Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana. Ameona vyema kutuzawadia siku ya leo tuwe miongoni mwa watu wake waliobahatika kuiona leo. Leo ni ya thamani sana kwako kuliko jana iliyopita, maana huenda jana ikawa inakuumiza kutokana na kosa ulilofanya, ila leo unao uwezo wa kurekebisha na kutubu pale ulipokosea.

Muda mwingine tunafanya vitu kwa uzembe kwa sababu tunajua tunao muda wa kutosha kuwa nacho, lakini inapogeuka kinyume chake huwa tunaanza kutamani tupewe nafasi ya pili kukimiliki. Wakati inakuwa haiwezekani tena kuwa nacho, maana vipo vitu vikishaondoka vimeondoka.

Leo unaweza kucheza na umri wako wa ujana, itafika muda utautamani muda uliochezea wakati u kijana. Utatamani siku zirudi nyuma lakini haitawezekana tena kwa wakati huo, ila kwa sasa ukiwa bado mwenye nguvu unaona kila kitu kawaida kawaida.

Leo mtu anamchukulia mtoto wake kawaida, tena wakati mwingine hajui maendeleo yake ya shule yakoje. Ila ikitokea yule mtoto amekutwa na tatizo mbaya ambalo wakati mwingine limetoa uhai wake, ndio anaanza kukumbuka umhimu wa yule mtoto wake.

Leo hii mtu hamtunzi/hawatunzi wazazi wake, wala hawajali sana hata pale wanapomletea mahitaji yao ya msingi na mara nyingine wanaumwa huko walipo lakini hajali sana. Hata ile kusema awe karibu nao hataki, kwa kujiona yupo na mambo mengi sana, ila ikitokea wamekufa ndio anazinduka kwenye ufahamu wake.

Vitu vingi sana tunavipuuzia tukiwa navyo, ila vikishapotea na hatuwezi kuwa navyo tena ndio tunaanza kuonyesha upendo kwenye hivyo vilivyopotea. Leo mtu alikuwa hawajali wazazi wake, baada ya kufa ndio anaanza kufanya mahudhurio kwenye makaburi yao kuweka maua. Maua yatasaidia nini kwa mfu/wafu, kama si akili za usingizini za mtu ambaye hakusimama kwenye nafasi yake.

Leo mtu anacheza na kazi yake, anafanya vituko vingi kweli, kama ni daktari utamkuta hatimizi wajibu wake. Muda mwingine anawaangalia wagonjwa wanapoteza maisha yao kwa uzembe wake, ila akishaipoteza hiyo kazi iliyokuwa inamfanya alipwe na apate kiburi. Ndio anaona uthamani wa hiyo kazi, tena anaanza kuwa na huruma na wagonjwa wakati siku yupo kazini alikuwa anaongea na mgonjwa huku anachati wasap,intagram, facebook.

Leo hii tunaona ibada sio muhimu sana, wengine ikifika siku za kwenda kanisani, siku hiyo ndio wanaona ni ya kufua nguo zao walizovaa wiki nzima. Ila siku ikiwafika hata ule uhuru wa kwenda kusali unakuwa haupo tena, ndio wanaanza kuona uthamani wa kwenda kukusanyika pamoja.

Leo tunaona kusoma Neno la Mungu sio muhimu sana, tena tunaona ni kupoteza muda wetu, itafika siku utatamani ungesoma Neno la Mungu kwa bidii sana usingekuwa hivyo ulivyo. Muda huo utakuwa huna nafasi tena ya kubadili chochote na utakuwa huna nafasi tena ya kusoma Neno la Mungu. Ni pale utakapogundua maisha yako yote ulikuwa kwenye imani potofu ambayo ilikuwa haimtumikii Yesu wa kweli bali yesu mwingine.

Neno la Mungu linagusa kila eneo la maisha yako kiroho na kimwili, unaweza kukataa kwa sababu hujajua hili ninalolisema hapa. Unapaswa kuwa na muda wako wa kujisomea Neno la Mungu, kujua maandiko Matakatifu yanasemaje juu ya maisha yako.

Tabia ya kuja kujua uthamani wa kuishi, wakati huo ndio muda wako wa kukata roho, haitakuwa na maana yeyote. Wanadamu tuna siku chache sana hapa duniani, vyema ukajua vizuri nafasi yako mbele za Mungu aliyokuleta hapa duniani.

Kufa ukiwa hujalitumikia kusudi la Mungu ni hasara kubwa sana, kusubiri mtu afe ndio tunakumbuka uthamani wake sio sahihi kama akiwa hai hatukumjali. Kusubiri upoteze kitu chako ndio ujue thamani yake, itakuwa haiwezi kubadilisha ukweli wa jambo hilo.

Mpende sana Mungu wako, na upendo wako utakamilika kama utamjua vizuri unayempenda kupitia Neno lake. Zaidi ya hapo unaweza kuta unampenda kweli lakini upo eneo ambalo halimpendezi yeye Bwana, ila unakuwa hujui kama ni chukizo mbele za Mungu. Na Mungu akijaribu kusema na wewe kupitia watumishi wake unakuwa mgumu kuwaelewa kwa sababu shetani amefunga ufahamu wako.

Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, usiache kukifanyia kazi ulichojifunza. Weka bidii yako katika kusoma Neno la Mungu, usipende kushikiwa wokovu wako mikononi mwa watu, kuwa na utaratibu wa kusoma Maandiko Matakatifu ili uweze kusimama kwa miguu yako mwenyewe.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovukwa masomo mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.