Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana wetu ametupa kibali cha kuiona tena. Tuna kila sababu ya kumrudishia sifa na utukufu kwa nafasi hii aliyotupa, lipo kusudi la mimi na wewe kuwepo siku ya leo.

Kusoma Neno la Mungu ni muhimu sana kwa kila mwamini wa Kristo, mengi tunajiaminisha kuwa ni dhambi lakini sivyo tunavyofikiri. Uchanga wetu wa kiroho na wa kutojua Neno la Mungu umetufanya tubebe mafundisho fulani ambayo mtu alifikiri kwa akili zake mwenyewe.

Bila kujitambua tumekuta tunasambaza uongo na kuwatia wengine hofu kwa kitu ambacho sio sahihi, yote ni kwa sababu na sisi tunaosambaza jambo hilo hatujafanya uchunguzi wa kimaandiko yanasema nini juu ya hilo jambo.

Vipo vitu hatuwezi kufanya kutokana na sababu zetu binafsi, au vipo vitu hatupendi kufanya kwa sababu zetu binafsi. Ila sababu hizo sio kwamba zinaweza kumwathiri kila mtu, bali ni kwetu binafsi, na sio kwamba wengine wakifanya inakuwa dhambi kwao la hasha.

Sawa na mtu hawezi kula nyama kwa sababu ya madhara fulani anayopata kwenye mwili wake anapokula tu nyama, sasa ni hatari kuanza kusema ni dhambi watu kula nyama kwa sababu zako binafsi zilizokupelekea usile nyama.

Mara nyingi tumetumia nguvu nyingi kuwaaminisha watu vitu ambavyo havipo hata kimaandiko, muda mwingine hata sisi tunaowaaminisha wengine uongo tunafikiri tupo sahihi. Kumbe usahihi tunaofikiri sisi haupo hivyo kabisa, upo ndani ya biblia na tukiambiwa Neno la Mungu halisemi hivyo tunaanza kupinga na kukataa.

Mara nyingine tunaweza kulaumiwa na watu wengine wanaojua hatupo sahihi kwa kutojua kwao mizizi iliyochimbiwa kwetu, na wale tuliokuwa tunawaamini sana. Tunashindwa kujua Neno la Mungu haliangalii nani alisema hivi na vile, Neno la Mungu lenyewe lipo palepale linatutaka tufuate kama linavyotuelekeza.

Binafsi kuna vitu sipendi kuvifanya kutokana na sababu zangu binafsi ninazoona zinanipelekea wakati mwingine kukosa amani. Kutokupenda kwangu siwezi kuanza kuwatangazia wengine kuwa kufanya hivi ni dhambi ikiwa halina madhara kwao, ila naweza kuwashauri kama lina madhara kwao yanayowapelekea wamkosee Mungu wao bila wao kujua kuwa makosa wanayofanya yanatokana na chanzo fulani.

Mfano mimi nimeachana kabisa na habari za kushabikia mpira kutokana na sababu ambazo niliona mwenyewe kwangu zinaniletea shida na zingine zitakuwa na madhara zaidi mbeleni, kwa hali niliyokuwa naiona kwangu na kwa wengine kadri siku zilivyokuwa zinaenda. Mtu akiniuliza kwanini sio mpenzi wa mpira nitampa sababu zangu, akiona zina mashiko kwake ataweza kuacha na yeye. Ila siwezi kumlazimisha kuwa ni dhambi kwa matakwa yangu binafsi.

Vipo vitu kweli haijalishi unakubaliana navyo, wala haijalishi hukubaliani navyo, wala haijalishi uliaminishwa ni sahihi, wala haijalishi uliaminishwa sio sahihi. Ikiwa Neno la Mungu limesema usifanye vile fanya hivi, ujue utapaswa kufuata Neno la Mungu linavyosema na sio wengi wanavyosema/wanavyoamini/wanavyotaka. Hata kama mnaoamini hilo jambo lililo kinyume na Mungu mpo wengi kiasi gani kuzidi wanaoamini, na kutembea katika kweli ya Mungu.

Shida inakuja pale tunapoamini jambo fulani ni dhambi kumbe siyo dhambi, na shida inakuja pale tunapoamini kutenda jambo fulani sio dhambi kumbe ndio tunamkosea sana Mungu. Hata pale Mungu anapotuma mtumishi wake kuwaeleza mnachofanya sio sahihi, tunaanza kumrushia mawe kwa kuona anatupotosha.

Lakini tungekuwa na bidii ya kulisoma Neno la Mungu ingekuwa rahisi kujua mengi ambayo hatukujua kabla. Na tusingefuata wingi wa watu bali tungefuata kweli ya Mungu inavyosema tuenende. Pia tusingetupiana lawama kuwa fulani anakosea kumbe hawakosei, ila sisi kwa kutojua kwetu Neno la Mungu ndio tunaona anakosea.

Naomba usininukuu vibaya katika mafundisho yangu haya, kweli yapo mambo yanajulikana kwa wazi hata kwa yule asiye msomaji wa Neno. Kuwa anachofanya fulani sio sahihi wala hahitaji muujiza wa Mungu kukufunulia hilo, ninachosema mimi ni kufikiri kufanya jambo fulani ni dhambi kumbe sio dhambi ila ni vile huelewi Neno la Mungu linasemaje unaona dhambi.

Ushauri wangu kwako, amini sana Neno la Mungu kuliko hekima za wanadamu, soma sana Neno la Mungu kwa kadri unavyoweza. Soma yako iwe kuelewa Mungu anasema nini juu ya maisha yako kiroho na kimwili, na sio usome kwa ajili ya kwenda kushindana na walimwengu.

Isikumbue kuwa mbona wengi wanaamini jambo fulani ni sahihi na wakati sio sahihi, elewa Luthu na wanaye ndio waliopona katika janga la kuangamizwa Sodoma na Gomora, kwa sababu walisimama katika matendo mema ya Mungu. Elewa Daniel, shadrack, Meshack na Abednego hakuwangalia wingi wa watu waliokuwa wanasujudia mungu wasiyemjua wao. Walisimama na Mungu wao mpaka siku ya mwisho, na watu wakajua kweli wana Mungu wa kweli.

Amini Neno la Mungu usiamini mawazo yako binafsi, utamwona Mungu katika maisha yako ya wokovu kwa kiwango cha juu sana. Na yale uliyoamini ni dhambi na ukaanza kuaminisha wengine nabasi wakati sio dhambi, basi unapaswa kuyaacha kuyaamini maana zilikuwa ni nyakati za ujinga.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii, bila shaka umeondoka na kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya wokovu na katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.