Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena njema kabisa machoni pa Bwana ameona vyema kutupa kibali kingine cha kuiona leo. Sifa na utukufu tumrudishie yeye Bwana mwenza wa yote, kutupa fursa hii adimu kwetu.
Kila jambo lina hatua zake, na mpaka kufikia hizo hatua lazima kuna changamoto utapitia ndipo uweze kueleweka vizuri. Mwanzo siku zote una changamoto zake ngumu, ila ukiwa umedhamiria kufanya na kukiishi kile unaamini ni kitu ambacho kitaendelea kuimarisha uhusiano wako na Mungu, kifanye kwa bidii zote.
Mwanaume umewahi kufikiri kwanini unapopenda jambo fulani na mke wako anakipenda hicho kitu, hasa hasa kama unaonyesha upendo kwa mke wako. Bila yeye kujielewa anajikuta anakipenda sana kile ambacho wewe unakipenda kukifanya, na atakuwa tayari kukisimamia kwa uwezo wake wote.
Ndivyo unavyoweza kumfanya mume/mke wako apende Neno la Mungu, ukibadilika wewe na Neno la Mungu likawa ndio chakula chako cha kila siku. Na mwenzi wako akazidi kuona mabadiliko makubwa kwako, ambayo mabadiliko hayo yanazidi kukutofautisha na yeye. Ipo hofu itaanza kujengeka kwake kuhusu wewe.
Upo uwezekano mwanzo wakati unasoma Neno la Mungu, alikuwa anakupinga na kukuvunja moyo. Usipovunjika moyo, ipo siku akikuona umeacha kusoma Neno la Mungu atakuuliza mbona siku hizi umeacha kusoma Neno. Usishangae akawa mkali juu ya hilo, maana anajua wakati unasoma Neno la Mungu kuna vitu alikuwa anavipata kutoka kwako.
Wakati mwingine anaweza asikuambie mke/ mume wangu upo makini na mambo ya Mungu, ila akiwa na wenzake huko nje hataacha kuwashuhudia habari zako. Juhudi zako kujifunza Neno la Mungu zinaweza kuzaa matunda kwa mwenzi wako, ile ile mbegu ikaenda mpaka kwa watoto wako.
Neno La Mungu lina kila maelekezo ya maisha yako, unavyozidi kujifunza Neno la Mungu ndivyo unavyozidi kupata mbinu za kumwondoa mwenzako kwenye hali ya kutopenda mambo ya Mungu. Na kumfanya akaanza kumpenda Mungu kupita hata wewe.
Usishangae siku moja akakuambia nakushukuru mke/mume wangu, umenifanya nimeacha mambo mabaya ya dunia hii. Na sasa namwona Mungu kwa viwango vya tofauti sana, yote hii ni wewe kutokubali kukata tamaa pale unapokutana makwazo.
Ukisimama vizuri na Mungu wako mama/dada, hata kama una mume mkali kiasi gani. Nakwambia kama kweli huna michanganyo ya dunia na wokovu, atafika kipindi ataanza kuogopa kukusemea maneno mabaya. Hii yote ni kujua ahadi za Mungu kwako na kuzifanyia kazi, utaenda mbele za Mungu kumwombea mume wako kwa mzigo mzito moyoni, kwa sababu unajua Mungu anaweza.
Itakuwa mbaya kama mke/mume wako haoni mabadiliko kwako, hata kama asipokuambia yeye anajua mke/mume wangu yupo vizuri. Yapo mambo yasiyoonekana kwa macho ya nyama, ila wewe unaweza kumsaidia mume/mke kwa kumweleza anachofanya sio kizuri hata kama anajua hujamkuta anafanya.
Uwezakano upo kwa mume/mke wako anakufanyia vitendo viovu kwa kuvunja heshima ya ndoa yenu kwa siri bila wewe kujua. Ukifikiri hawezi kufanya hivyo kwa sababu mnaenda wote kanisani, kumbe mwenzako kanisani ni mwavuli tu wa kujifichia.
Sio kila uvivu wa kutopenda Neno la Mungu ni uvivu wa kawaida, uvivu mwingine unaletwa na dhambi. Dhambi inaondoa kiu ya mambo mengi ya Mungu, unaweza kumwona mtu anafanya kitu/jambo si kwa sababu anajenga uhusiano wake na Mungu. Mwingine anataka aonekane kwa wengine amefanya basi, ila moyoni mwake anajua kabisa hayupo sawa.
Umepata Neema ya kumjua Mungu, na mwenzi wako bado hana mwelekeo wowote? Usichoke kumwombea. Na usiache Juhudi zako za kusoma Neno la Mungu, uwe na uhakika Neno la Mungu litakupa hekima ya namna ya kuishi na mwenzako.
Huwezi kuwa na kero ambayo itaanza kumfanya mwenzako aanze kujiuliza kama wokovu wenyewe ndio huu, bora uendelee nao mwenyewe. Utakuwa mfano mzuri ndani ya moyo wake, hata kama shetani atamtumia kukuzuia baadhi ya vitu. Uwe na uhakika Mungu atakupa Neno la maarifa namna ya kuweza kuendana naye, hilo Neno ndilo litakalomfanya akuone ni mtu wa pekee sana kwake.
Bila shaka lipo jambo umejifunza kupitia ujumbe huu, usije ukaacha bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu, hii ndio lengo kuu ya kukuandikia haya.
Mungu akubariki sana kwa kutoa muda wako kusoma ujumbe huu, endelea kutembelea ukurasa wetu CHAPEO YA WOKOVU kwa masomo mengine mazuri zaidi.
Imeandaliwa na Samson Ernest.
Chapeo Ya Wokovu.
chapeo@chapeotz.com
+255759808081.