Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona tena. Kwa ujasiri mkubwa kabisa, nasema sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana wetu kutupa kibali kingine tena cha kuweza kufanikisha yale tuliyopanga kuyafanya siku ya leo. Tunaamini wengi walipanga kufanya makubwa siku ya leo, hawakuweza kuifikia siku hii tuliyoifikia mimi na wewe.
Kuna vitu vya msingi kabisa hatupaswi kuleta utani wala kuvipuuza, nikiwa na maana kuna vitu unaweza kuingiza utani na kuvipuuza. Ila haviwezi kuwa vyote unaweza kufanya hivyo.
Nashangaa sana mtu anasema Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yake, anaanza kurahisisha vitu ambavyo hata Mungu mwenyewe amevikataza visindeke. Ila yupo mtu anasema Mungu wetu ni mmoja na wote tunamwabudu yuleyule.
Kwani Mungu halijui hilo? Kama analijua kwanini ameweka utaratibu wa kuweza kuingia mbinguni Kwenye maisha ya umilele baada ya haya. Kwanini hakusema hata wale wanaoabudu miungu mingine watauona uzima wa milele bila kuyaacha wanayoyafanya, kwanini hakuweka uhuru wa kuokoka au kutookoka lakini siku ya ufufuo wote wataingia uzima wa milele.
Mtu anamkataa Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wake, badala yake anaamini miungu yake. Alafu unasimama na kumtetea mtu kama yule na wakati mwingine unamfariji kuwa Mungu wetu ni mmoja asiwe na shaka, aendelee kuifuata imani yake.
Wote ni watu wa Mungu ila wamekataa kufanyika watoto wa Mungu, maana wote walioliamini jina la Yesu Kristo wamefanyika watoto wa Mungu.
Rejea; Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. YOHANA 1:11-13 SUV.
Wapo watu mpaka leo wanamwamini Mungu anaweza kuwasaidia ila hawataki kusikia habari za Yesu Kristo. Alafu mtu kama huyu unamfariji Mungu wetu ni mmoja, na wakati mwingine unamwambia niombee.
Naomba nikupitishe kwa huyu ndugu ambaye nilipata fursa ya kujibizana naye, kwa hapa nitampa jina la YEYE na mimi mwandishi nitajipa jina la MIMI. Lengo ni ili uone kiasi gani huwa tunapenda kurahisisha sana wokovu uliopatikana kwa gharama kubwa.
Naomba unielewe, haya mazungumzo yalitokana na mimi kutoa maandiko matakatifu kutoka ndani ya biblia.
YEYE; UMEANGALIA NA VITABU VINGINE?…WACHINA NA VITABU VYAO, QUARAN?…VITABU VYA BUDHA?
MIMI; Siangalii vitabu vingine vinasemaje, naangalia maandiko matakatifu yanasemaje…ndio mwongozo wa maisha yangu ya wokovu.
YEYE; Maandiko matakatifu yepi?…BUDHA SIO MATAKATIFU”…QUARAN?
MIMI; Hayo unajua wewe, ninachojua mimi ni Biblia iliyobeba Neno la Mungu.
YEYE; PANUA AKILI PIA…KUNA DINI NYINGI SANA DUNIANI…TENA WENGI HAWAIJUI NA HIYO BIBLIA YAKO.
MIMI; Hizo dini zafaa nini? Ikiwa wanamkataa Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wao?
YEYE; nao wanajua KUWA Humtaki MUNGU WAO NA MWOKOZI WAO. KUNA MTUME…BUDHA WANA MIUNGU ZAIDI YA 700…KAMA HUFUATI YAO,,,,NAWE MOTONI.
MIMI; Wewe unaamini nini kati ya hayo.
YEYE; 169,000 YA WAISRAEL NDO WAKRISTU…wote hawamjui, na wasiomjua Mungu idadi yao ni 8,323,248.
MIMI; Wewe ni muisrael? Nimekuuliza wewe imani yako ni ipi? Kwani aliyekuambia Mungu anayaangalia wingi wa watu wanaomwamini ni nani?
Hakunijibu tena hayo maswali niliyomuuliza, umepata picha jinsi watu tunavyojifariji kwa mambo ambayo hata Mungu mwenyewe anatushangaa. Mungu ametupa uhuru wa kuamua, tumfuate yeye au yale tunayoona wenyewe yanatufaa.
Ukiamua kumfanya mungu wako ni ng’ombe unaweza kufanya hivyo, ila Mungu wangu ninayemwamini mimi na ndiye mwenye mbingu anakataza hilo.
Hebu tupitie Maandiko Matakatifu kwa uchache tuone Mungu anasemaje;
Rejea;
Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. Kutoka 20:23 SUV.
Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo. Waamuzi 2:17 SUV.
Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao. Yeremia 11:10 SUV.
Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza. Yeremia 35:15 SUV.
Fuata Maandiko Matakatifu usiafute wingi wa watu, kuona wengine wanaoabudu miungu mingine wapo sawa. Unakuwa unakosea sana, hatuwezi kuwa sawa kama madai ya yule ndugu niliyekuwa naye kwenye mazungumzo.
Narudia tena fuata neno la Mungu kama linavyosema na si kama watu wanavyosema, na wewe uliyepata Neema hii ya wokovu. Hebu fuata biblia inavyokutaka unende kama mtu aliyezaliwa mara ya pili.
Rejea;
Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.Yohana 3:3 SUV.
Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;1 Petro 1:3 SUV.
Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele. 1 Petro 1:23 SUV.
Bila shaka kuna kitu umekipata cha kukufanya ujue namna ya kusimama Mungu wa kweli.
Nikutakie wakati mwema, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.