
Miongoni mwa vitu adimu sana na ambavyo huwezi kuvikuta kila eneo, ni kumkuta mwanamke mcha Mungu, kumkuta dada aliye siriazi na Mungu, kumkuta mama aliye siriazi na Mungu.
Mwanamke ambaye huwezi kumkuta kwenye makundi ya umbeya, mwanamke ambaye huwezi kumkuta kwenye kundi la kugombanisha watu. Mwanamke ambaye huwezi kumkuta kwenye kundi la kuchukua waume za watu.
Mwanamke ambaye yupo vizuri nyumbani kwake, hana dharau kwa mume wake, uboss wake au uheshimiwa wake mwisho mlango wa ofisi au kazini kwake, akiingia nyumbani mwake yeye ni mke. Mke anayepaswa kuwajibika na kumsikiliza mume wake.
Mwanamke ambaye ni mkarimu wa wageni, si mchoyo, wala si mnyimifu wa vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wake. Hachoki kujitoa kwa mambo ya Mungu, maana anampenda Mungu.
Mwanamke ambaye hata kama amechelewa kuolewa, huwezi kumkuta amejiunga na vikundi vya wanawake ambao wamekata tamaa ya maisha. Wanaona bora wazae tu, mwanamke mcha Mungu huwezi kumkuta kwenye kundi hilo.
Anajua hamchi Mungu kwa ajili ya kutafuta mume, ataendelea kulitumikia kusudi la Mungu huku akijua ipo siku yake atapata mume wa kumwoa, maadamu anajua analo hitaji hilo moyoni mwake.
Mwanamke mcha Mungu ni jasiri, kama ameolewa anaweza kugeuka faraja kwa mume wake anayepitia changamoto ya uchumi/kifedha. Huwezi kumkuta akimtangaza mume wake vibaya kwa watu nje, pale mume wake amekata tamaa yeye ndiye mtu wa karibu yake kumtia moyo.
Ni watu adimu sana ila wapo Tanzania hii hii, wapo mkoani kwako, wapo kanisani kwako, na wapo mtaani kwako japo ni wachache ila wapo. Huenda wewe unayesoma ujumbe huu ni miongoni mwao wa wanawake wacha Mungu.
Rejea: Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha. MDO 16:14-15 SUV.
Umeona hapo juu kwenye hilo andiko, sifa ya mwanamke mcha Mungu, kwanza hawezi kukaa kizembe ni mtu wa kujishughulisha(mwenye kuuza rangi za zambarau), anatunza Maneno ya Mungu moyoni mwake na si maneno ya umbeya umbeya(ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo)
Mwanamke ambaye anashurutisha watumishi wa Mungu kufanya kitu ambacho anajua ni hitaji la mtumishi(ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akawashurutisha), inaweza ikawa chakula akamshurutisha mtumishi kula, inaweza ikawa sehemu ya kulala wakati wa huduma kama tunavyoona kwenye hilo andiko takatifu.
Mwanamke yeyote mwenye sifa hizi za ucha Mungu, hawezi kukosa mume wa kuoa, Ninaposema mwanamke mcha Mungu najumlisha na mabinti ambao hawajaolewa. Kusema mwanamke simaanishi tu aliyeolewa, hapana, hata asiyeolewa ni mwanamke.
Hakikisha unakuwa miongoni mwa wanawake ambao ni wacha Mungu, na wanawake wacha Mungu sio wavivu, bali ni wachapa kazi, hawana muda mchafu wa kudhurura kwenye majumba ya watu, hawana muda wa kushinda salon kuongea upuuzi.
Mungu akubariki sana mwanamke mcha Mungu.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081.