Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuiona. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote.

Zipo changamoto ndogo ndogo ambazo zinaweza kuonekana ni kubwa sana kwa watu wengine, hizo hizo changamoto zinaweza kuonekana tofauti kwa mwingine. Nikiwa na maana kwa mwingine inaweza isiwe jambo kubwa sana linaloweza kumnyima usingizi na wakati mwingine kushindwa kula chakula.

Ukishaona vitu vidogo vidogo vinakunyima usingizi mpaka unafika wakati unaweweseka usiku, muda mwingine umeshindwa hadi kula chakula. Usione hiyo ni hali ya kawaida ambayo inamkuta kila mtu, ni kweli hakuna mwenye moyo wa chuma anayeweza kujisikia vizuri kwenye jambo lolote lile linaloumiza moyo wake. Ila utofauti unakuja kwenye uchukuliaji/ubebaji wa mambo moyoni, hapo ndipo wengi hujitofautisha.

Zipo tabia za kitoto ambazo ukiwa kama mtu mzima hupaswi kuwa nazo, maana usipokuwa nazo makini hizo tabia utajikuta umejaza vitu vingi sana moyoni mwako visivyofaa mbele za Mungu. Wakati mwingine unaweza kujihesabia haki kutokana na kosa ulilotendewa, ukaona kusamehe kwako haiwezekani kabisa.

Kuna siku nikiwa kwenye mizunguko yangu ya kazi, nilikutana na mama mmoja anajiapiza kwa mwenzake kuwa hataweza kumsamehe(akamtaja jina lake) mpaka anaingia kaburini. Hizi ni tabia za mtu aliyeshika dini moyoni pasipo Yesu Kristo moyoni, na vile vile hizi ni tabia za mkristo aliye mchanga kiroho.

Umekutana na mtu barabarani akakutukana wakati wote mnaendesha gari labda wewe ulimchomkea vibaya au yeye mwenyewe ndio alikuchomekea gari vibaya. Badala ya kukuomba radhi anakutukana, kwa uchanga wako hilo jambo linaweza kukutesa moyoni mwako siku nzima. Hilo tukio linaweza kukufanya usile chakula kisa ulitukanwa na mtu ambaye yeye ndio mwenye kosa, na wala humfahamu.

Tabia za kitoto/uchanga wa mtu zina mambo mengi sana ya kipuuzi, ambazo kila mtu anapaswa kuzikataa kwa kujaza maarifa yaliyomo ndani ya biblia. Kusoma Neno la Mungu kunakuondoa kwenye uchanga wa kiroho, ukiona wewe ni mtu wa kunyimwa usingizi na vitu vidogo vidogo ujue bado Neno la Mungu halijaanza kukubadilisha kwa kufanya kazi ndani yako.

Neno la Mungu likianza kukuingia vizuri ndani yako na likaanza kufanya kazi, zipo tabia nyingi sana za ajabu ajabu zitaondoka kwako. Ukiona kila siku unasoma Neno la Mungu lakini hubadiliki chochote, anza kujichunguza utaona mapungufu yako yalipo.

Huenda unasoma Neno la Mungu kwa mazoea ili watu fulani wakuone, uwe na uhakika hapo utakuwa unazuia vitu vingi vya kiMungu kushindwa kukubadilisha. Mungu hashindwi kubadilisha mtu, ila Mungu anataka utayari wa mtu binafsi. Hivi unafikiri Mungu hawezi kukata kiu za walevi wote wa pombe? anaweza kabisa ila ameweka kanuni na taratibu zake za kufuata.

Mtu ameonyesha dharau kidogo kwako, siku nzima inaisha umejaa hasira mpaka wakati mwingine unaanza kupandisha na presha. Huo ni uchanga wa kiroho, mtu aliyekomaa kiroho kitendo kile kingemuumiza ila sio kufika hatua ya kupandisha presha.

Jifunze kujaza maarifa ya Neno la Mungu yanayogusa kila eneo la maisha ya mwanadamu. Hakuna kitabu chochote kilichobeba maarifa yanayogusa maisha ya kiroho na kimwili, isipokuwa kitabu cha Maandiko Matakatifu. Watumishi wote walioandika vitabu, wamefunuliwa mambo mbalimbali kupitia mwongozo wa Neno la Mungu.

Madhara ya uchanga wa kiroho ni makubwa sana, unaweza kuambiwa ulipo sio sahihi hata Neno la Mungu linakataza hilo. Yule aliyekuja kukuambia hivyo, unaweza kumchukia kiasi kwamba amekuambia kitu cha kujinufaisha yeye mwenyewe kumbe ni kwa faida yako.

Ufanyaje sasa ili uweze kuondokana na hali hii? Ni kujitambua kwanini unasoma Neno la Mungu. Jambo lingine la muhimu ni kuhakikisha Roho Mtakatifu anakuwa ndani yako, pasipo Roho Mtakatifu mambo mengi yatakupita kushoto, kwa sababu mambo mengine yanahitaji ufafanuzi wa Roho Mtakatifu.

Hakikisha utoto toto wote unaondolewa na Neno la Mungu, usibaki kila siku unasoma Neno la Mungu alafu huoni mabadiliko yeyote. Kama huoni mabadiliko yeyote ingia magotini kumuuliza Mungu inakuwaje unasoma Neno lake huelewi. Na huna unachokipata cha kukusaidia katika maisha yako ya wokovu, upo kama ulivyokuwa jana.

Ukishaanza kuondoka kwenye uchanga wa kiroho, utaanza kuona unaanza kupunguza vijisababu vya kutokusoma Neno la Mungu. Utaanza kuona mabadiliko ndani yako kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, utaanza kuona moyo wa unyenyekevu ukiwa ndani yako, utaanza kuona hekima inaanza kukuvaa ambapo awali hukuwa nayo.

Vipo vitu vingi sana vizuri utaviona kwako, moyo wa utoaji, moyo wa ibada, moyo wa maombi, moyo wa kusamehe na kuachilia vitu, moyo wa kuwahurumia wengine, moyo wa kujitoa na moyo wa kuchukia dhambi. Vyote hivyo vinaweza kukuvaa na ukaanza kuviishi kama vile ulizaliwa navyo.

Mpaka hapo utakuwa umejiona upo kundi gani, kama bado una tabia ambazo unaona hupaswi kuwa nazo kama mkristo aliyeokoka. Nakusihi uweke bidii ya kuutafuta uso wa Mungu, soma Neno la Mungu kwa manufaa yako mwenyewe. Kufanya hivyo utaona mabadiliko makubwa sana ndani yako.

Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.

Chapeo Ya Wokovu.

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.