Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema atupe kibali cha kuiona tena leo. Siku zote huwa naona hizi ni fursa kubwa sana kwetu kwenda kufanya yale ambayo yanamzalizia Mungu matunda.

Uvivu ukishamkamata mtu, unaweza kumwendesha kiasi kwamba anaona anachofanya kwake ni sahihi na wala hakuna shida yeyote ile. Ndipo unamkuta mtu anajifariji kwa vitu vya kizembe anavyofanya, wakati alikuwa na uwezo wa kutofanya kizembe namna ile, angefanya vizuri kabisa.

Uzembe huu upo sana kwenye kusoma Maandiko Matakatifu, wengi tunapenda kusomewa biblia na wengine, wakati mwingine anayekusomea akipitiliza sana kukuambia fungua vitabu vingi unaona usumbufu, wakati mwingine akisoma mistari zaidi ya kumi unaona ni adhabu kwako.

Tumekuwa wasomewaji wa Neno la Mungu siku za ibada, hatuna muda wa kujisomea wenyewe kujua kilichoandikwa ndani. Hata ule muda wa kutulia wenyewe kupitia yale maandiko Matakatifu tuliyojifunza kwenye ibada, hatuna huo muda.

Wengi tukazana kuandika mistari mbalimbali tunayopitishwa siku za ibada na wakati mwingine tunaandika na yale muhimu anayosema mtumishi wa Mungu. Lakini hatuna muda wa kujipa wenyewe kupitia yale tuliyoandika na kujifunza.

Tunafikiri inatosha kabisa kufungua na kusomewa mistari michache ya biblia, tumejikuta hatuna uwezo wa kuweza kusimama kwa miguu yetu wenyewe. Hata ule umhimu wa kuwa na biblia hatuuoni, mtu ana biblia ya bei kubwa lakini ni ya kuendea kanisani, hana muda wa kuisoma yeye kama yeye.

Bila shaka tutaendelea kuwa wachanga kiroho kila siku, tunakuwa na miaka mingi kwenye wokovu lakini hiyo miaka haionyeshi matokeo yetu mazuri ya kukua kiroho. Mtu ana jivunia miaka mingi ya kuwa ndani ya wokovu lakini hana uwezo wa kujisimamia mwenyewe na Mungu wake.

Kujitoa kwenye eneo la kuendelea kuwa wachanga kiroho, tuachane na dhana ya kusomewa biblia, tuisome biblia wenyewe, tena tuisome kwa bidii zote. Huku tukimwomba Roho Mtakatifu atusaidie kuelewa kile Mungu anatutaka tukijue, hata kama mtu akitusomea tukubaliane naye anachokisema anakitoa ndani ya biblia.

Tusisubiri siku za ibada ndio tunaikumbuka biblia ilipo, wakati mwingine tunaona uvivu wa kuibeba badala yake tunaenda mikono mitupu. Wakati mchungaji anakwambia fungua kitabu fulani, utabaki unawatazama wenzako wanavyofungua ila wewe huna cha kufungua.

Ipo faida kubwa sana kusoma mwenyewe maandiko Matakatifu, nakwambia kuna faida ambayo sio rahisi kunielewa kwa sasa. Hasahasa wewe ambaye hujawahi kufanya hili zoezi, na kama umewahi basi uliishia njiani zaidi sana umebakiza kusimlia watu ulikuwa unasoma sana biblia siku za nyuma.

Unaweza kuanza sasa kusoma Neno la Mungu, huna biblia ya kawaida, anza na ya kwenye smartphone yako wakati unaendelea kutafuta pesa ya kununua nyingine. Unayo na uliifanya kama urembo wa kuendea kanisani, anza sasa kuisoma na kujua kilichoandikwa ndani, sio unasumliwa na watu.

Utasema kusomewa biblia kuna tatizo gani, mbona sms zako zinazoingia kwenye simu yako huwa huombi mtu akusomee. Ina maana sms zako ni za muhimu sana kuliko Neno la Mungu, ina maana sms zako ni jambo la siri sana kuliko Mungu. Wengine mpaka wanaingia na simu pafuni wanaoga nazo, inakuwaje ungekuwa mkali wa kujionya usiwe mtu wa kupuuzia hili la kusoma Neno la Mungu mwenyewe.

Ukiamua kutoka ndani ya moyo wako unaweza, tena unaweza na utakuwa mfano wa kuigwa na wakristo wengine ambao wapo kwenye kifungo kama chako cha kusubiri wasomewe biblia. Hiyo sio taarifa ya habari ambayo anayesoma anapaswa kuwa mtu mmoja mnayemsubiria saa mbili usiku, hata huyo naye kuna mtu ameipitia kwanza taarifa yake ndio akaisoma. Tena wengine hawana mpango wa kuangalia taarifa ya habari kwa sababu matukio yote anajua anayapata kwenye simu yake, na wakati mwingine amefanya marudio maana kila kitu alishakiona na kukisikia.

Kwanini na wewe usione mambo yote kuhusu Neno la Mungu unaweza kuyapata ndani ya simu yako ya kiganjani, ni rahisi kwako kufanya smartphone yako kuwa darasa lako la kujifunza mambo mbalimbali ndani ya biblia.

Mpaka hapo naamini kuna mwanga umeupata wa kuweza kusimama katika nafasi yako ya kusoma Maandiko Matakatifu. Ukishakuwa msomaji wa Neno la Mungu, utakuwa umefaulu kwa kiwango kikubwa sana.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovukwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.