Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye atupaye uhai wake bure pasipo kuulipia hata shilingi.
Umesikiliza watumishi wengi sana wakikusisitiza umhimu wa Neno la Mungu, wapo wameimba nyimbo za kukuhimiza usome Neno la Mungu, wapo wamehubiri sana bila kuacha kukuhimiza kusoma Neno la Mungu, wapo walimu wamesimama katika zamu zao kukufundisha mbinu mbalimbali za kuweza kusoma Neno la Mungu kila siku.
Ulivyosikia na ukahamisika kweli, na kuona ndani mwako unasikia kuanza zoezi la kusoma Neno la Mungu. Ulifanya hivyo au uliishia kuhamisika? Na ulivyoanza kusoma Neno la Mungu uliendelea na hilo zoezi au ulishia ile wiki ya kwanza baada ya kuhamasika?
Kipi kinakuzuia wewe usione umhimu wa kusoma Neno la Mungu na unasema umeokoka, wokovu wako utawezaje kuimarishwa zaidi ndani yako ikiwa ndani mwako hakuna msukumo wowote wa kusoma Neno la Mungu.
Unawezaje kutoa huduma nzuri kwa watu ikiwa Neno la Mungu ni mzigo kwako, unawezaje kuwaimbia watu habari njema za Yesu Kristo ikiwa ndani yako una mashaka yanayosababishwa na kutokuwa na Neno la kutosha.
Kusikia unasikia sana kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu, unavyosikia hili jambo unaliona halina maana sana kwako au huwa unalionaje moyoni mwako. Maana kama unasikia kila siku alafu hakuna mabadiliko ya hatua zozote unazochukua, lazima tuanze kuwa na mashaka na wokovu wako.
Haiwezekani wewe kila siku unaambiwa kusoma Neno la Mungu kuna faida kubwa kwa mwamini mwenye safari ya kwenda mbinguni. Lakini wewe wala hushtuki chochote ndani yako, tena upo tayari kusoma vitabu vingine ila sio biblia yako. Ulichobakisha kwenye biblia yako ni kuibeba kila siku za jumapili, na kwenda kufungua ule mstari utakaoambiwa na mchungaji/askofu/padrii ufungue.
Hebu leo jihoji ndani yako, je unajihisi upo salama ikiwa ndani yako husikii msukumo wowote wa kutenga muda wako kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu? Utawezaje kulikwepa hili la dhambi ikiwa unaona kuokoka kwako imetosha.
Rejea; Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Zaburi 119:11 SUV.
Moyoni mwako umeweka kitu gani hicho ambacho kimechukua nafasi ya Neno la Mungu, ikiwa ni mke/mume wako, ikiwa ni mchumba wako, ikiwa ni biashara zako, ikiwa ni cheo cha kazini kwako, ikiwa ni walezi/wazazi wako, ikiwa ni watoto wako. Je hao wote wataweza kukusaidia usitende dhambi? Je hao watakusaidie kukutetea hadi ile siku ya hukumu? Je mali zako ndizo zikazoweza kukusaidia usitupwe jehanamu?
Chakula chako pekee cha kiroho ni Neno la Mungu, ikiwa hukitumii unafikiri utakuwa na hali gani kiroho mpaka sasa. Tangu uokoke mpaka sasa unajua unaenda katika njia ikupasayo kuenenda au utakuwa umetoka nje ya mstari ila unajifariji upo vizuri. Ni nani atakayeweza kukuelekeza kila siku njia iliyo sahihi, ikiwa wewe mwenyewe hutaki kusoma Maandiko Matakatifu ya kukusaidia kuifuata njia sahihi.
Kanisani unakuwa na mchungaji, anakupa machache maana muda wenyewe hutoshi, tena wakati mwingine hasomi Neno la Mungu anaongea ya kwake. Unafikiri kwa jinsi dunia hii ilivyojaa uovu, utaweza kujiendesha mwenyewe pasipo kuingia kwenye mitengo ya shetani?
Utaachaje kutenda dhambi ikiwa umepungukiwa silaha muhimu ambayo ni Neno la Mungu, kipi utakikwepa kwako. Kila siku unasikia soma Neno la Mungu ni muhimu sana kwako, unaanza kwa moto na mbwembwe nyingi baada ya muda mfupi unaishia njiani. Nani unamkomoa? Bila shaka ni wewe unajikomoa.
Huenda hapo ulipo ulikuwa unasoma Neno la Mungu ila moyoni mwako unapanga kusitisha hilo zoezi, unafikiri ikiwa utaacha kula chakula cha mwili utaendelea kuishi au utakuwa mwisho wa maisha yako. Iweje Neno la Mungu isiwe zaidi ya chakula cha mwili? Kama ilivyo umhimu kula chakula cha mwili, ndivyo ilivyo muhimu kula chakula cha KIROHO.
Najua umeambiwa sana, najua umesikia sana kuhusu umhimu wa kusoma Neno la Mungu. Baada ya hayo yote umefanya nini, au umeona sehemu unayosali ni salama basi haina haja ya kusoma Neno la Mungu. Jambo la Kujiuliza umewahi kuona mchungaji wako amekusomea angalau sura moja ya kitabu chochote kile? Kama amewahi ilikuwa mara ya mwisho lini?
Ufike wakati uamke usingizini, acha mazoea ya kuona kila kitu ni kawaida kawaida. Yapo makosa mengi tunafanya tukifiri tupo sahihi, kumbe tunapotea njia. Na hii yote ni kwa sababu tumekosa dira yetu ambayo ni Neno la Mungu.
Inawezekana ukajipa sababu kuwa hujawahi kuambiwa umhimu wa kusoma Neno la Mungu, huenda umeokoka siku za karibuni. Ila kupitia ujumbe huu utakuwa umeelewa ninachokisema, huna kisingizio tena kuhusu hili jambo. Utapaswa kusoma Neno la Mungu kwa bidii zote, usihamasike alafu kesho ukabaki na simulizi za nilikuwaga nasomaga Neno la Mungu. Ukiulizwa kwa sasa mbona husomi unaanza sababu elfu, kwanini usiwe na sababu za kuendelea kusoma Neno la Mungu badala yake una sababu za kuacha kusoma Neno la Mungu.
Achana na habari za kusikiliza kila siku kusoma Neno ni muhimu, anza LEO kusoma Neno la Mungu. Acha kujidanganya na mazingira uliyopo, anzia hapo hapo ulipo, jiwekee ratiba usiyoweza kuivunja.
Mpaka hapo kuna kitu utakuwa umekipata kupitia ujumbe huu, kile umekipata usiache kukifanyia kazi. Utaona mabadiliko makubwa katika maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma makala hii, endelea kutembelea ukurasa wetu wa Chapeo Ya Wokovu kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Imeandaliwa na Samson Ernest.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.