Tunahitaji kuongozwa ili tuweze kufika mahali ambapo ni sahihi kwetu kufika, bila kuwa na kitu kinachoweza kutuongoza hatutaweza kufika mahali ambapo ni sahihi kwetu.

Mchana utaongozwa na mwanga wa jua, hata kama jua litakuwa limefunikwa na mawingu mazito, bado jua litaweza kutupa mwanga wa kuweza kutembea vizuri kabisa bila kutumia kifaa chochote za kutusaidia kuona.

Inapofika wakati jua likazama na usiku kuingia, tutahitaji mwanga wa kutusaidia kuona vizuri njia tunayotembea, bila mwanga tunaweza kudumbukia kwenye mashimo.

Magari yakikimbia usiku bila taa, hayo magari lazima yagongane tu, haijalishi barabara ni nzuri sana, bila kuwa na taa italeta shida kubwa kwa watu. Kwa hiyo mwanga wa jua ni wa muhimu sana, na mwanga wa taa ni wa muhimu sana.

Tukiwa kama watu tuliokoka, maisha yetu ya wokovu tunakuwa kama tupo safari ya kuelekea mkoa/nchi fulani, tunapokuwa tunasafiri, bila kujalisha gari limejaa mafuta na watu wamejifunga vizuri. Mtahitaji kupata kifaa cha kuweza kutoa mwanga mzuri.

Neno la Mungu ndilo litupalo mwanga, tukiwa na Neno la Mungu hatuwezi kujikwaa njiani, kila tutapokuwepo iwe mchana au iwe usiku. Tunayo taa ya miguu yetu, taa ambayo inatupa mwanga wa kutosha kwenye safari yetu ya wokovu.

Rejea: Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ZAB. 119:105 SUV.

Ukiwa na Neno huwezi kujikwaa na kisiki kilicho njiani, huwezi kuparamia mashimo, wala huwezi kugongana na mwenzako kwa sababu ya giza. Taa ya maisha yako ni Neno la Mungu, ili usikosee njiani kwenye maisha yako ya wokovu, hakikisha Neno la Mungu linajaa moyoni mwako.

Bila Neno la Mungu maisha yako ni giza, hakikisha unaepukana na maisha ya giza, kutembea kwenye giza tororo ni vibaya sana. Sio kana kwamba hujaokoka, kuokoka unakuwa umeokoka ila unakuwa huna Neno la Mungu moyoni mwako.

Mwaka huu mpya uwe mwaka wako wa kuweka nguvu zako zote kwenye Neno la Mungu, angalia vitu gani vilikukwamisha usiweze kusoma Neno la Mungu kwa mtiririko mzuri wa kusoma kila siku.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com