Kuna umhimu mkubwa sana wa kumsikiliza Roho Mtakatifu kwanza, kabla ya kuchukua hatua yeyote. Ndio maana ni muhimu sana kutumia muda mwingi kumtafakari Mungu wako.
Yapo mambo unaweza kufanya kienyeji, badala kuwa baraka kwako, yakawa balaa kwako. Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, jifunze kusikiliza amani ya moyo wako, amani inayoletwa na Roho Mtakatifu.
Tenga muda wako kusoma Neno la Mungu, pata pia muda wa kutafakari kwa kina yale uliyojifunza. Utaona Mungu akikufundisha mambo mengi sana ya kukusaidia katika huduma yako aliyokupa Mungu.
Mungu anaweza kukupa huduma nzuri sana, ila ukawa huna muda wa kukaa naye, ili umsikie anakupa maelekezo gani. Muda anaotaka kusema nawe, unakuwa bize na mambo yako, wakati mwingine huna hata cha maana sana unachofanya.
Hapa tunajifunza kwa nabii Yeremia, alipokea maagizo kwa Mungu, kuwa asipate shida ya kuanza kumwomba Mungu kwa ajili ya watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu. Mungu hatayasikia maombi yake, hii ni baada ya Mungu kuwaonya sana, lakini hawakusikia.
Rejea: Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, walakini sitawasikiliza. YER. 11:11 SUV.
Ukisoma vizuri hii sura ya 11 katika kitabu cha Yeremia, utaona ni jinsi gani Mungu alishawaonya watu hawa kupitia kwa nabii wake. Ila hawakusikia maneno ya Mungu, wakaendelea kutenda mabaya yanayomchukiza Mungu. (Soma Yeremia 11:10)
Sasa unaweza kujipinda ukamwombea sana mtu, kumbe Mungu alishamkataa. Kwanini amkatae? Alishatuma sana watumishi wake wamweleza ukweli aache njia zake mbaya amrudie Mungu wake.
Pamoja na kuambiwa sana, hakuwasikiliza watumishi wa Mungu, huenda alifikia na hatua ya kuwajibu vibaya. Sasa Mungu anapoachilia adhabu ya mabaya juu yake, alafu akatoa na oda kabisa, kwamba hakuna kuomba juu ya huyu mtu. Uwe na uhakika hata ukiomba hakuna kinachoweza kubadilika.
Mungu anaweza kumpiga mtu na ugonjwa usioleweka, ataenda kila hospital lakini hatopata suluhisho la ugonjwa wake. Uwe na uhakika hata uombe maombi gani, Mungu hatoyasikia, maana amesema mwenyewe.
Rejea: Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao. YER. 11:14 SUV.
Mungu atakuletea ujumbe wake kabla ya kuruhusu mabaya juu yako, Mungu atakupa ujumbe wake ili umrudie yeye. Hatakulazimisha, amekupa akili za kuweza kufanya maamzi, amekupa masikio ya kuelewa kile watumishi wake wanasema. Amekupa kufahamu kusoma Neno lake, anapokuonya anatazamia uchukue hatua za kuacha njia mbaya.
Utakapoenda kinyume na hapo, siku ya hukumu huna cha kujitetea, kama ni neno lake ulisikia, kama ni injili ulisikia ikihubiriwa.
Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, lichukue hili litakusaidia katika utumishi wako aliokupa Mungu. Maana ukiwa kama mtumishi, lazima utakuwa na mzigo wa maombi ndani yako.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081