Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, Mungu wetu ni mwema sana katika maisha yetu. Ameona vyema kutupa kibali cha kuiona tena leo, hatuna budi kumrudishia sifa na utukufu kwa nafasi hii adimu kabisa.
Tunajifunza Neno la Mungu kila siku, wengi wetu tumeanza kujua ahadi za Mungu juu ya maisha yetu, wengi tumeanza kujua makatazo mengi aliyotukataza Mungu. Lakini pamoja na kujua hayo bado wengi wengi wetu tupo kwenye vifungo fulani ambavyo sio halali yetu kuendelea kubaki navyo.
Huhitaji maombi ya kutisha sana ndipo utoke hapo Mungu alipokukataza, unapaswa kumwambia Mungu kupitia Neno lako hili nililosoma leo litendeke kwangu. Unamdai Mungu kitu alichokuahidi kwako kupitia Neno lake. Sio unasoma biblia kila siku inakataza wizi, alafu bado ile roho ya udokozi ipo ndani yako. Lazima umlilie Mungu kumweleza inakuwaje unakuwa na tabia ambayo yeye anaikataza na wewe umeshakuwa mtoto wake.
Hebu tuone Neno la Mungu linavyosema hapa;Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. GAL. 5:24 SUV.
Naomba nikuulize inakuwaje unasumbuliwa na tamaa ya uzinzi/uasherati ikiwa wewe ni mtoto wa Kristo na uliyelikiri jina lake kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako.
Inakuwaje leo umewaka tamaa za mwili, huwezi kutulia kanisani, huwezi kutulia kwenye ndoa yako, huwezi kutulia kwenye uchumba wako. Unarukaruka ovyo na wadada/wakaka/wababa/wamama.
Inakuwaje leo upo kanisani ni jambazi la kutisha, huonekani kama jambazi kwa mwenekano wa nje, kwa sababu umewapa vijana kazi na wewe ni mkuu wao. Upo kanisani unafanya vitu kwa kujitoa kweli watu wakifikiri njia yenu ni moja, kumbe sivyo wanavyofikiria.
Lazima ukae chini umwambie Mungu, inakuwaje umeokoka alafu bado unasumbuliwa na tabia za kale? Na kupitia Neno lake amesema hivi:=>>Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. GAL. 5:24 SUV.
Inakuwa mawazo yako yanawaza ujinga kila siku ikiwa wewe umeokoka kweli? Lazima kuna eneo hujaamua kujitoa kweli. Bado hujaamua kumdai Mungu haki zako, Neno la Mungu linasema hivi;Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. GAL. 5:24 SUV.
Ukishaona Neno la Mungu linasema jambo ambalo limekuwa kitanzi kwako unapaswa kumdai kwa ujasiri bila hofu yeyote, akuondolee hilo na akupe lililo jema. Tabia zote zinazoenda kinyume na Neno la Mungu, unapaswa kumwambia Mungu aziaziondoe bila kificho.
Haiwezekani Mungu kukataza jambo fulani alafu likawa gumu kwa mwamini aliyemkoa kwa thamani kubwa, ameshakuambia ukishakuwa wa Kristo, tamaa mbaya za mwili na mawazo mabaya yanasulubishwa/yanaondolewa.
Ikiwa hajasulumbishwa hayo yote unapaswa kufanya hili jambo;
Rejea; Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] MATHAYO 17:20-21 SUV.
Yapo mambo hayatoki kwa sababu hatuamini kama Mungu anaweza kufanya kweli, kuna mambo hayatoki mpaka kwa kufunga na kuomba. Ukiona una imani lakini unaomba jambo fulani likuachie lakini halikuachii, cha kufanya ni kuingia kwenye maombi ya kufunga kwa kumaanisha haswa huku ukiwa na imani mbele za Mungu.
Neno la Mungu likishasema limesema, linakuelewa kuliko hekima za wanadamu, linakuelewa kuliko hizo sayansi. Nakwambia ukweli kabisa, mwombe Mungu akaushe tamaa chafu, jitenge na marafiki wanaokuvuta/wanaokusababisha umtende Mungu dhambi.
Kuna uwezekano huwa unamtenda Mungu dhambi kwa kuwa na marafiki waliojaa mazungumzo mabaya, hapohapo Neno la Mungu linakuambia hivi:=>> Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.1 KOR. 15:33-34 SUV.
Huenda ungesema haya maneno nayaongea tu, haya Neno la Mungu linasema lenyewe kama unavyosoma hapo. Kama huamini chukua biblia yako uthibitishe mwenyewe huenda ukafikiri nimeyatoa kichwani mwangu tu.
Jifunze kumdai Mungu wako kupitia Neno lake, hakikisha unaishi kama Neno la Mungu linavyokutaka uishi. Usifuate mafundisho potofu ya kukufariji uendelee kutenda dhambi, utaumia ndugu yangu. Banana na Mungu wako mpaka kieleweke, mwambie ikiwa umesema hivi nab kukataza mbona mimi nafanya hivyo, na bado nasema wewe ni Baba yangu, na ninakukiri kama Bwana na Mwokozi wa maisha yangu. Iweje leo nakuwa na tabia chafu namna hii? KATAA.
Komaa na Mungu wako mpaka kimeeleweka, huhitaji kusaka manabii na mitume na maaskofu, huenda umefanya hivyo na umejishangaa tabia ni zilezile. Banana na Mungu wako chumbani kwako mpaka umetoka na majibu ya maswali yako, Neno la Mungu linakuonya na kukufundisha na kukuelekeza. Mwambie Mungu unapenda kuenenda sawa sawa na neno lake.
Bila shaka lipo jambo umejifunza kupitia ujumbe huu wa Leo, matumaini yangu unaenda kuwa mtu wa tofauti kabisa kuanzia leo. Maana unaenda kuchukua hatua ya kutengeneza na Mungu wako, hutokubali tena kuenenda kama watu wasiomjua Kristo aliye hai.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.