuna tabia zinaanza kuonekana ambazo kwenye uchumba hakuziona kwa mwenzake, kwa kuona hivyo anaanza kumtupia mwenzake lawama. Wengine huweka wazi kabisa kuwa wewe sio mtu sahihi kwangu nilikosea kukuoa/kuolewa na wewe.

Kauli kama hiyo na nyingine nyingi zinaweza kuleta sura tofauti kwa mmojawapo, zinapoleta picha isiyo nzuri kwa mmojawapo, wasipokuwa makini wanaweza kujiingiza kwenye ugomvi mkubwa mwanzo wa ndoa yao.

Zifuatazo ni moja ya sababu hizo zinazoweza kusababisha ndoa kuvunjika au kuwa na mafarakano;

  1. Uchanga Wa Kiroho

Ikiwa mmojawapo ni mchanga kiroho anaweza kusababisha ugomvi usioisha, mbaya zaidi mwenye changamoto hiyo ya uchanga hawezi kujiona au kukubali haraka kuwa ana shida hiyo. Yapo mambo atataka ayaendeshe kiroho wakati ni ya kimwili kabisa na anapaswa kuyafanya kama mwanandoa.

Mfano, mume anaweza akawa anahitaji tendo la ndoa ila kutokana na mke kuwa wa kiroho sana, anaweza kumzuia au kukataa kufanya tendo la ndoa. Anaweza kumwona mwenzake anapenda sana mambo ya mwili kuliko ya kiroho, hapa unaweza kuta mke ana maombi ya kufunga kila siku.

Wasipopata mshauri mzuri wa kuweza kuwasaidia wanaweza kuharibu ndoa yao kwa jambo dogo ambalo ukilisikia utasikitika, maana haikuwa na sababu ya kufika hatua ya kutengana au kuachana kwa sababu mume hampi haki yake mke.

Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu. 1 Kor 7:5 SUV

Muhimu sana kupatana na mwenzako kama mmoja wapo anahitaji kuingia kwenye maombi ya kufunga, vizuri akamshirikisha mwenzake, pia na mwombaji hapaswi kuwa na maombi bila kiasi. Nikiwa na maana maombi yasiathiri ndoa yenu, kama yataathiri basi ujue kuna mahali hujaenda sawa na umekosa maarifa sahihi.

2. Kuficha Mtoto

Watu wengi huwa hawapo tayari kueleza mambo yao yote kwa uwazi kwenye uchumba, hasa mahusiano yaliyopita kabla hajakutana na mwenzake waliyeoana. Unakuta mtu alikuwa na mahusiano na mwanaume/mwanamke mwingine na katika mahusiano hayo waliwahi kupata mtoto, na mtoto huyo alikuwa anaishi kwa mama yake au bibi yake na mwenzake hakuwahi kujua hilo.

Katika mahusiano yao ya uchumba hakuwahi kumwambia mwenzake kama ana mtoto, na wala mchungaji wake hajui kama ana mtoto aliyempata kabla ya ndoa. Ameficha hilo labda kutokana na kuogopa kukimbiwa na mchumba wake.

Wanapoingia kwenye ndoa rasmi na kuanza maisha mwenzake anakuja kugundua ana mtoto aliyempata nje ya ndoa yake, hapo ndipo vita nyingi huanzia na kukosa suluhisho kutokana na jambo hilo kufichwa hapo nyuma. Mungu asipoingilia katika hiyo ndoa inaweza kusambaratika mapema sana.

Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. Mit 28:13 SUV

Inawezekana kabisa umetubu mbele za Mungu juu ya kosa ulilofanya la kupata mtoto au watoto nje ya ndoa yako, yaani hukumficha Mungu ukawa umejiweka wazi mbele zake kama andiko linavyotuambia hapo, ila ukawa umemficha mume/mke wako asijue ujue hutafanikiwa kuficha siku zote.

Sisemi iwe matangazo kwa kila mwanaume anayekujia kutaka kukuoa au kwa kila mtu, unapaswa kuweka wazi kwa yule ambaye ameonyesha nia ya kweli au kamaanisha kuishi na wewe. Mwambie kwa uwazi, ukiona hilo ni gumu mwambie mchungaji wako amweleze, hii ifanyike kabla hamjatangaza uchumba madhabahuni, na ifanyike kabla ya kutolewa mahari.

3. Kushindwa Kupata Mtoto

Utoaji wa mimba umesababisha madhara kwa baadhi ya mabinti, wapo wameharibu vizazi vyao kwa utoaji wa mimba. Walipokuwa kwenye mahusiano ya uchumba walificha hili wakiwa wanajua kabisa hawawezi kuzaa tena kutokana na changamoto ya kuharibu kizazi, wanapoingia kwenye ndoa na kukosa mtoto, na wanapoenda kwa daktari ikabainika kuwa mke hawezi kuzaa tena, mahusiano hayo huingia kwenye shida na kupelekea kuvunjika.

Wengine huchelewa kupata mtoto kutokana na matatizo ya afya, inawezakana matatizo yakawa kwa mwanaume au mwanamke, hili huweza kuleta shida ndani ya ndoa. Wakati mwingine ndugu huingilia hili na kuwa sehemu ya kuwaumiza kwa maneno makali, maneno yanayogusa mioyo yao moja kwa moja.

Lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. 1 Sam 1:5-7 SUV

Hili la kushambuliwa kwa maneno alikumbana nalo Hana na wengine kwenye Biblia, Hana ni mfano tosha kuwa ndugu wanaweza kuwa sehemu ya kuleta shida kwenye ndoa. Ikiwa mke/mume hatasimama vizuri kama Elkana uwe na uhakika hiyo ndoa itasambaratika au itaingia kwenye mgogoro.

4. Mahusiano Ya Siri

Wapo wanandoa huingia kwenye ndoa wakiwa hawajaacha tabia zao mbaya, huendeleza mahusiano yao ya mapenzi na wale waliokuwa nao kabla ya kuoa/kuolewa. Wengi hukamatiwa kwenye sms za mapenzi, au kukutwa nao faragha, hili hupelekea kuvuruga ndoa zao siku za mwanzo kabisa wa ndoa zao.

Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. Mit 28:13 SUV

Biblia ipo wazi juu ya hili, ikiwa mwanandoa ataficha dhambi zake na kuendelea kuzifanya kwa siri hasa mahusiano ya siri mtu huyo awe na uhakika ataingiza ndoa yake kwenye shida. Njia ya kujiepusha na hili ni kukubali kuacha na kutubu mbele za Mungu, bomoa kabisa mahusiano yasiyompendeza Mungu.

5. Uchumi

Wengi hutumia gharama kubwa kwenye maandalizi ya harusi hadi kupelekea wengine kujiingiza kwenye madeni makubwa, mtikisiko huu unapoingia kwenye nyumba huanza kuibua mambo mengine ya kuvuruga Amani ndani ya nyumba na kupelekea ugomvi.

Wengine hukopa vitu vya ndani wanaposhindwa kutimiza makubaliano waliyokubaliana na aliyempa hivyo vitu, huja kuvichukua vitu vyao, jambo hili huleta aibu na fedheha ndani ya nyumba na kusababisha mgogoro unaovuruga ndoa.

Kwa kuwa fedha ni jawabu ya mambo mengi kama maandiko yanavyotuambia; Na fedha huleta jawabu la mambo yote. Mhu 10:19(b) SUV. Kwa kuwa mke hakujipanga kukabiliana na hili, wengi hugeuka na kuona walikosea kuolewa na mwanaume asiye na fedha, maana hataweza kununuliwa nguo nzuri, hataweza kwenda salon za gharama, na hatapata chakula kizuri na mengine mengi.

Ushauri, vizuri kuwa halisi, mchumba wako ajue mnaenda kuanza maisha ya kutafuta pamoja, na kama umeshaoa ni vizuri kukaa chini na mwenzi wako kuelezana hali halisi na namna ya kukabiliana nayo. Mwanaume usiwe muongo kumbuka hiyo ni ndoa na sio uchumba, kama ulizoea kuongea uongo mkiwa wachumba, tubu na mwambie mwenzako hali sio shwari, ninaamini atakuelewa ukimweleza katika hali ya upendo na kuonyesha kujuta juu ya uongo wako.

6. Wazazi/Ndugu

Unaweza kujiuliza mzazi anawezaje kuvunja ndoa ya mtoto wao, iko hivi; baadhi ya wazazi hupenda kujiingiza kwenye ndoa za watoto wao, hutaka wao ndio wawe waendeshaji wakuu. Unakuta maamzi mengi yanatolewa na wao, hadi bajeti ya familia hupanga wao, hakuna kitu watafanya bila kuruhusiwa na wazazi wao. Unakuta hii tabia anayo mwanamke/mwanaume anawasikiliza wazazi wake kuliko mume/mke wake, mmojawapo anaweza kuchoka/kuchukia na kusababisha ndoa kuharibika au kuingia kwenye mgogoro.

Wazazi tunapaswa kuwa makini sana katika eneo hili la ndoa za watoto wetu, hata kama tunahusika kuendesha maisha yao kwa kiwango kikubwa. Tuwafanye watoto wetu wajione sio tegemezi tena kwetu na kuwapa uhuru wa kuendesha maisha yao wanavyoona wao inafaa, hadi pale inapotokea wanahitaji wenyewe ushauri wetu.

Pia wanandoa wanapaswa kuwa makini juu ya hili, kama mwanaume unasikiliza sana wazazi wako au kama unaishi nao kwako na wao ndio wanapanga bajeti na sio mke wako ujue una shida na utamfanya mke wako ajione hana sehemu kwako.

Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Efe 5:31 SUV

Zingatia hili usije ukasahau, wewe uliachana na wazazi wako na kuambatana na mke wako, maana yake mjitegemee katika ndoa yenu, maamuzi yenu na mipango yenu inapaswa kutoka kwenu wanandoa. Ndugu au wazazi wanapaswa kushirikishwa kama itabidi kufanya hivyo vinginevyo hampaswi kuambiwa fanyeni hivi au msifanye hivi.

7. Kufanya Mapenzi Kinyume Na Maumbile.

Hii tabia ipo kwa baadhi ya watu, inawezekana ikawa kwa mwanamke au kwa mwanaume, anapoenda kukutana na hili kwa mume/mke wake huwa hawakubali kumtenda Mungu wao dhambi.

Nyie msiojua mnaweza mkajiuliza nini imeharibu hiyo ndoa na msijue haraka maana wengi huwa hawapo tayari kulisemea, hili linaweza kuwa tatizo lililopelekea ndoa hiyo kuvunjika au kuingia kwenye mgogoro. Muhimu sana kwa mwolewaji/mwoaji kutulia na kumwomba Mungu ampe mtu sahihi. Ngumu kujilazimisha kuishi na mume/mke mwenye tabia hii huku unajua ni chukizo mbele za MUNGU.

Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, WALA WAFIRAJI, WALA WALAWITI, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi. 1 Kor 6:9-10 SUV

Hii sababu inaweza kuvuruga ndoa yeyote ile hata ile ambayo sio changa, tunapaswa kuwa makini sana, kama kuna jambo unapaswa kuwa wazi mapema kabla ya ndoa ni muhimu sana ukafanya hivyo ili mwenzako afanye maamuzi mapema kabla hamjaingia kwenye ndoa.

Kuna vitu ukificha vikaja kugunduliwa vitakuletea shida, vyema ukaviweka wazi mapema ili visije vikakupa maumivu ya maisha yako, haina haja kuolewa/kuoa leo alafu siku chache baadaye ukaachwa/mkaachana. Utabaki na maumivu yasiyokuwa na sababu yeyote wakati ungeliepuka hilo kabla hamjafunga ndoa.

Pia kama una tatizo linalokusumbua na unajua linamkosea Mungu vyema kuomba msaada wa kiroho kabla ya kuingia kwenye ndoa, matatizo kama haya ya kufanya ngono na mtu wa jinsia yako au kinyume na maumbile ni jambo baya mbele za Mungu.

Mwisho, haya ni baadhi ya mambo yanayoweza kusababisha kuvunjika au kutengana kwa wanandoa, ukiyafahamu yanaweza kukusaidia kuepukana nayo na kumwomba Mungu akusaidie. Na ukiwa na maarifa sahihi Roho Mtakatifu anaposema nawe ni rahisi kumwelewa na kufuata maelekezo anayokupa.

Kwa masomo Zaidi ya kukupa bonyeza link hii Mahusiano – Chapeo Ya Wokovu (chapeotz.com)

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest

+255759808081