Haleluya, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena ya baraka kwetu Mungu ametupa kibali cha kuiona tena leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, unapaswa kumwambia Mungu akupe ufahamu wa kuweza kuenenda katika kusudi lako.
Karibu sana kwenye kurasa zetu za SOMA NENO UKUE KIROHOambazo zinakujia kila siku isipokuwa siku za jpili. Tunaendelea kuhimizana na kukumbushana yale muhimu, na kushirikishana changamoto mbalimbali namna ya kuepukana nazo ili tuwe na kiu/hamasa ya kusoma Neno la Mungu bila kuchoka.
Faida za kukua kiroho zipo nyingi sana na zimegawanyika katika maeneo mengi ya maisha yako ya wokovu, kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kumjua Mungu wako kupitia Neno lake. Kukomaa kwako kiroho inategemea sana bidii yako binafsi ya kumtafuta Mungu kwa bidii na kulisoma Neno lake.
Usishangae miaka yako yote ya wokovu ukajikuta bado ni mchanga kabisa wa kiroho, hii inatokana na wewe kutojishughulisha na yale muhimu yanayoweza kukuvusha na kukuondoa kwenye eneo la uchanga wa kiroho.
Unapokuwa mchanga wa kiroho hata uzalishaji wako wa matunda mbele za Mungu unakuwa haupo vizuri, badala yake unakuwa kwa kiwango cha chini sana. Ambao haupo kiviwango vinavyostahili. Hili huhitaji kuambiwa na mchungaji wako bali wewe mwenyewe unakuwa unaona moyoni mwako.
Pamoja na zipo faida nyingi za mtu kukua kiroho, zipo pia hasara za kuwa mchanga kiroho. Hasara hizi ni mbaya sana kwa mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, na mkristo mwenye kazi ya kulitimiza kusudi lake kabla ya kuondoka hapa duniani.
Wengi sana wamekuwa na chuki na hasira mioyoni mwao pale wanaposikia Neno la Mungu, mtu mchanga na aliyefungwa ufahamu wake. Pale anaposikia kweli ya Mungu anaona kama vile anasemwa yeye na si Neno la Mungu, yaani sio kwamba hilo Neno la Mungu analosema amelitunga anayelisema la hasha.
Najua umewahi kuona hali hii kwa wewe ambaye ulikuwa bado hujaamua kuokoka kweli yaani ulikuwa unaonekana kwa nje umeokoka ila matendo yako yalikuwa machafu. Umewahi kujikuta ukichukia watumishi wa Mungu pale wanapokuonya kupitia Neno la Mungu, uliwaona kama vile wakuzibia njia.
Chuki na hasira ndani ya moyo wako ni mbinu ya shetani kukufanya uendelee kubaki kwenye tatizo lako. Ni kuendelea kukutengeneza mazingira ya kujiona unachofanya kipo sahihi ila wanaokuambia uachane na hicho kitu hawajui kitu chochote.
Haijalishi watatumia Neno la Mungu, utaona wanakunyang’ana Uhuru wako. Badala kusikia kuumia na kuanza kutafuta msaada wa kutoka ndani ya shida yako, utaanza kutengeneza mazingira ya kuendelea kubaki kwenye shida yako.
Hizi chuki na hasira zimewaangukia sana watumishi wa Mungu wanaosimama kuihubiri kweli ya Mungu. Uchanga wa kiroho una tabu nyingi sana, uchanga wa kiroho utataka uwe unatamkiwa maneno ya baraka tu, uchanga wa kiroho utataka uwe unatabiriwa maisha yako, uchanga wa kiroho unapenda kusikia maneno matamu matamu tu.
Ukiguswa kwenye eneo ya kukuonya usiliendelee kutenda dhambi fulani, ghafla chuki na hasira zinaingia ndani mwako. Hiyo ni nafasi anayotumia shetani kupitia udhaifu wako wa uchanga wa kiroho, huwezi kuelewa haraka kama unakosea mpaka pale unakapotoka kwenye eneo hilo.
Hebu jichunguze na kujipa maksi mwenyewe, unaposikia maonyo ya Neno la Mungu huwa unajisikiaje ndani yako, unasikia kuumia na kutubu au unasikia hasira na chuki juu ya yule anayesema kweli ya Mungu kupitia Neno la Mungu. Ukijiona ndani yako unasikia huzuni kisha inazalisha chuki na hasira isiyotaka kuacha na kutubu, ujue una tatizo la uchanga wa kiroho.
Aliyekubali kumfuata Yesu Kristo, hata ukimwambia kufanya jambo fulani ni dhambi ataacha mara moja ilimradi biblia imeandika hilo unalomwambia. Akiona ni ngumu kuacha/kutoka atahakikisha anajua njia sahihi ili imsaidie kumtoa hapo alipo, na sio kujenga chuki na hasira za kuendelea kumwacha kwenye hali yake ya kumchukiza Mungu.
Lakini yule ambaye anasema Yesu ni Bwana na mwokozi wa maisha yake alafu kwenye matendo yake anamkataa, ujue huyo ana tatizo hili nililokuwa nakwambia hapa. Cha msingi hapa ninachoweza kukuambia ni kupambana kuhakikisha unatii Neno la Mungu, hakikisha moyo wako unakuwa na mawasiliano mazuri pale usomapo Neno la Mungu.
Ukijiona unasoma Neno la Mungu alafu husikii mguso wowote moyoni mwako wala hushtuki chochote, ujue una shida ambayo unapaswa kumlilia Mungu aiondoe. Hupaswi kubaki ngangari na sugu pale unasokisia Neno la Mungu linakuonya/kukurekebisha, unapaswa kusikia machozi moyoni mwako pale unapogundua ulikuwa unaenda kinyume na Neno la Mungu.
Chuki na hasira unayopaswa kuwa nayo ni pale unapoona mtu anataka kukurudisha dhambini, hii chuki itakuepusha na maovu mengi sana. Hufanyi hivi kumfurahisha mzazi, mlezi wala hufanyi hivi kumfurahisha mchungaji/askofu/padri wako. Unafanya hivyo kwa faida yako mwenyewe na Mungu wako.
Hakikisha Neno la Mungu linakuingia kisawasawa kama unavyokunywa maji yanaingia moja kwa moja, hakikisha wakati mwingine unalisikia Neno la Mungu linakuingia kama unavyochomwa sindano ya mkono/kidole. Hutokimbia kuchomwa sindano kwa sababu unahitaji kuchukuliwa vipimo vya kuweza kutambua ugonjwa unaokusumbua, na hutomchukia dokta kwa sababu ya kukuchoma sindano.
Neno la Mungu linaweza kugeuka sindano, usilichukie kwa sababu linakuponya eneo baya ulilokuwepo. Litakurudisha kwenye eneo ambalo Mungu anakutaka uwepo, baada ya maumivu makali unaokoa uhai wako wa kiroho.
Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, hakikisha unafanyia kazi kile umejifunza. Usibaki kusema kweli na kutikisa kichwa alafu ukaendelea kuona chuki na hasira ndani yako, huenda hata huu ujumbe umeleta chuki na hasira ndani yako, unachopaswa kuelewa ni Mungu anakutaka ubadilike.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.