Leo tumeingia mwaka mpya 2019, huenda ni mwaka ambao ulikuwa unausubiri sana kwa hamu kubwa kutokana na changamoto ngumu ulizokumbana nazo mwaka uliopita 2018.

Mwaka mpya sio kana kwamba unaweza kumaliza changamoto zako, isipokuwa mtazamo wako unaweza kubadilika namna ya kuzitama hizo changamoto zako.

Kubadilika kwenyewe kunakuja pale unavyoanza kusikia maneno mengi ya mwaka mpya, kutokana na maneno mengi ya kukuhamasisha kuanza mwaka mpya na mambo mapya. Unaweza kujikuta unaona ile changamoto yako si kitu tena.

Lakini ukweli ni kwamba changamoto yako ipo palepale, isipokuwa mtazamo wako umebadilika ndani yako, huenda ungepata maneno kama hayo kabla mwaka mpya hujafika. Ungeiona kama unavyoweza kuiona mwaka mpya.

Kwahiyo mwaka mpya una faida zake kwa watu ambao wanapata nafasi za kuhudhuria mikusanyiko mbalimbali ya ibada ama wale ambao wanapata nafasi ya kusoma jumbe mbalimbali zenye nia njema ya kuwabadilisha maisha yao.

Tunapoingia mwaka mpya, kelele zinaweza zikawa nyingi sana, sio kelele tu, unaweza kukutana na jumbe nyingi sana za kukufanya uchukue hatua za kuboresha maisha yako ya kimwili na kiroho.

Ukiachana na jumbe mbalimbali za kukuhamasisha, wewe mwenyewe unaweza ukawa na mipango mikubwa sana ya mwaka huu mpya. Moja ya mipango yako inaweza ikawa kumpendeza Mungu wako zaidi au kumtumikia Mungu kwa nguvu zako zote.

Pamoja na hayo yote uliyopanga kufanya mwaka huu mpya wa 2019, hakikisha unajiwekea utaratibu mzuri zaidi wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Lengo lako la kwanza liwe kusoma Neno la Mungu, huenda tayari umeshapanga malengo yako mengine, ila hili la kusoma Neno la Mungu lipe kipaumbele kikubwa.

Kuliweka hili jambo la kusoma Neno la Mungu liwe la kwanza utakuwa umefanya kitu cha msingi sana, hayo mengine yatafanikiwa tu maana utakuwa umechagua kuwekeza kwenye maarifa sahihi. Maarifa ambayo yakiwa ndani yako unakuwa salama kiroho na kimwili.

Tanguliza mambo ya Mungu mbele, jambo hilo mojawapo la kutangulizwa ni kusoma Neno la Mungu kila siku kwa bidii zako zote. Hakikisha unaenda katika mtitiriko mzuri wa kukusaidia kufikia Lengo lako.

Rejea: Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Zaburi 119:11.

Ndugu yangu, kama mwaka huu mpya unataka kukua kiroho, na unataka usiwe mtu wa kuanguka anguka dhambini, hakikisha Neno la Mungu linajaa moyoni mwako.

Shetani hutaogopa kukujaribu kwa sababu umefunga sana kwa maombi, utajaribiwa tu na shetani, ukiwa huna Neno la Mungu moyoni mwako. Maana ni rahisi sana kuingia/kunasa kwenye mtengo wa shetani.

Weka Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako, imarisha wokovu wako kwa kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako. Utaona baraka nyingi sana za Mungu zikikujia kwenye maisha yako mwaka huu mpya 2019.

Kama ni mwimbaji utaona uimbaji wako ukipanda kiwango kwa sababu Neno la Mungu linakuwa limejaa moyoni mwako, hata wimbo unaoandika unakuwa umetokana na Neno la Mungu. Unakuwa ni ujumbe unaogusa maisha ya watu na wakisikia wanabadilika, maana Neno la Mungu limewagusa moja kwa moja kupitia wimbo.

Kama ni mhubiri/mwalimu wa Neno la Mungu ndio kabisa, viwango vyako vya kuhubiri au kufundisha havitakuwa viwango vya kawaida, vitapanda zaidi ya ulivyokuwa mwanzo. Utasema mbona sasa hivi Mungu ananitumia sana, ndugu kama hujishughulishi kulijaza Neno la Mungu moyoni mwako, unajiandaa kwa anguko.

Kumtenda kwetu Mungu dhambi, imechangiwa kwa kiasi kikubwa sana kukosa Neno la Mungu mioyoni mwetu, laiti Neno la Mungu lingekuwa limejaa sawasawa mioyoni mwetu, tusingeanguka kizembe kwenye dhambi.

Kama unaona ni changamoto kujisimamia mwenyewe kusoma Neno la Mungu kila siku katika mtitiriko mzuri, karibu sana kwenye kundi la Chapeo Ya Wokovu. Hapa utakutana na watu wenye bidii ya kujifunza Neno la Mungu, sio hilo tu, mimi mwenyewe nitakusimamia kuhakikisha unasoma Biblia yako. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Ukichagua hili jambo la kusoma Neno la Mungu kila siku, mwisho wa mwaka huu utajipongeza sana na utamshukuru Mungu wako kwa hili uliloamua kufanya.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com