Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, pasipo yeye hapana awezaye haya yote.

Kile tunatamani wengine wawe nacho, tunapaswa sisi tunaotamani tabia fulani iwe kwa mtu,tuwe wa kwanza kuwa nayo hiyo tabia. Unatamani mwanao awe mcha Mungu, anza wewe kumpenda Mungu katika Roho na kweli. Ili kupitia wewe mwanao ajifunze mambo mbalimbali ya kumsaidia katika maisha yake.

Kijana unatamani kumpata mume/mke mcha Mungu, anza wewe kwanza kuwa mcha Mungu usiye na michanganyo michafu ya dunia. Utaona kile kipo ndani yako Mungu atakuletea kile kile cha kufanana na tabia yako. Kwanza hutokuwa na wasiwasi kukitambua maana tayari uhusiano wako na Mungu na kile unachokitamani kiwe chako, kitakuwa na uhusiano na Mungu aliye ndani yako.

Wakati mwingine wazazi tunashindwa kueleweka kwa watoto kwa sababu tabia zetu hazifanani na kile tunawasisitiza watoto wetu wawe. Unamkataza mtoto jambo fulani baya alafu anakuona baba/mama unalifanya, kama ni mavazi ya aibu anaanza kukuona wewe mama unavaa, kama ni kuhusu uaminifu kwenye ndoa yako anaanza kukuona wewe mzazi sio mwaminifu.

Watoto wananasa vitu ambavyo huwezi amini kama wanaweza kuhifadhi vitu vikubwa kiasi kile, hii ni kwa sababu ndani mwao bado hakuna vitu vingi. Kila watakachokisia wao wanakihifadhi, kila watakachokiona wao wana kiweka kichwani.

Tunawasisitiza watoto wetu wawe watu wa ibada, ila sisi wazazi hatufanyi hivyo. Mtoto anaona baba/mama kila siku ananiambia niende kanisani alafu yeye mwenyewe haendi, unaweza kufikiri unamtengenezea yeye kiu ya kumpenda Mungu. Kumbe wakati mwingine anakutazama wewe unafanya kile unamwambia, akiona hufanyi na yeye anaacha.

Asilimia kubwa ya tabia zetu, zina mchango mkubwa sana kubadilisha wengine kwa kuiga tunachofanya sisi. Ukiwa dada/kaka katika familia yako alafu ukawa na tabia njema au mbaya, una uwezo wa kuharibu wadogo zako kadhaa na una uwezo wa kuwajenga wadogo zako kwa tabia yako njema.

Tabia zetu nzuri au mbaya zina mchango mkubwa sana kubadilisha wengine, usifikiri maovu unayofanya unafanya tu peke yako. Wapo watu wanakuamini na bado hawajitambui, kupitia wewe wanaona kufanya kama wewe inafaa zaidi kumbe wanapotea. Vile vile ukiwa na tabia njema kuna watu wataiga tabia yako, utakuwa mkristo wa mfano kwa watu wengine.

Tukija kwenye kusoma Neno la Mungu ndivyo ilivyo, vile wewe unapenda kusoma Neno la Mungu na umejiwekea nidhamu ambayo imekuwa kama tabia yako ya kuzaliwa nayo. Una uwezo mkubwa wa kuwavuta wengi sana na wakawa na tabia ya usomaji wa Neno la Mungu.

Huenda hapo ulipo kuna mtu alikuvutia jinsi alivyo kuwa anasoma Neno la Mungu, mpaka leo wewe naye unasoma biblia. Huenda hapo ulipo kuna mtu ulimsikia akikupa faida za kusoma Neno la Mungu na ulizitazama kupitia yeye anayekuambia, ulivyoona ni kweli anachokisema mpaka leo unasoma Neno la Mungu.

Unapenda mtoto wako awe na tabia ya kusoma Neno la Mungu, anza wewe kusoma kila siku huku na yeye akikuangalia. Unapenda mke/mume wako awe na tabia hii ya kusoma Neno la Mungu, anza wewe kusoma Neno la Mungu na aone mabadiliko unayoyapata kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu.

Kile unatamani wengine wawe nacho, kama unaweza kukifanya wewe kuwa mstari wa mbele kwa vitendo. Hasa hili la kusoma Neno la Mungu, huhitaji uwe sijui nani, kama macho yako yanaona na ni mazima. Hakuna kisingizio chochote, maana ingekuwa shule ungesema umri umeenda huwezi tena kurudi shule badala yake ukawa unamsisitiza mwanao awe na bidii. Hilo linajulikana na wala mtoto hatakuwa na shida na hilo.

Je hili la kusoma Neno la Mungu utakuwa na kisingizio gani, bila shaka hakuna kisingizio. Unapaswa kuwa mfano mzuri kwa wengine, nakueleza kitu ambacho utajivunia mpaka unaondoka duniani na utaacha alama kwa kizazi chako na jamii yako.

Ukiwa kama kiongozi unapaswa kuwa mstari wa mbele kwa kile unachowahimiza watu wafanye, walio nyuma yako watakuwa na nguvu zaidi kufanya kile mmekubaliana. Kuliko wewe unawahimiza watu jambo alafu wewe hujitokezi kwenye hilo jambo, ni mbaya sana.

Soma Neno la Mungu kila siku, kupitia wewe utakuwa na uwezo wa kumshawishi na mwingine. Na hakikisha Neno la Mungu linakubadilisha wewe kwanza na wengine waone tofauti yako na yao, waone kabla hujawa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu ulikuwaje na sasa ulivyoanza kusoma Neno la Mungu umekuwaje.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, usiache kulifanyia kazi hili ulilojifunza. Utakuwa msaada kwa wengine kupitia wewe, kikubwa usiwe mchoyo kuwaeleza watu wanapohitaji msaada wa kujua ulifanikiwaje ukaweza kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu.

Tukatane kwa wakati mwingine tena, usiache kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.