Ninamshukuru Mungu wa mbingu na nchi kwa fadhili zake kuu kwetu, sifa na utukufu namrudishia yeye kwa kuwa ni mwema kwetu.
Kuna mazingira tunapitishwa kiasi kwamba tunaona mambo yanakuwa magumu kwetu na tunaona tulipofika uwezekano wa kuvuka ni mgumu mno.
Hebu fikiri mwanamke mmoja mwenye tabia chafu anamiliki mume wako bila aibu yeyote, mume wako anaacha kukutunza wewe kama mke wake na watoto wako. Anaenda kumtunza mwanamke mwingine kabisa ambaye hata hajui mlipotoka na mume wako.
Anatokea mke wako anatembea na mwanaume mwingine, huku kwako akiendelea kukuletea vituko ndani kwa sababu tu yupo mwanaume anampa kiburi cha kumfanya hivyo.
Umefika wakati unaona kama vile dunia inakuzomea, mume wako hakusikii tena, mke wako hakusikii tena, kila ukiomba Mungu amrejeshe mume/mke wako kama vile ndio kwanza umechochea moto uendelee kukuangamiza.
Hata yule anayetembea na mume/mke wako wala haoni aibu yeyote, zaidi sana anakucheka na kujiona yeye ndio mjanja zaidi yako. Hata marafiki zako mliokuwa nao mwanzo wamefika kipindi wamekutenga yaani ni kama maumivu juu ya maumivu.
Huenda hapo ulipo umeachiwa watoto wako na wewe ni mwanaume, mama yao ameenda kwa mwanaume mwingine. Umejaribu kusulihisha kila eneo imeshindikana.
Huenda hapo ulipo unatunza watoto wako peke yako na mume wako amehamia kwa mke mwingine, ameona aende kabisa na kukuonyesha waziwazi kuwa anaishi na mke mwingine.
Umeenda kwa wazazi imeshindikana, umeenda kwa wachungaji imeshindikana, umeenda kwa wazamini wenu imeshindikana, na umeenda kwa marafiki zake napo imeshindikana.
Lakini ninazo habari njema kwako za ushindi kwako, haijalishi ulifika kipindi ukaona maisha yako hayana tena maana kwako. Huenda ushaanza kufikiri kuuza biashara zako upotelee mbali, huenda kazini kwako boss wako alishaanza kufikiri kukufukuza kazi kutokana na utendaji na ufanisi wako wa kazi kupungua.
Lakini leo ukienda mbele za Mungu kwa kutubu na kunyenyekea, ataenda kubadilisha taarifa mbaya kuwa taarifa njema. Mwambie Mungu nimeteseka vya kutosha sasa nimetambua ya kwamba unaweza yote.
Mume aliyechukuliwa na mwanamke mwingine sasa anaenda kurejea kwako kwa jina la Yesu Kristo Wanazareti, sasa mke aliyeibiwa na adui sasa anaenda kurejea tena. Ndoa yeyote iliyokosa amani ndani kwa sababu ya mpuuzi mmoja aliyekuwa anatembea na mwenzi wako, sasa upanga unaenda kumgeukia yeye.
Wale wote walioiba furaha yako na wewe kubakiwa na huzuni, sasa Bwana anaenda kuirejesha furaha yako. Na huzuni iliyokutesa siku nyingi sasa inaenda kuwarudia maadui zako.
Unajiuliza sasa ndugu unasema nini, hizi habari unazitoa wapi na mimi nimeteseka miaka ya kutosha. Ninasema habari njema kutoka ndani ya biblia, tunaona malkia Esther akimiliki nyumba ya adui yao Hamani na Mordekai akimiliki kiti alichokalia Hamani.
Kile alichoandaa Hamani kwa ajili ya Mordekai kiligeuka kaburi lake, kile kibaya kilichoandaliwa kwa Wayahudi sasa kinageuka furaha na shangwe badala ya huzuni waliyokuwa nayo.
Rejea; Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu. Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani. EST. 8:1-2 SUV.
Kama uliona wokovu hauna maana tena kwako, rudi upya mbele za Mungu yeye ndiye tumaini la kweli, yeye ndiye mtetezi wako. Haijalishi taarifa uliyonayo ni mbaya kiasi gani itaenda kubadilika kuwa Nzuri, hakuna aliyefikiri Hamani atageukiwa na mfalme Ahasuero.
Udanganyifu wote uliofanyika na Hamani uligeuka kaburi lake, je wewe mwana wa Mungu si ndio zaidi? Mwamini Mungu wako atakushindia na utakuwa shuhuda kwa mataifa.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.