Asifiwe Yesu Kristo,

Wengi huwa tunafika hatua na kuona ukristo ni adhabu na unatunyima UHURU wa baadhi ya vitu, tunapofika hatua kama hizi tunaanza kutamani vitu vya nje ya ukristo.

Wakati mwingine tumeona wasiokoka wanafaidi sana vitu vingi na vizuri, kwa kujiona sisi tulio ndani ya ukristo unatubana sana kufanya maovu ya dunia hii.

Wengine tunaanza kutamani vijana na wazee wanavyokimbizana kwenye madisco usiku. Tunaona sisi kuna kitu tunakikosa, na tunafika hatua tunatamani sheria za Mungu zitabadilike.

Wengine wameona ni bora Mungu avunje kipengele cha ndoa, kinachosema mpaka kifo kiwatenganishe, ili apate kuoa mke mwingine, ili apate kuolewa na mume mwingine.

Huwezi amini yupo mkristo anaona ukristo ni adhabu kwake, maana unamzuia kunywa pombe, unamzuia kufanya uzinzi/uasherati, unamzuia wizi na rushwa.

Ukiona unaona wokovu umekubana sana, jua bado hujaamua kuokoka. Mtu aliyeokoka hawezi kuchanganywa na wanawake na kusema kuna watu wanafaidi vitu vizuri, kisa tu kamwona mdada mzuri amejaziajazia.

Hakuna siku utaona kunywa pombe ni kitu kizuri, ikiwa tu utaamua kuokoka kweli. Nakueleza kitu ambacho nakiishi, sijawahi kujuta kwanini niliokoka, wala sijawahi kuona kutenda uchafu ni jambo zuri na kuona nakosa kitu fulani.

Shida inayotukumba wengi ni kuokoka nusu nusu yaani vya nje bado unavitamani na vya ndani ya wokovu navyo unavipenda. Ndipo shida inapoanzia, ndipo utamwona dada alikuwa kanisani lakini kaolewa na mtu asiyemjua Kristo. Ndipo utamkuta mkaka amemjaza mdada mimba huku yupo kanisani, ndipo utamkuta mkaka anaishi na mdada ndani kwake huku hawajaoana.

Ukiamua kumkabidhi YESU Kristo maisha yako yote na kwa moyo wako wote, nakwambia hutokaa useme haya masheria ya ukristo mbona mengi sana. Badala yake utafurahia wokovu na maelekezo yake, na mazuio yake, na makatazo yake.

Neno la Mungu linathibitisha hili;

Sheria ya Bwana ni kamilifu, Huiburudisha nafsi. Ushuhuda wa Bwana ni amini, Humtia mjinga hekima. Maagizo ya Bwana ni ya adili, Huufurahisha moyo. Amri ya Bwana ni safi, Huyatia macho nuru.Tena mtumishi wako huonywa kwazo, Katika kuzishika kuna thawabu nyingi. Zaburi 19 :11 SUV.

Hebu jihoji mwenyewe kwanini huwa unachukia maonyo ya Neno la Mungu, kwanini ukisikia kufanya uasherati kabla ya ndoa unajisikia hasira na kuchukia, kwanini ukiambiwa usiwe na tabia fulani mbaya unajisikia kukasirika. Badala ya kujuta mbele za Mungu na kuomba toba ya kweli, unajisikia moyoni kumchukia anayekueleza kweli ya Mungu? Badilika!

Tena NENO LA MUNGU linasema wakati wengine wameanguka na wameng’ang’ania hapo hapo bila kutubu na kuacha yale yanayomkosea Mungu. Wale wenye Mungu ndani yao, wale wenye sikio la kusikia na kuonywa, wameamua kujirudi na kuendelea na Mungu wao.

Rejea; Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama. ZAB. 20:8 SUV.

Usikubali kuanguka alafu ukaendelea kulalia uovu wako, inuka haraka utubu ili usimame tena. Usilalie dhambi itakuangamiza vibaya sana, dhambi itakufanya uone wokovu ni adhabu.

Tumejifunza sheria za Bwana hufurahisha moyo wa mwamini, hakuna mzigo wa kuzifuata sheria za Bwana kwa mtu aliyeamua kutoka ndani ya moyo wake kumfuata Yesu Kristo.

Mungu akuinue moyo wako ili uweze kuufurahia wokovu wako kwa kuzikataa tamaa mbaya, na kufurahia maelekezo ya Neno lake.

Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.