Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona tena. Tunapaswa kuitumia vyema siku ya leo kwa ajili ya kumzalia Bwana matunda yaliyo mema.

Karibu sana tushirikishane baadhi ya mambo yanayoweza kukusadia katika maisha yako ya wokovu. Yapo mambo huenda ulikuwa huyajui, kupitia ujumbe huu unaenda kuyajua. Na kama ulikuwa unayajua basi unaenda kujikumbusha kwa njia ya kujifunza zaidi.

Tunakutana na elimu nyingi sana zikitufundisha mambo mbalimbali katika maisha yetu, yapo mambo mazuri tunayapata na yanatufaa katika maisha yetu ya mwili. Kutufaa katika maisha yetu ya mwili, sio kigezo cha moja kwa moja yakatufaa katika maisha yetu ya wokovu(kiroho).

Wakati mwingine tumepotoshwa kwa kusomewa Neno la Mungu, na kufundishwa kwa mapokeo ya wanadamu. Ambayo mafundisho hayo ni ya watu wasiomjua Kristo kama Bwana na Mwokozi wao. Nasi kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni, tumeyabeba kwa kuamini ndio kweli ya Mungu.

Rejea; Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Wakolosai 2:8 SUV.

Yapo mafundisho ambayo si ya jinsi ya Kristo, japo yamekaa kama ni mafundisho ya Yesu Kristo. Ni namna shetani anatumia mwanya wa kuendelea kuwadanganya kanisa kwa mafundisho ya mapokeo ya wanadamu.

Wengine kwa kutaka kuendelea kufuata nia zao, kwa kutotaka kubadilika kama watu waliozaliwa mara ya pili. Wanajitafutia walimu wa uongo na kuikataa kweli ya Mungu, wengine kwa kujua. Na wengine kwa kuchotwa tu elimu hizi za uongo kutokana na uchanga wao kiroho, na wangine ni kwa sababu wana masikio ya utafiti.

Rejea; Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti. 2 Timotheo 4:3 SUV.

Mtu anaona kuliko kuacha kutenda dhambi aliyoambiwa ni chukizo kwa Mungu, anatafuta walimu watakaomwambia hilo ni sahihi endelea kufanya. Lakini akirudi katika Neno la Mungu limkataza kabisa na unaweza kumwambia nionyeshe andiko linaonyesha uhalali wa kutenda hivyo. Atakufikirisha kwa mafundisho ya mapokeo ya wanadamu yaliyo kinyume na maandiko matakatifu.

Ukweli tulipaswa kufundishwa mafundisho sahihi ya Neno la Mungu, badala yake tumeyakataa na kutaka mafundisho laini laini. Na kuona wanaofundisha kweli, wanafundisha mafundisho magumu yanayotuzuia tusiendelee na maovu yetu.

Rejea; Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. Waebrania 5:12 SUV.

Tunapaswa kupata mafundisho yanayotufaa na yanayotujenga imani yetu, sio mafundisho yanayotutakia tu mafanikio na baraka. Huku yakituacha tukienenda katika dhambi zetu, huku yakituacha tukiwa hatuna uwezo wa kuondokana na maovu yetu.

Kwa kuwa tunapenda kusikia mafundisho fulani ya kutufariji tuendelee kubaki katika dhambi, shetani ametumia nafasi hiyo kuendelea kutupotosha tunayofanya ni sahihi. Kumbe tulipaswa kupokea mafundisho ya neema ya Kristo.

Rejea; Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. Waebrania 13:9 SUV.

Leo watu hawataki kusikia maonyo ya Neno la Mungu kwa kuona hata kushiriki ibada za sanamu na miungu yao inafaa. Wameona mafundisho ya mapokeo ya wanadamu yanafaa zaidi kuliko Neno la Mungu. Wengine wameenda mbali zaidi kwa kuhalalisha kuzini.

Rejea; Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.Ufunuo 2:14 SUV.

Napenda ujue kuwa hiyo ni mbinu ya shetani kukufanya uendelee kuwa kondoo wake, jambo lolote linalokatazwa katika fundisho la Kristo, uwe na uhakika ukilitenda ni dhambi. Haitajalisha aliyekuambia hilo unalolitenda ni sahihi, ni mtu mnayeheshimiana naye sana au ni mtu wa dini sana au ni mtu aliye na msimamo ya dini sana. Kama amekupotosha lazima uwe tayari kukataa kufuata kuamini kwake na kufuata vile Neno la Mungu linakuelekeza.

Rejea; Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine. Ufunuo 2:24 SUV.

Siamini kama hupendi mbingu, siamini kama unashikilia hilo jambo lililochukizo kwa Mungu, kwa vile hutaki kumwangusha mzazi/mume/mchungaji wako. Ikiwa ni kinyume na maandiko matakatifu, uwe mtu wa kukubali kufuata kweli ya Neno la Mungu.

Soma Neno la Mungu likutoe hapo ulipoaminishwa ni kweli wakati sio kweli, Neno la Mungu likipingana na unachoamini na kukifanya. Haraka sana unapaswa kuacha na sio kuanza kutafuta mafundisho mengine ya kukufariji uendelee kuamini upotofu huo.

Umechagua kuijua kweli ya Mungu, kubali kubadilika kama Neno la Mungu linavyokutaka uenende, usiangalie watu wanasemaje. Angalia Neno la Mungu linasema nini, wakati mwingine hao unaoamini watakushauri vizuri. Ndio hao hao wamelishwa mafundisho potofu.

Hakikisha unalielewa vizuri Neno la Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu, mwombe Mungu aweze kufungua moyo wako ili Neno lake liweze kukubadilisha. Na si wewe kutamani kulibadilisha Neno la Mungu, ukishaona unatamani Neno la Mungu likufuate wewe ujue una shida ndani yako.

Mpaka hapo nina imani utakuwa umepata Mwanga wa kukusaidia kuona mafundisho ya kweli ya Mungu ni muhimu sana kwa mwamini wa Kristo. Usikubali kuenenda kwa mafundisho potofu, kubali kuenenda katika njia sahihi ya Kristo.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kutembelea ukurasa wetu kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukuhimiza kuifuata kweli ya Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.