“Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu”, 1 Tim 1:20 SUV.

Linaweza likawa neno la kushangaza kusikia Shetani amepewa watu awafundishe, Shetani ambaye tunamjua ni baba wa uovu Leo hii anakabidhiwa watu awafundishe.

Paulo kuwakabidhi waamini kwa Shetani inaonyesha walishindikana kabisa kutokana na tabia zao mbaya mbele za Mungu.

Inaonyesha hawa watu wawili yaani Himenayo na Iskanda walitengwa na kanisa kutokana na mienendo yao mibaya.

Tunapoupokea wokovu na tunavyokuwa na muungano wetu katika kanisa, tunaabudu pamoja  na kushirikiana mambo mbalimbali katika ibada tujue kuna ulinzi mkubwa wa Kimungu upo katikati yetu.

Kuondolewa kanisani au kwenye kundi la waamini, kunayaweka wazi maisha ya mtu na kufungua mlango wa mashambulizi ya uharibifu ya Shetani.

“Mkabidhini mtu huyu kwa Shetani, ili mwili wake uharibiwe, ili roho yake iokolewe katika siku ya Bwana”, 1 Wakorintho 5:5 NEN.

Wengi huona mtu kutengwa na kanisa au kuondolewa kwenye kanisa ni kitendo cha kikatili na kisichofaa kabisa.

Tunapaswa kuelewa huu mfumo ni wa Kimungu, wapo watu tabia zao huzidi na huanza kuleta athari kwa kanisa, zisiposhughulikiwa huleta madhara makubwa.

Mtu kuadabishwa na kanisa husaidia kumrejesha au kumleta kwenye toba, Imani ya kweli na wokovu katika Yesu Kristo.

Ukiwa kiongozi hupaswi kuogopa kumchukulia mtu hatua pale anapoenda kinyume na utaratibu wa Mungu, hasa yule aliyeonywa mara nyingi na akawa hataki kusikia.

Kupitia njia hiyo unaweza kumwokoa yeye na kanisa kwa ujumla, maana wapo watu wasipoona mwenzao amechukuliwa hatua kwa jambo baya alilolitenda ni kama umewaambia ruksa kufanya mpendacho.

Jilinde usikabidhiwe kwa Shetani yaani usitengwe mbali na wenzako, unaweza kujiona ni sawa ila unapaswa kujua Shetani anaweza kukushughulikia vile apendavyo maana umeondolewa kwenye usalama.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081