Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa na njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye, kwa sisi tuliopata kibali cha kuiona siku hii, wengi waliitamani leo ila hawakuweza kuifikia, wengi tulitamani ndugu zetu wawepo leo lakini haikuwezekana.

Leo tuzungumzie hili jambo muhimu sana; “Unalichukuliaje Neno La Mungu Unavyolisoma Na Kabla Hujalisoma”vizuri ukajihoji hili jambo ili kujijua ukoje ndani yako. Huenda tunahimizana kusoma Neno la Mungu na kuliheshimu Neno la Mungu, lakini ndani yako huelewi kabisa kwanini uliheshimu Neno la Mungu na kwanini usome Neno la Mungu kila siku.

Huenda katika usomaji wako wa Neno la Mungu, umekuwa wa mazoea na ukawaida, yaani usome na usisome Neno la Mungu vyote unavyoona kwako ni sawa tu. Unapoambiwa Neno la Mungu linaweza kumbadilisha mtu tabia yake mbaya na kuwa katika mstari mzuri wa Mungu, kwako unaona ni kitu ambacho hakiwezekani.

Sio kana kwamba hujaokoka, sio kana kwamba huendi kanisani, vyote unafanya ila ndani yako hakuna uzito wowote kuhusu Neno la Mungu. Hata ukikutana na mtu anadhihaki Neno la Mungu huwezi kujisikia vibaya ndani yako, unaona kawaida kabisa kama ilivyo kwa vitu vingine vya kawaida.

Unaweza kuwa hata unaposikia mtumishi wa Mungu anayapitia maandiko Matakatifu mbalimbali, ndani yako unasikia vibaya na wakati mwingine huoni uzito wowote juu ya Neno lile analolifundisha.

Swali la msingi kwako;Unalichukuliaje Neno La Mungu Unavyolisoma Na Kabla Hujalisoma. Kuna kitu gani unajisikia ndani mwako usikiapo Neno la Mungu likitamkwa, ukielewa hili jambo hutokaa uhimizwe kusoma Neno la Mungu, hutokaa uambiwa litii Neno la Mungu. Nasema haitakuwepo siku zako zote.

Badala ya watu kuanza kukupigia kelele za SOMA NENO, utakuwa na ratiba yako maalum ya kujisomea maandiko matakatifu. Lakini kabla hujaelewa nini maana ya wewe kuwa na tabia ya kusoma Neno la Mungu, utaendelea kubaki kama ulivyo.

Kwa kukusaidia katika hili, anza kuliona Neno la Mungu kama mwongozo sahihi wa maisha yako ya wokovu. Kwenye ufahamu wako ona pasipo Neno la Mungu maisha yako ya kiroho na kimwili hayawezi kuwa salama.

Huhitaji nguvu kubwa sana kuliweka moyoni mwako jambo hili, sikia kiu ndani yako usipopata muda wa kusoma Neno la Mungu. Kuelewa kama hili jambo limekuingia vizuri ndani yako, jisikilizie ndani yako pale unaposikia Neno la Mungu linahubiriwa/linafundisha moyoni mwako unajisikiaje. Kama hujisikii msisimko wowote au kama husikii msukumo/uzito wowote, ujue umekufa kiroho unahitaji msaada wa kukufuliwa upya.

Kufufuliwa kwako ni kumpokea Roho Mtakatifu kuwa ndani yako, vinginevyo utabaki kuona hadithi na kitu kisichowezekana kusoma Neno la Mungu kila siku. Lakini Roho Mtakatifu akiwa ndani yako utasikia kiu ya kusoma Neno la Mungu, wakati huo umeshajua umhimu wa Neno la Mungu. Na huwezi kusikia kiu ya jambo usilolijua umhimu wake kwako.

Pasipo Neno la Mungu hatuwezi kumpendeza Mungu, pasipo Neno la Mungu tutaona kutenda dhambi ni jambo la kawaida, pasipo Neno la Mungu hatuwezi kujua uthamani/umhimu wa kuokoka kwetu. Kinachotufanya tumweshimu Mungu wetu ni Neno la Mungu, kinachotufanya tufunguke zaidi kiakili ni Neno la Mungu.

Mkristo safi aliyejitambua, fahamu kwamba Neno la Mungu limempika ndio akawa hivyo. Haikutokea tu ghafla akawa hivyo, na kadri siku zinavyozidi kwenda mbele anazidi kuimarishwa zaidi kiroho kuliko jana iliyopita.

Kuokoka tu haitoshi, unapaswa kuendelea kujifunza zaidi Neno la Mungu ili ujue uliyemwamini Utofauti wake upo vipi na uliyekuwa unazitenda kazi zake mbaya. Usipolifahamu hilo utakuwa mkristo anayeenda kwa waganga wa kienyeji, utakuwa mkristo lakini mzinzi/mwasherati, utakuwa mkristo lakini mlevi kama asiyeokoka, utakuwa mkristo lakini muongo, mwizi, mseng’enyeji/mchonganishi.

Umhimu wa kusoma Neno la Mungu ni jambo la msingi sana ambalo siwezi kukufariji kuwa usome usisome yote sawa. Huko nitakuwa nakufariji uendelee kubaki kwenye ujinga ambao utakugharimu baadaye. Jiwekee utaratibu wa kusoma Neno la Mungu, utaanza kusema labda mpaka uende chuo cha biblia ndio utaelewa. Unaye Roho Mtakatifu ndani yako mtumie kukusaidia kuelewa kile unasoma, bora uwe na maswali kwa kitu ulichokisoma kuliko kuwa na maswali kwa kitu usichokisoma.

Chukulia hili jambo kwa uzito mkubwa utaona mabadiliko ya huduma yako, utaona mabadiliko ya ukristo wako, utaona kiwango chako cha maombi kinakua cha tofauti, utaona kiwango chako cha uchukuliaji mambo magumu unabadilika kabisa na utaona kiwango chako cha imani kikua. Hii yote ni pale utakapojua umhimu wa Neno la Mungu.

Bila shaka kuna kitu umekipata kupitia ujumbe huu, kile kimeugusa moyo wako kichukulie kwa uzito ili uweze kusimama katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Kama ulikuwa hujaanza kusoma Neno la Mungu anza sasa, na kama ulikuwa unasoma lakini huelewi unachofanya sasa utakuwa umejigundua tabia yako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi ya kukusaidia kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.